31 March 2011

Sadaka kwa Babu yafikia mil. 50/-

*Yeye kupata mil 10/-, kanisa, wasaidizi mil. 20/- kila moja
*Kanisa kujenga jengo la huduma la kukaa watu 700 kwa pamoja
*Wanasayansi Kenya wathibitisha dawa yake kutibu maradhi mengi


Na Said Njuki, Arusha

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati limetangaza kiwango cha
fedha ambazo kimekusanywa kutoka kwa wagonjwa wanaokunywa kikombe cha dawa ya Mchungaji Ambilikile Masapila kuwa ni sh milioni 50.

Akitangaza fedha hizo jana, Askofu wa kanisa hilo, Thomas Laizer alisema fedha hizo zimepatikana tangu kuanza kwa tiba hiyo mwishoni mwa mwaka jana, kutokana na mchango wa sh. 500 kwa kila mgonjwa.

Kutokana na mgao wa fedha hizo kama alivyosema Babu ni kuwa yeye anabaki na sh 100 huku sh 200 zikienda kanisani na 200 kwa wasaidizi wake, yeye atapata sh milioni 10. Kanisa sh. milioni 20 na wasaidizi wake sh milioni 20.

Wakati huo huo, Kanisa hilo limekamilisha mipango ya ujenzi wa banda kwa ajili ya tiba ya Mchungaji Ambilikile Masapila ‘Babu’ kijijini Samunge litakalogharimu sh. milioni 100 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya mchungaji huyo.

Jengo hilo litakalohudumia watu 700 kwa wakati moja litakua la mviringo na litajengwa karibu kabisa na babu anakotolea tiba hiyo hivi sasa ambapo kutakuwa na viti vya watu zaidi ya 300, eneo la kutolea dawa, kuchemshia dawa hizo na sehemu ya kuhifadhia hiyo dawa.

Askofu Laiser alisema jana kuwa uamuzi huo umekuja wakati ambao idadi kubwa ya watu wanateseka kumfikia mchungaji huo kwa kuwa katika jua kali, na wakati mwingine mvua wakisubiria tiba.

Alisema ujenzi wa jengo hilo utaanza hivi karibuni huku akiwaomba au wengine wakiwemo serikali kutoa ushirikiano wa dhati katika kukamilisha malengo yaliyokusudiwa ili tiba hiyo ipatikane katika mazingira mazuri na yenye tija.

“Kanisa limeona ni wakati sasa wa kujenga jengo hilo litakalochukua idadi hiyo ya watu na kutolewa huduma zingine bila ugumu wowote. Tangu kuanza kwa tiba hiyo watu na wagonjwa wanaotoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi walikuwa wakisimama kusubiri tiba hiyo,” alisema Askofu huyo.

Sanjari na hiyo Kanisa hilo limefungua akaunti maalumu benki ya CRDB Na 0150036432600 na kuwaomba watu wenye mapenzi mema kuchangia huduma
zinazotolewa na Mchungaji Masapila kupitia akaunti hiyo ama moja kwa moja kijijini kwa mchungaji huyo ambapo kutakuwa na utaratibu maalumu kwa ajili hiyo.

Akizungumzia uchakachuaji wa barabara unaofanywa na baadhi ya madereva kwa kupitia Longido ili kuwahi kikombe cha babu bila kufuata foleni, Askofu alisema hiyo ni sawa na magendo mengine jambo ambalo halina baraka ndani yake.

Alisema anaamini hata hao walipata kikombe hicho ni wazi wanakimbiza baraka zao kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo hatima ya magonjwa yao ipo katika imani zao lakini si jambo zuri.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Elias Wawa Lali kwa upande wake alisema kuwa foleni katika Kijiji cha Samunge imeanza kupungua kwa kiwango kikubwa hivyo kuwa na uhakika kwamba muda ulitolewa na mchungaji huyo utafikiwa.

Pia alikiri kuwepo na madereva walikuwa wakichakachua njia ya Longido
kupitia Ziwa Natron na kumfikia babu kirahisi na kwamba hali hiyo ilitokana na watu wa Longido kuchelewa kuweka kizuizi lakini sasa hakuna tena uchakachuaji huo.

