28 February 2011

Mradi wa bil 1/- wajengwa kwa Mzindakaya

Na Juddy Ngonyani,Sumbawanga

WAKAZI wa vijiji vya Nkundi na Fyengeleza vilivyopo katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wataanza kunufaika na maji safi na salama  baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa bwawa la Kawa ambalo ujenzi wake upo katika hatua za mwisho kumalizika kwenye eneo la aliyekuwa mbunge wa Kwela, Bw. Chrisant Mzindakaya.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo wa ujenzi wa bwawa la Kawa Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji, Bw. Frida Rweyemamu alisema kuwa ujenzi wa bwawa hilo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni moja ikiwa ni mikakati ya wizara hiyo ya kuwaondolea  wananchi kero ya maji.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne ijayo.

Licha ya serikali kutumia fedha nyingi katika mradi huo utakaowaondoa wananchi katika kero kubwa ya maji, wananchi hao wamedai hawakuwa na taarifa sahihi juu ya serikali kuanzisha mradi huo katika eneo la shamba hilo.

Bw. Manfredy Mpepo, Bi. Costansia Lingamila, Bw. James Ntalwila walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakisikia kuwa katika shamba la mwekezaji huyo kuna bwawa la maji linajengwa wakidhani ni la kwake kwa ajili ya matumizi yake na wanyama wake.

Lakini Bw. Chrisant Mzindakaya alisema kuwa mradi huo unajengwa katika eneo lake baada ya wataalamu wa maji kutafiti na kuona kuwa eneo hilo linafaa kwa ajili hiyo lakini maji yatatumiwa na wananchi wote wa vijiji hivyo.

Alisema kuwa kitendo cha wananchi kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu mradi huo ni ukiritimba wa viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wanasiasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Nkasi, Bw. Peter Mizinga licha ya kukiri kuwa mradi huo haujawahi kujadiliwa katika vikao vya baraza la madiwani, alisema kuwa watatembelea mradi huo kwa kuwa una manufaa kwa wananchi wao.

Kwa upande wake mkandarasi kutoka kampuni ya Nyakilanyangi, Bw. Mautha Nyakilanyangi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa bwawa hilo alisema kuwa mradi huo upo katika hatua za mwisho kukamilika.

No comments:

Post a Comment