16 March 2011

'CCM inahitaji upasuaji makini'

*Wasomi wadai bila hivyo watagawana mbao

Na Tumaini Makene

WAKATI Chama Cha Mapinduzi kikijiandaa kujivua gamba kama alivyoahidi mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, imeelezwa kuwa
kinapaswa kuwa makini kwani 'kinahitaji upasuaji wa uangalifu' ili kurudisha imani ya Watanzania.

Uchunguzi wa Majira kwa siku kadhaa juu ya mstakabali wa chama hicho, umebainisha kuwa kwa hali kilipofikia chama hicho kinapaswa kufanya mabadiliko ya dhati, ili kiweze kuweka 'gamba jipya la kusimamia matakwa ya watu na jamii na kuuhisha miiko ya uongozi iliyopotea, vinginevyo mwakani au 2015 wanaweza 'kugawana mbao'.

Mmoja wa wabunge wa chama hicho akizungumza na Majira jana kuwa hata vikao vya CCM vinavyotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Dodoma vinaweza visikisaidie chama hicho iwapo watu 'wanaosema ukweli' ndani ya chama wataendelea kushughulikiwa na makundi fulani.

Mbunge huyo ambaye hakutaka kutajwa jina akizungumza na Majira jana katika semina ya wabunge juu ya usimamizi wa bajeti inayoendelea Dar es Salaam alisema kuwa vikao vya Dodoma havitaweza kuiponya CCM iwapo watu wanaosema ukweli, ndani ya chama hicho, kwa kukemea maovu na kushauri pale inapobidi 'wanashughulikiwa' kwa kupitia makundi ya umoja huo, hususan Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM).

Alisema kuwa vikao hivyo haviwezi kuisaidia CCM kwani imepoteza ushawishi kwa wananchi wa chini kwa kushindwa kusimamia na kuzungumzia kero zao, badala yake 'viongozi walafi na wabadhirifu' wamepewa nafasi na wale 'waadilifu wanaosimamia
uwajibikaji na uadilifu wanasakamwa au kuwekwa kando'.

"Nikwambie kitu chama hiki si kimoja tena.  Hakipo. Kimeparanganyika mno na ushindi wake mwaka 2015 ni mfinyu sana, watu huko chini hawana imani nacho tena, hebu kaulize mikoani au wilayani, akina nani wanaofanya mikutano tena, ukiona mbunge
anafanya mikutano sasa si kwa sababu watu wanakitaka chama bali wanamkubali yeye, basi.

"Chama hakiwazungumzii watu tena, wala hakiwezi kupona kwa kufukuza watu pekee. Usishangae hata mimi kesho nikashughulikiwa na vijana kwa yale niliyoyasema hivi karibuni katika vyombo vya habari," alisema mbunge huyo.

Pia, Profesa wa masuala ya uchumi, Samuel Wangwe amelieleza Majira kuwa ili CCM iendelee kuwa salama hasa kuelekea uchaguzi wa ndani 2012 na ule mkuu wa mwaka 2015 haina budi kufanya marekebisho makubwa la sivyo itakuwa katika hali mbaya.

"Kwa hatua iliyofikia sasa CCM lazima ifanye mabadiliko makubwa, la sivyo hali itakuwa mbaya 2015, wanaweza kufanya mabadiliko...ikiji-organize inaweza, bado wana nafasi ya kujirekebisha, lakini kwa maumivu fulani. Haitaweza kufanya marekebisho bila kuumia, lazima ikubali kuumia, kama alivyoshauri mwenyekiti kuna haja ya kujivua gamba.

"Itachukua muda kwa CCM kufa kwa sababu bado iko vijijini, bado ina nguvu maeneo mengi ya nchi vijijini, lakini kama hali itaendelea kuwa hivi kuna hatari ya kupoteza ushawishi hata huko pia," alisema Profesa Wangwe.

Mchambuzi mwingine, Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bw. Bashiru Ally alisema ili kujivua gamba kama afanyavyo nyoka, CCM inatakiwa kujifanyia upasuaji mkubwa, ili iendelee kuwasemea watu, wakulima na wafanyakazi ambao ndiyo wazalishaji wakuu wanaonyanyasika na mfumo mbovu.

Bw. Bashiru ambaye alisema kuwa bado anaamini kuwa maneno ya Hayati Babab wa Taifa kuwa 'bila CCM imara nchi itayumba', alisema kuwa chama hicho hakina budi kujifanyia 'upasuaji wa kitaalamu' ili kuondoa mfumo uliozalisha makundi ndani ya chama, yanayotumia matatizo ya watu kujihalalisha katika jamii.

"Sijui kama Mwenyekiti wa CCM alisema juu ya mageuzi makubwa ndani ya chama baada ya kufanya uchambuzi wa kina, gamba la CCM si sawa na gamba la nyoka ambalo linajivua naturally baada ya kufikia kipindi fulani, halina usumbufu katika kujivua na haliathiri maisha ya nyoka. Hili la CCM ni tofauti, hili limeganda haliwezi kutoka smoothly. CCM inahitaji zaidi ya hapo. Inatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kitaalamu.