Wataka chumba cha maiti

Serikali imetakiwa kujenga chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Samunge Arusha ili wagonjwa wanaokufa njiani wakiwa kwenye foleni kuelekea kwa Babu ili maiti zao zihifadhiwe.

Pia imetakiwa kuwawajibisha polisi wanaochukua rushwa ili kuwaruhusu watu wanaoenda kwa babu wakati serikali imezuia watu wapya hadi waliotangulia wapungue.

Bw. Edward Mtakimwa, aliyesema ametoka kwa babu kupata kikombe alisema kwenye ofisi za Majira kuwa serikali ijitahidi kumsaidia mchugaji huyo ili aweze kuendelea kutoa huduma ya uponyaji katika mazingira yanayostahili.

"Polisi wanachukua rushwa kwa wagonjwa wanaoenda kwa babu ili waweze kuwarusu wakati serikali imetoa tamko la kuwazuia hadi waliotangulia wapungue," alisema.

Bw. Mtakimwa aliiomba serikali kuendelea kuiruhusu helkopta ya Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Phillemon Ndesamburo ili iwawaishe wagonjwa mahututi, na iingilie kati bei ya vyakula ambapo sahamo moja inauzwa kati ya sh. 2,000 hadi 3,500, nyama kwa kilo ni sh 8,000 hadi 10,000, maji ya kunywa chupa nusu lita sh 1,500 na lita moja ni sh 5,000.

Malori yapigwa marufuku

Serikali mkoani Mwanza imepiga marufuku aina zote za malori kusafirisha wagonjwa wanaokwenda kupata kikombe cha babu katika kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Abbas Kandoro kwenye kikao kilichowashirikisha wadau wa vyombo vya
usafirishaji pamoja na vyombo vya habari.

Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Babu kuomba msaada wa serikali kufuatia wagonjwa wengi kufariki wakiwa safarini na kwenye kufuata huduma yake.

Imeandaliwa na Daud Magesa,Mwanza; Agnes Mwaijega, Dar na Said Njuki, Arusha

20 comments:

  1. HAYA KILLA LA KHERI NAONA HAPA KAMA KUNA UCHAKACHUAJI MAANA DATA ZILIZOKUWA ZINARIPOTIWA UMATI WA WATU KILA KUKICHA INA MAANA MPK SASA NI WATU LAKI MOJA TUU NDIO WALIOKUNYWA DAWA KWA BABU? MAANA LAKI 1 X 500=NDIO MIL.50.HONGERENI KKKT!!! NAONA MAKATO HAYA KAMA TFF NA KLABU ZA YANGA NA SIMBA MAANA MMHHHH!!

    ReplyDelete
  2. babu hajafaidi lolote. Ni kazi ya Mungu. Mungu aendelee kumpa nguvu zaidi.
    Amen

    ReplyDelete
  3. NAWASIWASI KUNA UCHAKACHUZI YAANI WATU WALIOKWENDA KWA BABU NI LAKI MMOJA TU???

    KWELI KKKT KANDA YA KASKAZINI NI WACHAGA HASWA DUU!

    ReplyDelete
  4. IKIWA UWANJA MPYA WA MPIRA(NATIONAL STADIUM)UNA INGIZA WATU ELFU SITINI INA MAANA TOFAUTI NI WATU ELFU 40 NDIO IFIKIE UMATI WA KWA BABU AMBIKILE.KKKT ACHENI KURONGOFYA!

    NISHAANZA KUWA NA WASIWASI NA HIYO HUDUMA SASA! AU NI AINA MPYA YA UINJILISHAJI MPYA?

    ReplyDelete
  5. Jamani tuwe fair, wale wanaolinganisha na wanaoingia mpirani, mbona hawafikirii kuhusu viingilio? Mpira gani una viingilio vya 500 kwa wote? Lakini pia kumbuka mwanzoni hawakuwa wanakwenda watu wengi hivyo, maana taarifa zilisambaa kwa kusimuliana, hadi februari vyombo vya habari vilipomfahamu Babu. Hata hivyo, kama Babu angekuwa anatibu watu 2000 tangu mwanzo (let say kwa miezi 6 au siku 180 tangu Oktoba) angekuwa na watu 360,000. Honestly, mimi naona ni sahihi hakuna uchakachuaji, na kama upo si wa kupoteza muda kujadili.

