29 December 2010

Ngeleja abeza msimamo wa TUCTA

Na John Daniel

WAZIRI wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja amekejeli tishio la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), kutaka kuandamana kupinga ongezeko la bei ya umeme na kueleza kuwa Watanzania si wajinga kuburuzwa na watu wenye
maslahi binafsi.

Alisema kiwango cha juu kilichoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (UWURA) ni sh. 28 kwa kila uniti moja katika matumizi ya kawaida, kiasi ambacho kwa mujibu wa Bw. Ngeleja si kikubwa kama inavyotafsiriwa na TUCTA na baadhi ya watu.

Kwa kiwango hicho, mteja wa TANESCO alikuwa anatumia uniti 100 za umeme kwa mwezi, kuanzia Jumapili atalazimika kutoa sh 2,800 zaidi ya bei aliyokuwa anatoa awali.

"Nilichoelewa ni kuwa TUCTA walikurupuka kutoa kauli bila kujua ukweli wa kiwango gani kilichoidhinishwa, kilichoongezeka kwa kila uniti ni sh. tano, sh. tisa, sh. 11 na kiwango cha juu kabisa ni sh. 28, kutegemea na aina ya matumizi.

“Hivi ni nani akipewa sh. 28 anaweza kununua chochote kwa dunia ya leo, wasidhani Watanzania ni wajinga wanaweza kuburuzwa tu na fikra binafsi za watu kujitafutia umaarufu hapana tutafute ukweli jamani," alihoji Bw. Ngeleja.

Alisema TANESCO iliomba ongezeko hilo kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na kwamba mara ya mwisho bei hizo ziliongezwa Januari 2008.

"Serikali kwa maana ya TANESCO inatambua uwezo wa wateja wake ndio maana inajitadi kubeba sehemu kubwa ya gharama za umeme, ukiangalia tangu mwaka 2008 bei ya vitu ikiwemo mitambo imepanda kwa kiasi kikubwa," alisema Waziri Ngeleja.

Tanesco ilikuwa imeomba ongezeko la asilimia 34.6 lakini EWURA baada ya kusikiliza hoja za wadau ikapitisha asilimia 18.5.Wakati huo huo TANESCO imetoa taarifa inayoonesha mchanganuo wa ongezeko la bei mpya ya umeme kwa watumiaji kulingana na matumizi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kundi la watumiaji wadogo majumbani (D1) itapanda kwa sh. 11 kwa uniti moja hivyo kuwa sh. 60 kwa uniti badala ya sh.49 za awali.

Kundi la watumiaji wa kawaida (T1) ambao ndio wamepanda zaidi watalipa sh 157 kwa uniti moja kutoka sh. 129 za awali, sawa na ongezeko la sh. 28 kwa uniti moja.

Taarifa hiyo ya TANESCO imetaja kundi la mahitaji ya juu ya msongo mdogo (T2) kuwa na ongezeko la sh. tisa kwa kila hivyo na kufikia bei ya 94 kutoka sh. 85 za awali.Kundi la mahitaji ya juu ya msongo mkubwa (T3/T3a) ongezeko ni sh. tano kwa uniti, hivyo kupanda kutoka sh. 79 ya awali hadi sh. 84.

Kundi la mwisho linalohusu Tanzania visiwani (T5/T3b) ongezeko ni sh. nane kwa uniti moja hivyo gharama zitapanda kutoka sh. 75 hadi 83 kwa kila uniti moja.Wiki iliyopita Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nicholas Mgaya, aliitaka Serikali kufuta uamuzi wa kupanda kwa bei ya umeme na kutishia kuandaa maandamano ya amani nchi nzima kupinga hoja hiyo.

Bw. Mgaya alisema Kamati ya Utendaji ya TUCTA ilifikia maamuzi hayo kwa maelezo kuwa ongezeko hilo ni kubwa na haliendani na hali ya Mtanzania na hivyo litazidisha ugumu wa maisha kwa wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.

9 comments:

  1. Ama kweli mambo yamebadilika Zamani ongezeko la bei linaangalia yule wa kima cha chini (kawaida) inaongezwa asili,ia ndogo, siku hizi yeye inakuwa asilimia kubwa Kwa sasa kuna ongezeko la sh 5 mpaka 28 Watumiaji wakubwa ni sh 5 watumiaji wa kawaida sh 28 Jamani tuhurumiane

    ReplyDelete
  2. Mimi nadhani viongozi wa TUCTA wako sawa kama kima cha chini cha mshahara ni laki moja na nusu ukiongeza bei ya umeme umeongeza bei ya kila kitu. Ingekuwa ni umeme tu umepanda watu wangekubali ila kila kitu kimepanda gharama mara tu baada ya uchaguzi. Je Mtanzania wa kawaida ataweza kumudu hali hii?
    Ukiangalia Mtanzania wa kima cha chini ndiye anayetakiwa kulipa zaidi kuliko anayetumia umeme meingi Je huu ni uungwana? Inasikitisha sana kuona hali kama hii kila kitu Tanzania kimekuwa shaghala baghala ni heri kutawaliwa na mkoloni kuliko kuwa mtumwa chini ya mtanzania mwenzako. INASIKITISHA na INAUMA SANA.
    Watanzania tuamke.

