04 February 2011

Ufisadi umeshusha hadhi ya nchi-Wasomi

*Matabaka sasa yatishia mustakabali wa taifa
*Kongamano kuhusu suala hilo kufanyika kesho


Na Tumaini Makene

UFISADI unaoendelea kuigubika Tanzania, kama vile wizi wa mabilioni ya umma, uporaji wa rasilimali, kukosekana kwa uzalendo, mauaji,kuporomoka k w a
k i w a n g o c h a e l i m u ,kukosekana kwa dira na mwafaka wa kitaifa, zimelipotezea taifa heshima iliyokuwepo kabla ya kuzuka kwa mambo hayo.Imeelezwa pia kuwa juu maovu hayo yanayolizunguka taifa kwa sasa, kubwa jingine lililopo linalotishia mustakabali wa mtangamano wa kijamii,ni kujengeka kwa matabaka, ambapo kumekuwa na kasi ya tabaka la wenye nacho kufaidika kwa kunyonya na kupora tabaka la wasio nacho.

Kutokana na nchi kuwa katika utata huu , Watanzania wametakiwa kutafakari kwa kina Azimio la Arusha, ambalo liliweka misingi ya ubinadamu na uzalendo kwa taifa, ili waweze kufahamu walipojikwaa na kuona jinsi ya kujikwamua.

Hayo yamo katika sehemu ya taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Chama Cha Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA) ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kuhusu kongamano la kujadili maadhimisho ya miaka 44 ya Azimio la Arusha, litakalofanyika chuoni hapo, kesho Februari 5. Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa SAVITA-UDSM, Bw. Sabatho Nyamsenda, ilisema kuwa kaulimbiu ya kongamano hilo itakuwa ni “Tafakuri ya kina juu ya Azimio la Arusha. Je, lina nafasi gani katika Mjadala wa Katiba Mpya?”

Alisema kuwa kongamano h i l o l i t a a n z a k w a m a d a itakayowasilishwa na Prof. Issa Shivji (Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, UDSM), itakayofuatiwa na mjadala wa washiriki chini ya uenyekiti wa Bw. Bashiru Ally ambaye ni mhadhiri msaidizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, hapo UDSM.

Katika taarifa yake hiyo, Bw. Nyamsenda alisema kuwa washiriki wa kongamano hilo, hususan vijana, watapata fursa ya kujifunza na kujadili kwa kina maudhui ya Azimio la Arusha,na kutafakari iwapo kuna haja ya kuyatumia katika mjadala wa katiba mpya.“Ni matumaini yetu kuwa,mbali na kujenga ari ya tafakuri tunduizi miongoni mwa washiriki, kongamano hili litakuwa chachu kuzalisha vijana wazalendo, wenye kujiamini, wapigania usawa,wenye uchungu na rasilimali za nchi yao na wanaotumia elimu yao kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa manufaa ya watanzania wanyonge. “Kwa nini maadhimisho ya Azimio la Arusha? Ni haki yetu ya kihistoria kufanya maadhimisho haya. Lakini kubwa zaidi ni kwamba hali tuliyo nayo sasa haitoi matumaini juu ya mustakabali wetu kama taifa.

Zamani ulikuwa ukitaja Tanzania taswira inayojengeka ni udugu, utu, uwajibikaji na utulivu. “Pamoja na umaskini wetu, azimio liliwafanya Watanzania waishi kwa matumaini. Ni matumaini hayo yaliyojenga amani na mshikamano miongoni mwetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza; “Leo hii utajapo Tanzania ghafla unakutana na kashfa za wizi wa mabilioni ya wanyonge, uporaji wa rasilimali, kukosekana kwa uzalendo, mauaji, kuporomoka k w a k i w a n g o c h a e l i m u , kukosekana kwa dira na mwafaka wa kitaifa, n.k. Kubwa zaidi ni kujengeka kwa matabaka; tabaka la wenye nacho likifaidika kwa kunyonya na kupora tabaka la wasio nacho. “Hata sisi tunaosoma hatuoneshi dalili njema juu ya mustakabali wa taifa letu. Wengi tumetawaliwa na tamaa za kujilimbikizia mali
na kuishi maisha ya anasa za kitajiri na ubinafsi pindi tu tupatapo nafasi. Wengi tunaapa kufanikisha dhamira zetu hata kama itatulazimu kuuza nchi yetu,achilia mbali utu wetu.

