09 February 2011

TAKUKURU yamng'ang'ania Mungai

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kesi ya rushwa inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Joseph Mungai
haijafikia mwisho.

TAKUKURU imesema licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa kuondoa kesi hiyo kwa sababu mbalimbali za kisheri,a taasisi hiyo itakata rufaa haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Uhusiano wa TAKUKURU, Bi. Doreen Kapwani, kesi hiyo haijafikia mwisho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU ilipokea maamuzi yaliyotolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kuhusiana na kesi ya Rushwa namba CC 05/2010 iliyokuwa ikimkabili Bw. Mungai na wenzake.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika uamuzi huo uliotolewa Januari 31, mwaka huu na Hakimu Mary Senapee, mahakama hiyo iliondoa hati ya mashtaka ya awali kutokana na sababu za kisheria.

Taarifa hiyo ilitaja sababu ya nyingine kuwa ni kutoa mwanya kwa upande wa mashtaka kuifanyia marekebisho hati hiyo na kuiwasilisha upya mahakamani.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa uamuzi huo wa mahakama ulilenga pia kutoa mwanya kwa upande wa mashtaka kuandaa hati mpya ya mashtaka na kuiwasilisha mahakamani.

"Tunapenda kuujulisha umma kwamba uamuzi huu haumaanishi kuwa watuhumiwa wameachiwa huru kama ilivyodaiwa na vyombo mbalimbali vya habari.

Serikali itakata rufaa na itairejesha kesi hii upya mahakamani kama hukumu ilivyoelekeza," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

TAKUKURU pia ilitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi waendelee kukipa ushirikiano kwa kutoa taarifa za kuwafichua wanaojihusisha na vitendo vya Rushwa.

4 comments:

  1. Mr Joseph Mungai alipata lini uprofesa?

    ReplyDelete
  2. Na mimi nashangaa. Kaupatia wapi? Au siku hizi nae mganga wa kienyeji?

    ReplyDelete
  3. sio profesa huyo may be jamaa wa gazeti wamekosea tu ktk uchapaji

    ReplyDelete
  4. Next time when you report an issue,tell the mass what is an ingredient collateral to the case."what is Mungai convicted thereof'.

    ReplyDelete