    ReplyDelete
  3. kama waziri anaona ongezeko la umeme si tatizo wangeliweka ndani ya ilani yao ya uchaguzi ili kupata kuungwa mkono na wananchi...

    ReplyDelete
  4. Nadhani waziri Ngeleja anachosema ni kwamba watanzania ni wajinga wa kuburuzwa tu na kwamba hiyo ndio sera ya CCM. Ila akumbuke mwisho wa CCM unakuja soon. HUWEZI PANDISHA BEI YA UMEME ILI UPATE KUWALIPA KINA ROSTAM,LOWASSA,IDRISSA,MKONO BILIONI 185!Halafu unasema MAISHA BORA KWA KILA MTU! Semeni maisha bora kwa viongozi wa CCM kwa kutumia ujinga wa watanzania. Kila la kheri ngeleja!

    ReplyDelete
  5. kama ngereja anaona gharama ni ndogo basi wizara yake iwajibike kwa hizo gharama,hivi itakuwaje mwanachi ndo apewe gharama ya kulipa dowans kwa ongezeko la umeme,jamani CCM TUULUMIENI

    ReplyDelete
  6. Ngeleja ndio muongo na mnafiki. Wizara za serikali na idara zake wameshindwa vipi kulipia bili za umeme na ofisi za TANESCO walizovamia, wakati pesa zote hizo zilikwisha kutolewa kwenye bajeti? Hiyo pesa tu ya kupewa mkononi wameshindwa kuifanyia kazi ambayo wenyewe wameipanga, itakuwa fedha ambayo wananchi wanaitafuta kwa jasho? Kingine yeye ndiyo anataka kutufanya sisi wajinga, wananchi hawatalipia kiwango cha nyongeza tu, wanalipa kiwango chote ambacho Serikali imekuwa ikikiongezea karibu mara mbili kila mwaka. Ngeleja anadhani kwamba malipo yanayowasulubu wananchi ni ya umeme tu? Tunalalamika kwa sababu hii inapelekea gharama za vitu vingine kupanda kwa sababu gharama za uzalishaji pia zinaongezeka. Kama yeye kama Waziri anachukulia mambo kirahisi tu hivyo, basi huyo hafai maana ana ufinyu wa fikra.

    ReplyDelete
  7. Tatizo la viongozi wetu hawaoni mbele kuna nini kuhusu haya maisha yalivyopanda. Serikali inasema gharama sio kubwa kwa sababu wanalinganisha shilingi yetu na hela ya KENYA, DOLA NK. Sasa huyu mfanyakazi unaempiga kwanja namna hiyo mboreshee sasa mshahara apate mshahara sawa na shilingi ya Kenya au Dola sio unamnyonya tu.

    Nyinyi akina Ngelege mnajilipa MIDOLA halafu mnasema hata nchi iuzwe haiwezi kutoa mshahara wa 350,000 kima cha chini. TUCTA hakuna kukata tamaa maandamano ni lazima piga ua. Tena nchi nzima hatuwezi kuburuzwa namna hii. Kama wanalinganisha na hela za wenzetu waipandishe shilingi dhamani watazipata hizo hela kama wao wanavyozipata lakini sio kutokana na matumizi yalivyo Tanzania sasa hivi.
    Watanzania wanaishi kutokana na hali ilivyo sasa hivi ya uchumi bado mnawaongezea mzigo mwingine. Ina maana mtanzania asimpeleke mtoto shule, asile, asijitibu, asitafute malazi mazuru, bado awe kulekule kwa zama za kale, haliwezekani. Hivi hilitabaka la kibepari baba wa taifa aliliacha kweli. Tusilewe madaraka hivyo, serikali itafute njia mbadala ya kusaidia wananchi wake kutokana na rasilimali zilizopo. Acheni kubweteka acheni kutumia muda mwingi kwenye vikao vya kuongea umbea, mjungu ingieni mtaani muone maisha wanayaishi watanzania mtawaonea huruma.

    Mimi ninashangaa eti kila asubuhi kikao mnapanga nini na mnatathimini nini jinsi ya kumnyonya huyu masikini au. Sasa mlete mabadiliko kutokana na vikao vyenu. Unaweza kwenda ofisini kwa mkurugezi kila siku anavikao. Ina maana kazi yake iliyompeleka pale ni kufanya vikao kila siku. Na akitoka kwenye kikao ni msosi wa saa sita huyu anafanya kazi saa ngapi na kundi lake hilo la vikao kila siku. Hapo kuna posho ya kikao na bado mshahara mwisho wa mwezi. Jamani tubadilike.

    Yaani ukiangali kwa sasa tanzania kuna mwachano kubwa sana kati ya tajiri na masikini. Huyu masikini unataka kumnyang’anya hata ile pumzi anayo pumua.

    ReplyDelete
  8. hakuna cha ongezeko swala ni kwamba hiyo yote wanataka kulipa madeni sijui nilini sisi walala hoi tuta pumua umeme bei juu na niwa wasiwasi.

    ReplyDelete
  9. Ngeleja na viongozi wote wa CCM ni vichaa wanawaona watanzania kama ni wajinga. Kila kitu kina mwisho nadhani DAMU IKIMWAGIGA ndipo wataona kuwa WATANZANIA WAMECHOKA.

    ReplyDelete