    ReplyDelete
  6. Hiyo takwimu ya fedha iliyokusanywa ni ya kuchakachuliwa,haingii akilini kuwa ni watu 100,000 waliotibiwa na babu na wakati kili siku linaonekana kundi kubwa la watu wakieleekea kwa babu.KKKT hebu tupeni takwimu sahihi ya fedha zilizokusanywa kwa babu.

    ReplyDelete
  7. Wewe unayesema kuna uchakachuaji una uhakika gani wa maneno yako au unataka kuchochea hisia mbaya kati ya Kanisa na wananchi. Inakusaidia nini kujua ni kiasi gani cha fedha kilichokusanywa? Mimi ninaona ni vema tuone ya kuwa Mchungaji Mstahafu huyu ambaye anatoa huduma hii asaidiwe kuboresha mahali hapa ili watu wapate tiba hii kwa urahisi. Ninaungana na Dayosisi kwa mpango wake kutumia sehemu ya fedha hizo katika ujenzi wa mahali pa kutolea huduma hii. Kuboresha barabara hadi kijijini hapo si manufaa ya Mchungaji pekee yake bali ni kwa wakazi wa eneo hilo pia na kama ni kwa manufaa yao basi hata mimi nisiyeishi hapo ila kama Mtanzania ni manufaa ya nchi yangu. Bado sijaamua kwenda kupata kikombe cha Babu lakini japo nitajisikia kuumwa basi nitafunga safari nikapate tiba kwa imani. Mungu azidi kumpa Mzee huyu afya na baraka.

    ReplyDelete
  8. KWA NINI SERIKALI IMEKAA KIMYA KUHUSU SAKATA HILI. VYOMBO HUSIKA WAJIBIKENI KWA KUOKOA MAISHA YA WANANCHI.

    IWAPO DAWA INA USHAHIDI WA KITAALAMU WA KUTIBU KAMA INAVODAIWA, MPENI MVUMBUZI(BABU) MSAADA UNAOTAKIWA NA TOENI TAARIFA SAHIHI KWA TAIFA.

    ReplyDelete
  9. Hili kanisa KKKT linaingiaje hapa.Babu ni mstaafu. Sasa hawa KKKT wana haki gani kujua mapato ya BABU. Unaona sasa hawa watu wa Mungu nao ni FISADI tu. BABU anachapa kazi bure.Labda atalipwa mbinguni. Wanaokula pesa ni wengine. Je serikali inadai kodi ya mapato??

    ReplyDelete
  10. kuna mwingine kaoteshwa MAGU MWANZA yeye kikombe kimoja shilingi 1000=mimi yangu macho.msukuma.

    ReplyDelete
  11. Kustahafu kuwa mtumishi kwenye Usharika KKKT hakumfanyi mstahafu kuvua uchungaji wake na kuwa nje ya Kanisa bali yeye ni Mtumishi wa Mungu na anaendelea kulitumikia Kanisa hadi mwisho wa maisha yake. Sijui kama Mchungaji huyu katamka ya kwamba sasa hana uhusiano na Kanisa lake kwani amestahafu!! Ninavyojua mimi ni kwamba Kanisa halikufanya mkataba wa kupokea chochote toka kwa Babu bali Babu mwenyewe kama alivyotangaza kuhusu mgawo wa 500 utakuwaje ndivyo inavyotendeka sasa. Babu angeliweza kugawa apendavyo. Je hapa ufisadi wa kanisa unatoka wapi? Kama Magu kaoteshwa mwingine yataonekana matunda yake; maana yawezekana ya kwamba watatokea wengine wa uongo hilo nalo si jambo jipya; la msingi kila mtu ahitajiye tiba ndiye apaswaye kufikiria kwanza kwa nani aende. Hata kwa madaktari wa kawaida watu huwapima kwa uwezo na ubingwa wao. Hata Hospitali nazo: Je niende Bugando au Muhimbili au KCMC nk.?