SAVITA katika taarifa yake iliongeza kuwa Watanzania wanapoingia katika mchakato wa kuandika katiba mpya hawana budi kujitazama upya kwa kuangalia wapi walipojikwaa ambapo mengi ya matatizo yanayosumbua taifa sasa, hayahusiani na umasikini wa kipato.“Je, tatizo ni nini? Ni wazi kuwa, kwa kulitafakari kwa kina Azimio la Arusha, tutafahamu ni
wapi tulipojikwaa na kuona jinsi ya kujikwamua,” ilisema taarifa hiyo.

Mara kwa mara, wanazuoni wa UDSM wamekuwa wakifanya makongamano juu ya umuhimu wa Watanzania kulijadili na
kulifanyia tafakari ya kina Azimio la Arusha ambalo lilizaliwa Februari 5 mwaka 1967, ambalo pamoja na mambo mengine liliweka misingi ya kitaifa pamoja na miiko ya uongozi. Katika azimio hilo, ambalo
limebaki kuwa moja ya alama zisizofutika za uongozi makini, uliojali maendeleo ya watu za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, liliweka dira ya taifa, likielezea kuwa Tanzania itakuwa ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea,huku uongozi ukielezwa kuwa ni dhamana.

Mwaka huu mjadala juu ya Azimio la Arusha unafanyika huku nchi ikiwa imegubikwa na hoja za ufisadi mbalimbali,ambazo zimekuwa zikionesha dhahiri kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa jamii,hususan viongozi wanaopaswa
kuwa watumishi wa umma.

Mjadala huo unafanyika wakati nchi ikiwa katika mjadala mzito wa sakata la Kampuni ya Dowans, ambayo baadhi ya wasomi wa UDSM juzi walisema kuwa ni sehemu ndogo ya familia kubwa ya ufisadi iliyoenea katika sekta mbalimbali nchini katika sura tofauti tofauti kama vile mikataba mibovu, ubinafsishaji hovyo wa mali ya umma, na migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi wanyonge Walisema kuwa ‘familia ya ufisadi’ hiyo inaliangamiza taifa na kutishia mstakabali wake,ambapo walionya kama hatuastahili hazitachukuliwa kwa kuangalia chanzo cha matatizo yaliyoifikisha nchi hapo ilipo,kuna hatari ya kufuata mkondo
wa Tunisia, Misri, Algeria, Yemen na Jordan.Katika mijadala juu ya Azimiola Arusha, kumekuwa kukiibuka
hoja mbalimbali kuwa ni vyema taifa likafikiria namna ya kulifanyia kazi kulingana na muktadha wa wakati huu,hasa kwa kuangalia misingi ya utu, ubinadamu, uzalendo na miiko ya uongozi, huku ikielezwa kuwa “Azimio la Arusha liliwajali wanyonge.”

11 comments:

  1. Wakitembelea nchi za wenzao zenye utawala bora na maadili utaona wanacheka kama mazuzu bila kuona aibu ya uchafu wa ufisadi uliojaa nchini kwao.

    Kuporomoka kwa maadili kunatokana hasa na mafisadi yaliyojaa katika halmashauri kuu ya chama tawala ambayo yanaitafuna hii nchi kama saratani. Ndiyo maana utaona halmashauri kuu iliidhinisha ulipaji wa Dowans kabla wabunge wa chama hicho hicho kukataa. Hii si nchi yenye mafisadi tena bali ni mafisadi wenye nchi! Kwa hali hii twaelekea kubaya sana.

    ReplyDelete
  2. Nawapa changamoto viongozi wa nchi hii na pia wale wote waliotajwa katika "orodha ya aibu" (list of shame) kama wanao ubavu wahudhurie kongamano hilo na kushiriki katika mijadala ya kongamano hilo.

