23 December 2010

Ngeleja atetea umeme kupanda

*Asema lengo si kutafuta malipo ya DOWANS

Na Rose Itono
WAZIRI wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja ametetea kupanda kwa bei ya umeme kuwa ni kutokana na kupanda kwa gharama za endeshaji na si kulipa fidia ya kampuni ya Dowans kama inavyodaiwa.Juzi Shirika la Umeme nchini (TANESCO) lilipata
baraka za Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (UWURA) kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari Mosi, hatua ambayo imelalamikiwa na wadau, huku baadhi wakidai huenda inakusanya fedha za kulipa deni la Dowans.

Dowans ilishinda kesi katika Mahakama ua Usuluhishi ya Kimataifa kuwa inakiwa kulipwa dola milioni 69 na TANESCO kutokana kuvunjwa kwa mkataba baina yake, uliorithishwa na Richmond Development LCC, wa kuzalisha umeme wa dharura. Akizungumza jana Dar es salaam alipotembelea ofisi za EWURA, Waziri Ngeleja alifafanua kuwa bei zilizokuwa zikitozwa na TANESCO zilikuwa hazikidhi gharama za uendeshaji, na kulifanya shirika kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Alisema kuwa, hata Desemba 2007 EWURA ilipitisha bei za umeme kwa TANESCO baada ya kulitaka Shirika hilo kuwasilisha taarifa kuhusu gharama halisi za huduma ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini. Alisema hukumu juu ya Dowans na serikali imetolewa Novemba mwaka huu wakati TANESCO imeshapeleka mapendekezo juu ya bei mpya ya umeme EWURA.

Alisema baada ya kupokea maombi la TANESCO Mei 28, 2010, EWURA ilifuata taratibu zote za kisheria kuchambua na hatimaye kufikia maamuzi.
Bw. Ngeleja alisema umeme utaongezeka kwa wastani wa asilimia 18.5, na akawataka wananchi kuelewa maamuzi hayo. Alisema gharama hizo mpya zitaanza kutumika Januari mosi na kuongeza kuwataka wananachi kuonyesha ushirikiano kwa hilo ili kuliwezesha Shirika hilo liweze kujiendesha.

Bw. Ngeleja alisema pamoja na shirika hilo kupandisha gharama hizo suala la kuwepo kwa mgawo wa umeme litakuwa likiendelea, na kasi ya mgawo itakuwa ikipungua siku hadi siku.Waziri alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inamaliza kabisa kuwepo kwa tatizo la mgawo wa umeme ndani ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Bw. Haruna Masebu, kiwango hicho cha asilimia 18.5 kitakachoanza kutozwa na TANESCO Januari Mosi, mwakani ni karibu nusu ya ongezeko lililoombwa na TANESCO la asilimia 34.6.

Bw. Masebu naye wakati anatangaza ongezeko hilo alitetea gharama hizo akisema kuwa wamefikia uamuzi huo bila kupendelea upande wowote na kwa kuzingatia mawazo yaliyotolewa na wadau wakati wa kujadili maombi ya shirika hilo."TANESCO waliomba ongezeko la asilimia 34.6 lakini baada ya kuangalia kwa makini gharama zao za uendeshaji na kwa kuzingatia mawazo ya wadau ambao walishirikishwa, tulifikia uamuzi wa kukubali ongezeko la asilimia 18.5 ili shirika liweze kujiendesha na hatimaye kutoa huduma nzuri kwa wananchi," alisema Bw. Masebu.

Alisema kuwa baada ya kupata maombi hayo, waliyaangalia kwa kina na ilionekana kuwepo kwa hoja ya msingi, lakini haikukubaliwa kama ilivyowasilishwa.Kulingana mambo hayo, TANESCO iliomba kuongeza bei ya umeme kwa kipindi cha miaka mitatu kwa maana ya asilimia 34.6 kwa mwaka 2011, asilimia 13.8 kwa mwaka 2012 na asilimia 13.9 mwaka 2013.

Kuhusu mambo hayo ya miaka miwili iliyobaki, Bw. Maseru alisema kuwa wataangalia baada ya suala hilo kufanyiwa utafiti wa kutosha na mtaalamu atakayependekezwa na EWURA hapo kufanyika na kumalizika mwakani.

