07 March 2011

Watu 80 wakamatwa Mbarali

Na Esther Macha, Mbarali

MGOGORO wa shamba la mpunga la mwekezaji katika Kata ya Ubaruku Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya unaoendelea kwa takribani mwezi mmoja sasa, unazidi
kuchukua sura mpya na sasa wananchi wapatao 82 wamekamatwa na Jeshi la Polisi, huku mabomu ya machozi yakipigwa.

Imeelezwa kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa tukio lililotokea Januari mwaka huu, ambapo mwananchi mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa katika mapambano ya askari na wananchi, baada ya wakazi hao kuhoji uhalali wa polisi kuruhusu gari lenye uzito wa tani 10 kupita katika barabara ya Igawa-Ubaruku, ambayo ilishaamriwa magari yenye zaidi ya tani nane yasipite.

Wananchi wameamua kudai warejeshewe shamba la Mbarali Eastate lenye ukubwa wa hekta 3,500 ambalo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga, wakisema awali lilikuwa mali yao kabla serikali haijalibinafsisha kwa mwekezaji.

Juzi vurugu hizo ziliendelea ambapo polisi walikuwa wakiingia katika nyumba za watu na kuwapiga bila kuchagua, ambapo katika moja ya nyumba alipigwa mwanamke mjamzito (miezi 8) aitwaye Bi. Lucy Mbeyela.

Ilielezwa kuwa askari polisi wa Kikosi cha Kuzuia Fujo (FFU) walikuwa wakipiga mabomu ya machozi kuwatanya wananchi waliokuwa wakijaribu kuweka magogo barabarani na baadaye kukamata wananchi 82.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Abdala Nyenza alisema kuwa sababu za kuweka magogo katika barabara hiyo inayoelekea kwenye shamba hilo ni kutokana na mwekezaji huyo kuanza kuhamisha vitu kama mashine, vipuli, na raslimali mbalimbali ambazo ni mali ya shamba hilo,

Bw. Nyenza alisema kuwa mwekezaji huyo alilikuta shamba hilo likiwa na miundombinu mbalimbali iliyotengenezwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, kwa manufaa ya wakazi wote wa Mbarali na si kwa ajili ya mtu mmoja, huku wananchi wakibaki wakiteseka kwa njaa.

Alisema kuwa walipata taarifa kutoka kwa wenzeo kuwa  mwekezaji anasomba mali za kampuni ya shamba usiku kwa usiku akitumia magari yake makubwa kwa kisingizio cha kupeleka kokoto.

“Kufutia hali hiyo tuliamua kuweka doria usiku yakapita magari makubwa yakiongozwa na madogo yenye bendera nyekundu, baada ya kupita kuingia huko kwa mwekezaji umeme ukazimwa, tukaona hapa tunataka kuzidiwa akili, tukaweka vizuizi vya magogo ili kubaini nini kinachopitishwa usiku huo.

Bw. Edsony Joseph alisema kitendo cha mwekezaji huyo kupora ardhi hiyo kunasababisha wawe masikini kutokana na kukosa maeneo ya kulima huku mwekezaji akikodisha ekari moja ya shamba hilo kwa sh. 150,000, ambapo wananchi walio wengi wameshindwa kumudu bei hiyo, hivyo kukumbwa na baa la njaa.

"Tunashangaa wananchi wakiandamana viongozi wakubwa wanakwenda kutatua mgogoro lakini sisi tunauawa huku kwa madai ya kilimo kwanza, hakuna kiongozi anayekuja kusikiliza kilio chetu, zaidi ya mbunge na diwani,” alisema Joseph.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Bw. Advocate Nyombi alisema kuwa uwepo wa askari katika eneo hilo la Ubaruku ni kutuliza ghasia na kuleta amani kwa wananchi hao.

No comments:

Post a Comment