"Maana upasuaji makini wa kitaalam lazima utagusa maslahi ya kakundi kalikoteka chama, kuweka gamba jingine litakalozingatia sera, matakwa ya watu na jamii, miiko ya uongozi na maadili ili kuwaondoa viongozi walanguzi na waporaji walioko katika
chama, kiongozi wa namna hiyo akijitokeza tena anashughulikiwa siku na saa hiyo hiyo. Hicho ni chama cha wafanyakazi na wakulima wazalishaji wakuu.

"Chama kinachopaswa kuwasemea wakulima wa pamba Shinyanga wanaolia kwa kuuziwa dawa ya kabeji badala ya pamba, hiki cha sasa kimegueka, hakilindi maslahi ya wakulima wala wafanyakazi tena...viongozi walanguzi wanatumia jasho la mkulima asiyekuwa na
mtetezi...upasuaji huu unapaswa kuhusisha maandalizi ya msingi, wasiende Dodoma kukatana mitama, bali wafanye upasuaji wa kitaalamu, kisha wanachama wazaliwe upya, wasioweza wajiondoe wenyewe," alisema Bw. Bashiru.

"CCM hakina budi kurejea katika misingi yake ya awali, badala ya kuendelea kukumbatia wafanyabiashara, wachuuzi, walanguzi, wababaishaji wanaojilimbikizia mali kupitia gamba la chama hicho, hao watafute chama chao katika mfumo kama huu wanaweza kabisa kuwa na chama chao cha walanguzi na wachuuzi, badala ya kuendelea kutumia jasho la wazalishaji na wavujasho."

3 comments:

  1. Tena waachane na hao wafanyabiashara wakubwa na kuwapa vyeo ndani ya chama hao ndiyo wanao fanikisha wizi nadhani wanafahamika pia wale viongozi ambao wameonekana ni mzigo kwa chama na kuwa na kauli za kupenda sifa pia waachane nao.Mawazo yao imekuwa kwamba wanamsadia Mwenyekti kumbe wanampotosha timua wote.

    ReplyDelete
  2. Watu wabaya wapo katika sehemu zote ndani ya jamii na si ndani ya CCM tu. Nasema hivyo nikimaanisha ya kwamba si wafanyabiashara wote wakubwa nchini mwetu waliomo CCM ni wabaya ila wapo kweli wanaojilimbikizia mali na umaarufu wa kuwatumia wananchi kwa manufaa yao. Hawa siwaungi mkono. Kama tutarudi nyuma ni jinsi Baba wa Taifa alivyokuwa mimi siwezi kusema ya kwamba alijilimbikizia mali kwa ajili yake na familia yake. Na kwa sasa sina habari za uhakika kama Kikwete amejilimbikizia mali; maana sijaibaini na kama nitapata ushahidi huo basi nitasema. Tuangalie pia wanachama wa kawaida wa CCM wenye mali nyingi. Je nao wamezipata wapi? Usafishaji wa chama utuguse sisi wote wana CCM ili tujipange sawa kwa manufaa ya nchi yetu. Jakaya hawezi peke yake bila nguvu ya umoja wa wana CCM wakiwemo vijana. Nawatakia UVCCM baraka na busara.

    ReplyDelete
  3. chama ccm ni kizuri isipokuwa kimepoteza malengo mila na desturi zake, hebu turejee katika misingi halisi ya chama hiki cha ccm, ilikuwa ni kulinda na kutetea maslahi ya wakulima na wafanyakazi, na ndiyo maana hata alama zilizopo katika bendela ya chama hicho ni jembe na nyundo, jembe likiwakilisha mkulima, na nyundo ni mfanya kazi. je viongozi wa sasa wa chama hicho wanajua hata maana ya hizo alama? au wanadhani ccm ni kuvaa nguo za njano na kijani? hiyo ni elimu ndogo ya awali ambayo nadhani viongozi wa chama hiki waliowengi hata hawajui. Nampongeza kiongozi mstaafu alitoa ushauri kuwa chama kina viongozi ambao hata hawakijui chama , hata historia yake. Mwalimu alikuwa anapeleka makada wake ktk chuo cha siasa ili wakapate elimu ya siasa. Leo siasa za ccm zimevamiwa na walanguzi, majambazi, watukanaji wenyeviburi wsiojua hata miiko ya ungozi. ushari kwa mwenyekiti wa ccm; kaka jitahindi kuondoa uswahiba na kujuana katika masuala ya msingi kama haya na ndipo utakinusulu chama kilichokuwa kinang'ara na kutia matumaini kwa watanzania walio wengi. usione haya wakati wa kujivua gamba mheshimiwa, kumbuka usipofanya hivyo watakuharibia mazuri mengi uliyopanga kuwafanyia watanzania.Pia washauri hao walanguzi waunde chama chao wasijichanganye kwenye chama hiki, wasitumie kivuli cha ccm kuleta uchafu katika nchi nzuri ya watanzani. Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete