09 February 2011

Matokeo uchaguzi mkuu yahojiwa bungeni

Na Kulwa Mzee, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvi amesema hakuna uchakachuaji uliofanywa na CCM katika
Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana na vyama vyilivyoshindwa sera zao zilikataliwa na Watanzania hivyo waziweke kabatini wasubiri mwaka 2015.

Waziri alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chambani, Bw. Salim Hemed Khamisi (CUF) aliyesema kwamba wapiga kura walijitokeza wachache, hivyo taarifa za matokeo ya uchaguzi zitakuwa zimechakachukuliwa na migomo inayoendelea inaonesha Watanzania wamechoshwa na CCM, hivyo kuna kila sababu ya chama hicho kuachia ngazi.

Akijibu swali hilo alisema suala la wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi halihusiani na CCM, hivyo ni wajibu wa kila chama kushirikiana kuhamasisha wananchi kupiga kura.

"Hakuna chochote kilichochakachuliwa, yeyote aliyeshindwa hawezi kukosa visingizio, kama tunafuata demokrasia, CCM imeshinda kihalali," alisema na kuongeza kwamba walioshindwa sera zao ambazo Watanzania walizikataa waziweke kabatini hadi mwaka 2015.

Akijibu swali lingine la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe (CHADEMA) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuunda tume huru na si kuiachia Tume ya Uchaguzi kwani ilikiuka utaratibu halali katika uchaguzi.

Bw. Lukuvi alisema kweli CHADEMA ililalamikia hilo, tume ya Uchaguzi itatoa taarifa ya tathmini ya uchaguzi kuonesha jinsi uchaguzi ulivyokuwa wa huru na haki.

Waziri huyo awali alijibu swali la msingi lililoulizwa na Bw. Khamisi ambapo alitaka kujua Serikali inatathmini vipi mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi, hatua gani zitachukuliwa ili uchaguzi uje kuwa bora zaidi.

Alisema baada ya uchaguzi tume iliendelea kufanya tathmini kuona kwamba uchaguzi ulifanyika vizuri, isipokuwa zipo changamoto zilizojitokeza miongoni mwake ni wapiga kura kujiandikisha au kwenda kurekebisha taarifa zao siku za mwisho na kusababisha msongamano.

Pia vituo vya kupigia kura kuwa mbali na wanakoishi, mwitikio mdogo wa wananchi ambapo zaidi ya asilimia 57 ya Watanzania wenye sifa hawakupiga kura, baadhi ya vyama vya siasa kutozingatia maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni na kutokuwepo na chombo cha kuratibu na kusimamia elimu ya mpiga kura.

Hatua zitakazochukuliwa alisema ni kurekebisha sheria inayohusu uchaguzi kwa kuzihuisha sheria za gharama ya uchaguzi ya mwaka 2010 na sheria namba moja ya mwaka 1985.

Kuweka mikakati ya kutoa elimu ya uraia, kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura, kutumia teknolojia rahisi na sahihi katika mchakato wa uchaguzi.

3 comments:

  1. William Lukuvi, jitahidi usome magazeti na maandiko mbali mbali kabla hujakurupuka kujibu swali bungeni.

    Kuna maandiko mengi tu yanayoonesha hesabu kamili za kura zilizopigwa na ushindi wa kila mgombea. Zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi ni za kwao wenyewe kwa maslahi ya JK na CCM yake.

    Mimi ni mwuungwana sana, nitafute kwa email hii: najaribu@gmail.com nikutumie matokeo sahihi kabisa. Upo hapo William?

    ReplyDelete
  2. jamani mamboyenu ya uchaguzi hatuyataki kusikia sasa simuandamane tu kama hamridhiki na serikali iliyopo madarakani muone nyie vibaraka wa chadema kama mtapata watu?wabishi tu kama viongozi wenu upeo mdogo hata kama mmesoma

    ReplyDelete
  3. Wadau hawaelewi. wanajichanganya hao chama cha mafisadi. chadema ndo chama chenye wasomi waliobobea,ndo maana wakapata viti vyote vya mjini,ambako ndo kwenye wasomi.vijijini wamepata kwa kuwa waliweza kuiba huko.mjini walisimamiwa kidete.huyo raisi ni wa vijijini,kura za mjini ni za chadema,vijijini waliojua wizi ndiko kapata.tupambane kwa ailimia uone.chadema ndo chama kilifanya kweli uchaguzi huu.watu tadhmini kwanza.

    ReplyDelete