26 July 2013

HUKUMU VIONGOZI DECI KUTOLEWA LEO



Na Rehema Mohamed
HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo inatarajiwa kutoa Hukumu ya kesi inayowakabili Wakurugenzi wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), iliyokuwa ikijihusisha na kuendesha na kusimamia mchezo wa upatu.Kesi hiyo inawakabili wachungaji wa makanisa tofauti ya Pentekoste, ambao ni Jackson Mtares, Dominic Mtares, Timotheo Ole Loitingye na Arbogast Francis.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa leo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Stuwarti Sanga, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo ikiwa takriban miaka minne imepita tangu washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani.Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 16 pamoja na vielelezo mbalimbali huku washtakiwa hao wakijitetea wenyewe pasipo kuleta mashahidi wengine.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na wakili wao, Hudson Ndusyepo, huku upande wa mashtaka ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi Prospar Mwangamila.Washtakiwa wanadaiwa kati ya mwaka 2007 na Machi 2009 katika Makao Makuu ya DECI, Mabibo Dar es Salaam walikusanya fedha kutoka kwa wananchi wakiwaahidi kuwa watapata faida ya riba kubwa. Mpango huo uliitwa wa kupanda na kuvuna ambapo wanadaiwa kufanya shughuli hiyo bila leseni.
Juni 12, 2009, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi Na.109 ya kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.Kampuni ya DECI iliyowanufaisha watu wengi hasa wale waliojiunga mwanzoni, iliibua malumbano kati ya Serikali, viongozi wa kampuni hiyo na wanachama wao, waliopinga hatua ya Serikali kusitisha shughuli zake kwa madai kuwa haiko kihalali.
Kusimamishwa kwa shughuli za kampuni hiyo, kulitokana na uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutoa taarifa ya kutahadharisha Watanzania waliojiunga na upatu huo kuwa, taasisi hiyo haiko kisheria na wanaweza kupoteza fedha zao walizopanda.Shughuli za kupanda na kuvuna mbegu DECI zilisitishwa baada ya Serikali kusimamisha akaunti za kampuni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika, hali ambayo baadaye ilisababisha uvunjifu wa amani katika ofisi za kampuni hiyo, baada ya wanachama wake kuamua kuchukua sheria mkononi kwa kuvunja vioo vya magari ya viongozi, wakitaka warejeshewe fedha zao.
Inadaiwa kuwa zaidi ya Watanzania 700,000 nchini walijiunga na taasisi hiyo na walikuwa wakipanda na kuvuna pesa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuchukua amana za watu bila ya kibali kwa kuwa waliomba kibali cha kuendesha shughuli za kifedha na si cha kuchukua amana ambapo katika utetezi wake Mchungaji Mtares alikiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote wa taasisi hiyo .
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, Mtares alidai katika barua ya majibu ya kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi hiyo, BoT iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote iwe kwa hiari au kwa lazima.
Hata hivyo alipoendelea kuhojiwa na kupewa barua hiyo ambayo ilipokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha upande wa mashtaka, Mtares alidai kuwa Mkurugenzi mwenzake ambaye pia ni mshitakiwa ndiye atakayetoa maelezo zaidi.
Katika utetezi wake Mtares aliwasilisha kielelezo ambacho ni barua ya maombi waliyoandika kwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi ambazo ni kusaidia watu wenye kipato cha chini kujikimu kimaisha.
Mtares aliendelea kudai kuwa, Benki ya Afrika (BOA) ilikataa kuhifadhi fedha za taasisi hiyo hivyo walizihamishia katika akaunti ya kanisa lake la Jesus Christ Deliverance iliyopo katika Benki ya Wananchi Dar es Salaam (DCB) ambayo ilikutwa na zaidi ya sh. bilioni 1.3 baada ya shughuli za DECI kuzizuia.
Alipoulizwa sababu za benki hiyo kukataa kuhifadhi fedha hizo, alidai hajui bali walipewa taarifa kuwa wanatakiwa watoe fedha hizo haraka ndipo bodi ya wakurugenzi ilipoamua fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti ya kanisa lake.
Aliendelea kudai kuwa wanachama walikuwa wanalipa kiingilio cha sh. 30,000 na baadaye wanaweka fedha na kupata uwezeshwaji (riba) ya asilimia 150 ya fedha ambayo mwanachama ameweka.
Alipobanwa kwa maswali na upande wa mashtaka, Mtares alidai fedha za riba zilitokana na fedha walizokuwa wanaweka wanachama kwa sababu DECI ilikuwa haijishughulishi na biashara yeyote zaidi ya kusaidia watu wenye kipato cha chini.

No comments:

Post a Comment