    ReplyDelete
  12. Mambo ya tiba za kienyeji zinazo jitokeza sasa ni dalili wazi jinsi Watanzania wamechoka na hata kushindwa kufanya uamuzi wa kutatua matatizo ya msingi yao. Nikama tumepigwa marufuku kufikiri na kutafakari! Kila mtu amechanganyikiwa viongozi na wanaoongozwa wote mbioo Kikombe!! Tunaenda wapi. Katika hali hii kila mtu anazungumza na kudhani kuwa kila anachokisema ni sahihi! ndio maana kule visiwani kwa fikra finyu kabisa mtu anashauri wabakaji wahasiwe!! eti ni adhabu!! na je wanaoenda nje ya nyumba zao iweje! nao wahasiwe! wa kwanza ni watoa hoja hii!! Hivi sasa hakuna ujasiri hata wa kujiuzuru ni ubinafsi mtupu! maadili ya uongozi na uwajibikaji hakuna! Hospitali za Rufaa ni hospitali za rufaa ya kifo! kama hukufa kwenye zahanati basi rufaa yako inakumaliza! Mtoto wa maskini gani atapata huduma Muhimbili utaishia kwenye bench!na kutoa maiti lazima ulipe! Hovyoo kabisa! nadhani tunamhitaji Mjermani ambaye akisema reli itapita hapa lazima ipite hata kama kuna jabali! inauma sana!!

    ReplyDelete
  13. Kuna jamaa amenikera kuwataja KKKT kama wachaga wachakachuaji!! jamaa wanaofahamika na wanaolaumiwa kama mafisadi ni wachaga tu? mwogopeni Mungu! Kama unachuki binafsi na hili kabila basi useme!! tabia ya wizi, uchakachuaji, au ufisadi ni silka ya mtu bila kujali ni kabila gani!! Usiandike tu kujifurahisa! write with a critical mind!

    ReplyDelete
  14. Yaani maoni yanayotolewa yamejikita katika fikra zilele za ufinyu na mgando wa mawazo! udini ukabila hauna tija wala haupo. Akifa mwislamu wote tunaenda kwenye maziko na hata kwa mkristu na hata mpagani!! udini haupoo! hebu tujitaabishe kufikiri! TATIZO LETU NI UKOSEFU WA UWAJIBIKAJI, UBINAFSI KATIKA UTENDAJI WETU WA KAZI NA UKOSEFU WA UZALENDO KATIKA NGAZI ZOTE. ZAMANI NAKUMBUKA WATU WALIKUWA WANAENDA KAZINI MBIO UKICHELEWA KITI KIMECHUKULIWA NA KAZI HAKUNA NA LEO KUNA NINI HAKUNA. Wangonjwa wanakufa hata bila kuonana na Daktari hasa maskini wenye kupata mlo kwa siku mara moja. HUYU HAKAJIKUMWONA SPECIALIST KATIKA MAISHA YAKE YOTE. AKITOKEA MTU KAMA BABU HUYO NDO KIMBILIO LAKE. MAWAZIRI WAKURUGENZI MAKATIBU HEBU WAJIBIKENI KAMA TUMESHINDWA TUMKABIDHI MJERUMANI NCHI HII SIO MWARABU!! MWARABU ALITUDHARIRISHA SANA KWA KUWAHASI BABU ZETU. NDO FIKRA WALIZONAZO WATU FULANI WAKIDHANI KUHASI NDO UFUMBUZI WA MATATIZO!

    ReplyDelete
  15. Eheee, hivi biashara ya mapato makubwa hivi inalipiwa kodi? Mbona wafanyakazi na mama ntilie pato dogo kodi kubwa? Hapa kuna mengi yamejificha. Haramu huzaa haramu. Tusubiri hasa hao wasaidizi wanavyohenya, jamani mbona hamna huruma? Mnawapiga panga juu kwa juu! kweli pesa ilifanya Yesu asalitiwe. Serikali kaeni mbali, karibu bomu litalipuka! Mara anahamia bondeni kwa wafu, mara tunamjengea jengo hapo hapo! Babu usikubali wakujengee ghorofa home Tukuyuu!

