11 February 2011

Ripoti yalimwagia sifa bunge la tisa

Na Tumaini Makene

WAKATI ripoti ya tathmini juu ya utendaji kazi wa bunge la tisa chini ya Spika Samuel Sitta imeonesha kuwa lilikuwa na ufanisi na ubunifu, imeelezwa
kuwa bunge la sasa limeanza kwa 'kuchakachua' kanuni, hivyo kutakiwa kuwa makini ili lisije likapoteza uhalali machoni pa wananchi.

Hayo yamesemwa jana katika uzinduzi wa ripoti ya tathmini ya bunge la 9, iliyoandaliwa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambapo jopo lililopewa kazi hiyo ya kutathimni liliifanya kwa miaka mitano 2005-2010.

Ripoti hiyo imesema kuwa bunge lililopita lilipata ufanisi na mafanikio kadhaa, kutokana na ubunifu na ujasiri wa baadhi ya wabunge wakiongozwa na utayari wa Bw. Sitta, ambaye wakati akishika nafasi hiyo aliahidi kuwa 'spika wa kasi na viwango.'

Mafanikio yaliyopatikana katika bunge hilo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni pamoja na kutungwa kwa kanuni mpya za bunge za mwaka 2007, ambazo zimeelezwa kuwa zilisaidia kwa kiasi kikubwa kuliwezesha lifanye kazi kwa ufanisi kama vile kuondoa ukiritimba wa serikali kuwa ndiyo pekee inayoweza kupeleka muswada bungeni.

Kanuni hizo mpya za mwaka 2007 ambazo zilitokana na kufanyia marekebisho makubwa kanuni za bunge za mwaka 2004, zilitoa mamlaka kwa kamati za kudumu za bunge kuwa na uwezo wa kupeleka mswada kwa ajili ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwa sheria.

Mambo mengine yaliyolipatia sifa bunge la tisa kutokana na mabadiliko ya kanuni za bunge, ni kuruhusu uwasilishwaji wa hoja binafsi bungeni, ulazima wa kamati za kudumu za bunge kushirikisha umma katika kujadili mapendekezo ya miswada mbalimbali.

Masuala mengine ni kamati za kudumu za bunge kuwa na uwezo wa kujadili na kuwasilisha mapendekezo yao bungeni kwa ajili ya kujadiliwa, pia bunge kuwa na uwezo wa kuanzisha kamati maalumu zilizo na uwezo wa kuchunguza mambo kama ile iliyochunguza kashfa ya Richmond, uvunjifu wa haki za binadamu kwa kuchafua maji ya Mto Tigiti huko Mara.

"Mapema kabisa Bw. Sitta aliahidi kuendesha bunge katika namna mpya. Kwa maneno yake mwenyewe alisema kuwa bunge la tisa litaendeshwa kwa 'kasi na viwango'. Kwa hakika wachambuzi wengi wanasema kuwa ameifanya kazi hiyo kwa kiwango kikubwa, kubadili mwonekano wa chombo hicho muhimu," ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Ikiendelea kuchambua ufanisi wa bunge la 9 kutokana na tathimini ya miaka 5, ripoti hiyo inasema kuwa katika kutimiza moja ya majukumu yake ya msingi ya kikatiba, lilibadili na kutunga sheria kadhaa kwa maslahi ya jamii, zilizokuwa na mtazamo wa haki za binadamu, kama vile Sheria ya Mtoto ya 2009, Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Watu wenye Ulemavu (2010).

"Katika mikutano yake 20, bunge la 9, sheria 102 zilitungwa katika mikutano 19 ukiweka pembeni mkutano wa kwanza wa Desemba 2005. Ukilinganisha na bunge la 8, bunge la 9 lilijikita zaid katika kutunga sheria ambazo kwa kweli zilikuwa na uhalisia wa mahitaji ya jamii, zikitilia maanani haki za binadamu.

"LHRC pamoja na wadau wengine walijadili jumla ya miswada 35 kabla haijajadiliwa bungeni...LHRC ilitoa mapendekezo 21 kupitia Kamati ya Kudumu ya Maendeleo ya Jamii, 11 yalifanyiwa kazi, 8 yalichukuliwa kama yalivyo.

2 comments:

  1. MTU MKWELI CCM HAWAMTAKI, ANGALIA SITTA ALIVYOCHAKACHULIWA KWENYE NAFASI YA SPIKA NA TIDO MHANDO ALIVYOFANYIWA TBC,NDIO UTAJUA CCM HUWA HAWAPENDI WATU WANAOWEKA MASLAHI YA TAIFA MBELE.BUNGE LA SASA HAKUNA CHOCHOTE ZAIDI YA KUMPONGEZA JK. WABUNGE WANAACHA KUJADILI MATATIZO YANAYOLIKABILI TAIFA KWA SASA KAMA MAJI NA UMEME,WANATUMIA MUDA MWINGI KUMPONGEZA RAIS KANA KWAMBA NCHI HAINA MATATIZO. KWA MWENENDO HUO SIJUI KAMA MATATIZO YATATATULIWA. TUMECHOKA KUSIKILIZA PONGEZI ZENU, ZUNGUMZIENI MATATIZO YA SASA YANAYOTUKABILI WANANCHI SIO MBUNGE ANAPATA NAFASI YA KUCHANGIA HOJA BUNGENI,ANAISHIA PONGEZI TUUUUUUUU HAKUNA ANAJADILI MATATIZO YA SASA YA TAIFA.

    ReplyDelete
  2. kwa mtazamo wangu Spika makinda amewekwa kwa maslahi ya rostam, kikwete na lowasa ndio maana hoja inayogusa chama tawala anahamaki na kuwa mbogo bila hata kuitathimini, mathalani mbunge Lema aliomba mwongozo wa spika yeye akahamaki badala ya kutoa majibu, sasa makinda, lowasa, rostam na kikwete mnaipeleka ccm kaburini subirini kimbunga cha nguvu ya uma 2015

    ReplyDelete