10 January 2011

Mnyika aendelea na mchakato wa hoja

Na Gladness Mboma

MBUNGE wa Ubungo, Bw. John Mnyika ameamua kuendelea  kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu katiba kama alivyokusudia kutokana na serikali kuacha kutoa ufafanuzi wiki moja baada ya mwito wa kutakiwa kufanya
hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Bw. Mnyika alisema kutokana na Rais Jakaya Kikwete na serikali yake kuacha kutoa ufafanuzi kuhusu hoja binafsi wiki moja baada ya mwito wa kutakiwa kufanya hivyo inaonyesha bayana kwamba hakuna mpango wa kuhusisha umma.

"Inaonyesha bayana kwamba hakuna mpango wa kuhusisha umma kuanzia hatua za awali katika mchakato kupitia kuwasilisha hoja au muswada bungeni ili kuwekwa mfumo wa kisheria wa kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa kuandikwa kwa katiba mpya," alisema.

Alisema ushahidi kuhusu serikali yake kutokuwa na dhamira ya kuandika katiba mpya inayohusisha umma na badala yake kuendeleza kuhodhi ya serikali ambayo inaweza kusababisha mapitio yenye kasoro zile zile za miaka yote, ni kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mwaka mpya mbele ya mabalozi.

Bw. Mnyika alisema kwenye hafla hiyo Rais Kikwete amerudia tena kauli ya kuunda moja kwa moja tume ya kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa maoni bila kuhusisha bunge katika hatua za msingi.

"Baada ya kauli niliyotoa ya kutaka ufafanuzi na matamko yaliyotolewa na wadau mbalimbali ya kueleza kasoro za hatua ya Rais Kikwete ya kutaka kuunda tume nilitarajia kwamba katika kauli yake ya kwanza kabisa ya mwaka huu angetumia fursa hiyo kufafanua suala husika, ikiwemo kueleza kusudio la kupeleka mapendekezo ya mchakato bungeni," alisema.

Bw. Mnyika alisema kuwa hiyo inadhihirisha kwamba Rais Kikwete anataka katiba mpya kwa maneno tu, lakini haonyeshi kwa vitendo kuwezesha mchakato husika kwa kuushirikisha umma kwa ukamilifu.

Alisema kutokana na maoni aliyopokea na utata wa kauli za serikali kuhusu mchakato wa katiba mpya, anaendelea kukamilisha taratibu za kuwasilisha hoja binafsi kwenye bunge la Februari kuhusu mchakato wa katiba mpya, na tayari alikwishawasilisha taarifa ya hoja Desemba 27 mwaka jana.

Mbunge huyo alisema kutokana na mjadala unaoendelea inaonekana bayana kwamba bado iko haja ya suala hilo la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea Ibara ya 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni ya umma.

Pia kuwa serikali inafanya kazi kwa niaba na bunge ambalo ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63 (2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

2 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWAJanuary 10, 2011 at 9:17 AM

    Kaka Mnyika,CCM hawana dhamira ya Katiba mpya.akawetu sisi wanasheria,Tume ya Katiba haihusiki na kuundwa kwa Katiba mpya.Chombo pekee kinachohusika na uundwaji wa Katiba ni Mkutano wa Katiba.Kuna hatari ya kutokea yale yaliyojiri nchini Kenya mara ya kwanza kwenye upigiaji kura wa Rasimu ya Katiba.Ikumbukwe kuwa Rais Mwai Kibaki aliteua kamati yake(kama anavyotaka kufanya Rais Kikwete)iliyoandaa Rasimu ya Katiba.Ile ilikuwa Tume,si mkutano wa Katiba.Kampeni kali za kiupinzani zilifanywa.Akina Kibaki wakiwa upande wa ndio(ndizi) na akina Odinga upande wa hapana(chungwa).Upande wa chungwa ukashinda.Kwanini? Ulishinda kwakuwa Rais Kibaki alienda kinyume na utaratibu wa kuandika Katiba mpya.Huo ndio ukawa mwanzo wa vyama vya ODM(Orange Democratic Movement) na ODM-Kenya.Nasi tunaelekea huko.Mh.Kikwete anatuongozea huko.Tusikubali.Nasisitza kuwa CCM hawana utayari wa Katiba mpya...wanafanya usanii mtupu.Ni wa kuwaogopa kwa kila kauli yao na matendo yao.

    ReplyDelete
  2. Katika maoni tunayotoa kuelekea katiba mpya ni vizuri chuki na hasira tuviweke pembeni tujadili mustakabali wa Taifa letu.

    Kina John Mnyika waacheni watuoneshe njia, na njia sahihi tutaifikia. Kikubwa serikali iandae njia itakayokubalika na Watanzania walio wengi katika kuandaa rasimu ya katiba mpya.

    Tanzania ni yetu sote, hivyo haki ya mabadiliko ya katiba na ridhaa yake lazima itokane na watanzania wenyewe.

    Kipo kikundi cha watu wachache hasa wanaoneemeka na katiba hii ya sasa, Muda wa mabadiliko umewadia na hatuna jinsi ni kuacha hali halisi ichukuwe mkondo wake wenyewe kwa salama. Ikiwa tutazuia ni lazima njia hiyo itafanyika kwa nguvu ya walio wengi. Sasa tusifike huko kwani huko ndiko kwenye vurugu zaidi.

    Serikali ibebe jukumu lake kuongoza maandalizi ya Rasimu ya Katiba mpya Tanzania kwa kuandaa mazingira shirikishi kwa kila mtu bila kujali chama anachotoka, kanda kabila au dini ya mtu.

    Watanzania bado ni wamoja wanauwezo wa kujadili mambo yao kwa amani na utulivu.

    ReplyDelete