    ReplyDelete
  16. Inasikitisha sana jinsi watanzania wenzetu wanakufa huko vijijini kwa sababu ya ukosefu wa huduma za msingi za afya. Akina mama wajawazito wanaotuletea taifa la kesho wanavyokufa!! KAMA KWELI CHADEMA wanataka kuleta mabadiliko ktk nchi hii waonyeshe kwa vitendo. MAANDAMANO HAYANA TIJA! JE KWA KUANDAMANA ARUSHA , MWANZA ,SHINYANGA WAMEPUNGUZA VIFO VYA AKINAMAMA WAJAWAZITO!!! WANGONJWA WANGAPI WAMEPATA HUDUMA ZA HOSPITALI YA RUFAA!!! HAKUNA TUKO PALEPALE! YAANI BADALA YA KUFIKIRI YA MBELE WATU WANAJADIRI MAPATO YA HUYU BABU, UJINGA MTUPU!bAHATI MBAYA HATA TIBA YA BABU IMEVAMIWA NA MANYANGUMI NA MASKINI AMEBAKIA MTUPU. KAMA KWELI CHADEMA INATAKA NGUVU YA UMMA ILI ICHUKUE MADARAKA IONYESHE KWA VITENDO HASA KATIKA huduma ya afya vijijini! AKINAMAMA WANAKUFA SANA VIJIJINI! CHADEMA GUSA AKINA MAMA VIJIJINI UTAIBUKA MSHINDI! MAANDAMANO HAYANA TIJA SANA SANA NI VIJANA WAVUTA BANGI AMBAO HATA KURA HAWAPIGI!!! NA CCM IKISHINDA OHOO!WAMECHAKACHUA!! ACHENI SIASA ZA KWENYE MAJUKWAA TULETEENI MAENDELEO KWA VITENDO NDO TUWAPE DOLA!! WATANZANIA WOTE NI WAGONJWA SI MNAONA WENYEWE!! TUNATAKA MATENDO HASA KATIKA HUDUMA ZA AFYAA! TUACHANE NA VIKOMBE VINAVYOZUKA KILA SIKU!!!

    ReplyDelete
  17. Mtu unasema eti mnataka kuleta machafuko kati ya babu na Kanisa KKKT mapato yanakuhusuni nini? Hv tulikuuliza au kuna mtu alihoji?Ni habari imeandikwa ndio tumeshangaa kuona hesabu hizo maana kuna gazeti liliwahi kuandika kuwa kuna wakora toka Kenya wanataka kumuibia babu eti mpk sasa katibu watu Mil 6 kwa hiyo ana bill 3 hayo yote tunayasoma ktk magazeti sasa tusihoji tuwe kama manamba kusikiza na kukubali kila kitu? kwa hiyo basi hakuna haja ya kuandika idadi ya watu wala fedha wala haina haja ya kumtangaza kila kukicha acheni kujiona mwajuwa na mahodari wa kila kitu eti wengine wajinga wewe unaeona wenzako ni wajinga wewe ndio kiongozi wao

    ReplyDelete
  18. Jamani mwacheni Babu aokoe watu waliochoshwa na magonjwa sugu,na serekali imsaidie kuboresha mazingira ya Babu ili huduma itolewe katika mazingira yanayoridhisha.Badala ya kuanza kulumbana juu ya mapato yanayopatikana.

    ReplyDelete
  19. WACHAGA ASILI YENU WEZI NA MAKATILI TOKA ENZI NA ENZI WENGINE SASA WANAJIFUNZA

    ReplyDelete
  20. Huyo anayesema wachaga wezi hawajui wachaga. Wachaga ni watu wa kazi, wanafanya kazi. Matokeo ya kufanya kazi kwa bidii ndio mafanikio ya wachaga. Wachaga wanajua kuhangaikia maisha na kuona mbali. Wachaga wanatoa sadaka acha mchezo, hiyo ndio siri ya mafanikio yao. Jaribu uwaige uone mambo yatakavyokunyookea.

    Wachaga ni wasomi, ni ofisi gani katika idara gani utamkosa mchaga? We kaa ukisema wachaga asili yao ni wezi uone kama hujajilaani mwenyewe. Mimi si mchaga ila nawa-admire sana wenzetu. Hongereni wachaga. Tungengefanya kazi kama nyie tungekuwa mbali sana. hata hivyo si wote, wapo wavivu lakini wengi ni wachapa kazi.

    ReplyDelete