    ReplyDelete
  3. Ndugu watanzania shime tushikamane kulikomboa taifa ni lazima katiba mpya itamke wazi kutekeleza azimio la arusha kama sera ya Taifa no way jinsi ya kuwaandhibisha viongozi wa ccm wanayoifanya nchi ni yao na serikali ni yao hadi kurubuni watawala wa jeshi kutoa matamko feki kinyume na maadili yao pamoja na kuuwa raia,jamani majeshi ya tanzania jifunzeni MISIRI MNAONA WANATAWANYA MAANDAMANO? WAO WANALINDA ILA HUKABILIANA NA WALE WANAOLETA VURUGU TU KWENYE MAANDAMANO.

    ReplyDelete
  4. Hongera UDSM kwa kutuletea mijadala yenye tija.
    Hawa mafisadi mbona tutawangoa tu.

    Azimio la Arusha lipo mioyoni mwetu. Wote tuliosoma kabla ya Mwinyi kutawala tunaliamini

    Tuwafundishe wadogo zetu na watoto wetu hii misingi ya Azimio la Arusha.

    Napendekeza vipeperushi vya misingi ya Azimio la Arusha viandaliwe na visambazwe mashuleni, vyuoni, kwenye masoko, maofisini, na vituo vyote vya magari nchini kote

    ReplyDelete
  5. Kama ni lawama katika hili, CCM haiwezi kukwepa. Wao ndiyo hasa waliotufikisha huku tulikofika sasa. Zile mbio zote za kukimbilia CCM, na bungeni, ni katika kukimbilia aidha kupora mali za taifa hili, au kujificha baada ya kupora. Haijabakiza mtu. Toka Marais , Mawaziri, Wabunge na Makada mbalimbali wa Chama hiki tawala, wamejihusisha kwa namna moja au nyingine, kujigawia sehemu ya uchumi wa nchi kuwa vya kwao binafsi. Wamehodhi maliasili, viwanda, mashirika, mabenki nk., kama vya kwao, matokeo yake huoni nchi inaendelea, kwani kila cha ziada kinachozalishwa, ni cha mtu.
    Ukiangalia leo foleni za Watalii wanaolipia kuingia Serengeti tu, utashangazwa na vipato tunavyosikia vimepatikana. Angalia bandari na migodi, unaambiwa hamna kitu!!
    Jamani, mbona kuna nchi, uchumi wao unatokana na Bandari tu basi!..na hawakopi kwa mtu. Kuna nchi zinaendeshwa kwa utalii tu, na huwasikii kugonga hodi IMF wala WB, ila sisi tu wakati hivyo vyote tunavyo!!
    Viongozi wetu, na hasa wa Serikali na hivyo Chama, jamani, tupunguze ubinafsi, uchoyo na tamaa, hebu tuikumbuke nchi yetu, ili na wengine waifaidi. Mbona mnakuwa kama Wachawi? Hamna hata huruma?
    Halafu mimi kitu kinachonisikitisha zaidi, ni pale hawahawa,wanapofanya kila jitihada, mpaka za kichawi, kuwaingiza na watoto wao kwenye mfumo huohuo. Huku si kufundishana wizi na ufisadi? Tunapelekana wapi?

    ReplyDelete
  6. sio ufisadi ndo ulioshusha hadhi ya nchi bali ni kuwa na viongozi wasiokuwa na uzalendo na nchi yao bali kujijali wao na familia zao. kuwa na rais anewalinda wachache ndio kumetufikisha hapa. naona baba salma hafai kuwa rais wa nchi hii kwa sabab zifuatazo.
    kwanza hana msimamo katika maamuzi yake, pili ni kiongozi dhaifu kifikra mpaka mwili hana sauti kama rais, na tatu ni mwizi wa raslimali za nchi yetu kwa kutumia majina na kampuni hewa. dowans kwa vyovyote jamaa(kikwete) anaijua kwa undani sana. hivo ndivo vinavoitia udhaifu nchi yetu. kaka ndani ya miaka mitano chunga sana yasikukute kama yanayomkuta mubarak na rais wa tunisia.

    ReplyDelete
  7. Jamani sio CCM tu nchi hii inaliwa na kila mwenye meno,na vyombo vya sheria ni kuti kavu,mwenye pesa hafungwi na akifungwa huko jela anakaa kama kwake VIP,wanasiasa wangapi wamechukua pesa NSSF akiwemo Mbowe wa Chadema,je mimi na wewe mlalahoi na ndio wachangiaji wakuu wa mfuko huo tunaweza kupata kwa urahisi? mkianza kuwanyooshea CCM pekee yao na wao wanakuwa wanajilinda,tujadili hapa tulipo na jinsi ya kulinda maliasili yetu.SASA HIVI WABUNGE WANATAKA KUJENGEWA NYUMBA DODOMA HII NI HAKI KWELI? MWENYE NACHO ANAENDELEA KUONGEZEWA.