EWURA iliitaka TANESCO kuhakikisha inafungua akaunti maalumu zikiwemo za matengenezo na marekebisho, mpango wa uwekezaji wa mtaji, mpango wa gharama za kukunua umeme unaozalishwa nje.Masharti haya yanalenga kudhibiti mapato ya TANESCO ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa kila mpango zinatumika kama ilivyokusudiwa, na akaunti hiyo itakaguliwa kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza kuhusu hali ya uzalishaji umeme jana, Bw. Ngeleja alisema ufungaji wa transfoma ya Kipawa ulikamilika jana, hali itakayopunguza tatizo la mgawo kwa wakazi wa maeneo hayo.Mbali na suala la umeme, Bw. Masebu alimweleza Waziri Ngeleja kuwa mpaka sasa wamedhibiti suala la uchakachuaji wa mafuta kutoka asilimia 78 hadi asilimia 40 Juni 2010.

Hata hivyo, Bw. Masebu alisema EWURA inakabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na ukosefu wa uhakiki na ubora.

3 comments:

  1. Ngeleja anamdanganya nani iwapo umma unajua kuwa ufisadi ndicho chanzo kikuu cha kupanda gharama za umeme? Kwanini hawasemi kweli kuwa serikali ndiyo chanzo cha yote kutokana na kutumia vibaya umeme na isilipe ukiachia mbali kuleta wawekezaji wezi wanaoshirikiana na wakubwa wa serikali kama ilivyotokea kwa Richmonduli-Dowans ambazo ni za vigogo wake?
    Tuombe Mungu umeme uzidi kupanda ili wananchi waamke na kuitia adabu serikali hii fisadi na sanii.

    ReplyDelete
  2. mie hata sikuelewi ngeleja, nakuona kama haupo focused and inawezekana huwa unaongea bila kuwa na details, anyway last time ulitutangazia kuwa mgoa wa umeme sasa ni basi - hasa baada ya kusikia kuwa mh.kafulila ataleta hoja binafsi, na katibu mkuu wako akatao deadline ya siku 6 badala ya 12 waliyosema wataalamu kuwa tatizo la mgao litakuwa limekwisha, ila from there naona ni yale yale, sasa siwezi amini iwapo kuongezeka kwa gharama za sasa si uhusiono na issue ya dowans?

    ReplyDelete
  3. Chonde chonde dogo Ngereje, usituangushe vijana watanzania kwa kuanza kupiga siasa wakati ni kipindi cha utendaji. Wewe kijana lakini huonekani kabisa kuwa mzalendo. Ikiwa ni hivyo huwezi kufika kokote kwa kuwe wewe si mzalendo tena. Ni lazima uelewe kwamba matatizo ya Tanesco ni ufisadi uliotawala kwenye shirika hilo. Mikataba ya kifisadi, wakubwa na makampuni makubwa kushindwa kulipa bills zao. Policy mbovu zinazodhoefisha shirika kwa sababu wakubwa wanalitumia kutengeneza tenda za ajabu ajabu ili wapate faida kwenye biashara zao. Wakubwa wa Tanesco kulitumia shirika kwa manufaa yao. Matokeo shirika linakuwa mahututi wanapeleka mzigo kwa maskini wanyonge. Chonde chonde jamani muwe na huruma na wananchi maskini. Tunaomba sana mkusanye madeni kwenye mashirika na tasisi za serikali kama magereza, majeshi kwani hao serikali huwapa bajeti zao za kulipa umeme lakini hawataki kulipa kwani wakubwa wanakura fedha zake na pamoja na wenye viwanda wajanja wasiotaka kulipa bills zao. Mkikusanya madeni yote shirika la Tanesco halitakuwa na haja ya kuwapa mzigo wananchi maskini. Msifanye deal na wafanyabiasharaa kwa kuweka mikataba ya ajabu ajabu ili kulikomoa shirika mhimu kwa uchumi wa nchi. Jamani ifike mahali watanzania tuiondoe serikali ya dharimu ya CCM. Serikali inayonyonya wananchi wake bila huruma haifai hata kidogo.

    Ngereja onyesha uzalendo wako katika jambo hili tafadhari vinginevyo utaonekana umeshindwa kazi ama hufai kuingia kwenye siasa kwani huna uzalendo kwa nchi yetu na wananchi wake.

    ReplyDelete