26 January 2011

Chelsea yazinduka yaichapa Bolton 4-0

BOLTON, England

BAO safi lililofungwa na mshambuliaji, Didier Drogba usiku wa kuamkia jana liliifanya timu ya Chelsea kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Bolton
na kuwafanya mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo ya Ligi Kuu England, kupata ushindi wake wa kwanza mnono tangu Oktoba mwaka jana.

Drogba alipachika bao hilo kwa shuti kali akiwa umbali wa yadi 33  lililomshinda mlinda mlango, Jussi Jaaskelainen dakika ya 11 ya mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa  Reebok.

Wachezaji wenzake, Florent Malouda aliipatia bao kwa mkwaju mkali dakika 41, Nicolas Anelka akapachika bao jingine kwa shuti la guu la kushoto dakika ya 56 na Ramires, akaongeza jingine ambalo ni bao la kwanza kwa Chelsea dakika ya 74.

Kwa matokeo hayo, Chelsea ambayo wiki iliyopita iliifunga Blackburn  inaonekana kushinda mechi mbili kwa mfululizo kwa mara ya kwanza tangu ilipoifunga Wolves Oktoba 23, mwaka jana na kisha ikaichapa Blackburn siku saba baadaye ushindi ambao ulikuwa ni wa mwisho katika michuano ya ligi.

Pamoja na ushindi huo mnono, Chelsea bado ipo nyuma kwa pointi saba dhidi ya vinara Manchester United huku ikiwa inaendelea kushika nafasi ya nne wakati ikiwa imecheza mechi moja zaidi.

Didier ametupeleka mbali kwa kuwa na mwanzo mzuri kwa kufunga bao ambalo  pengine ndilo bora kwa msimu huu hadi sasa na sisi tumefanya kazi kweli kweli, yote ikiwa ni juu ya kutaka kuondoka na ushindi," alisema nahodha wa Chelsea, John Terry. "Tuliwazuia  Bolton kucheza na wakawa wakifanya kazi kwa ajili yetu," aliongeza.

No comments:

Post a Comment