    ReplyDelete
  8. 1.Kuhusu maandamano ya wanachuo:
    Hivi nchi hii itafika wapi?
    Wengine tunashindwa cha kusema.
    Haki isipotendeka huleta malumbano na vifo kama misri na sehemu kwingineko.
    Rushwa ni adui wa haki. Wanafunzi wasiposhiba watafanya kila aina ya uovu wapate chakuala.
    Mpe chakula mwanafunzi, hata kama hakuna mwalimu atatulia. Shibe ni adui wa kwanza wa mwanafunzi, uongozi uelewa. halafu wakati mnaandamana wanafunzi mjifunze kuwa wizi wa taifa ni mbaya kwani wengi wenu ni wezi tayari na mnakula sahani moja na sesem yenu na ndiyo tunaowategemea muwe wanyonyaji wa kesho, kwani baba zenu mawaziri walisoma hapohapo na kuandamana leo hii ndiyo mijizi mikubwa, udnukim yenu!

    2.Elimu: Hata ikishuka, ngoja ishuke ila watoto wawe shuleni wakue kabla ya kuozwa kwa ng'ombe wawili baada ya darasa la saba.

    3. kuhusu nchi yetu.
    Siyo mbaya sana kama watu wanavyodhani. nimetembea nchi 40 za Afrika kwa kweli hatuko nyuma sana. Kinachotakiwa ni marekebisho madogo tu ikiwa ni pamoja na kubadilisha chama,utawala na katiba tutasonga mbele. we are poor but not miserable like many indians or those of bangladesh (the majority)Msife moyo!

    ReplyDelete
  9. Comments zote ni nzuri, ila ninachoshangaa kila mtu anakwepa kueleza chanzo cha matatizo Tanzania. Tukiwa hatuongea straight chanzo cha matatizo kweli hatutatatua matatizo yetu. Ukeli ni Kwamba Rais Jakaya Kikwete Ndiyo ameendekeza haya yote. Tutasema Azimio la Arusha, Tutasema Viongozi wa CCM lakini wote hao wapo chini ya Kikwete. Aidha Kikwete aamue kufanya kazi yeye mwenyewe ya kuwajibisha Mafisadi kitu ambacho ni ngumu kwani yeye mwenyewe ni sehemu ya Ufisadi, au watanzania tukubali tulikosea kuchagua kiongozi asiyekuwa na uwezo tusubili tu mpaka muda wake ufike. Kama tunaumia sana basi, Misri Tunisia Nk ni mifano mzuri ya Kuigwa, ila shida yake lazima tujue damu nyingi itamwagika, kwani uwezo wa raisi wetu ni wakutumia nguvu zaidi kuliko akili.

    ReplyDelete
  10. Tanzania sasa inatawaliwa kijeshi. Wanajeshi wamevaa sale za CCM na Suti za kifisadi na sasa ndiyo Watawala ( siyo Viongozi ) wa Nchi.Hesabu kamili ya Wanajeshi serikalini na kwenye CHAMA TAWALA inajulikana na inaongezeka. Tanzania ni sawa na Misri. Hatari!!

    ReplyDelete
  11. Jamani waandaaji, napenda kutumia sehemu hii kuwapongeza kwa ajili ya kongamano hilo la miaka 44 ya Azimio la Arusha.

    Maoni yangu ni kwamba, katika yale yote yatakayojadiliwa yasiishie hapo Nkurumah Hall. Yapelekwa katika sehemu husika ikiwa ni pamoja na mambo muhimu yaliyohubiriwa na Azimio la Arusha.

    Kuna mambo mengi nadhani watanzania tumeanza kuasahau kama, uzalendo, udugu na umoja wetu, viongozi kuweka maslahi binafsi mbele badala ya maslahi ya taifa.

    Hilo lisipofanyika matabaka yatakuwa chanzo cha mparaganyiko wa taifa letu teule la Tanzania.

    ReplyDelete