11 January 2011

TTCL sasa kuuzwa Vietnam-TEWUTA

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) kimesema serikali ina mpango wa 'kuiuza' tena Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa mwekezaji kutoka Vietnam, hatua ambayo wanaamini
itaifanya izidi kudumaa.

Akizungumza na Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Bw. Junus Ndaro alisema kuwa uwekezaji huo hauna nia nzuri, bali kuiuza TTCL kwa gharama poa.

"Upo ushahidi wa kutosha kuwa bado serikali haijajifunza kutokana na matukio ya nyuma. Kwa mara nyingine serikali inakusudia kuleta kampuni nyingine ya simu (VIETEL) kutoka Vietnam kuwekeza ndani ya TTCL, mazungumzo bado yanaendelea kwa pande zote mbili, na sasa ipo kampuni nyingine kutoka India (Airtel) nayo imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza ndani ya TTCL," alisema.

Alisema kuwa TEWUTA wanatambua kuwa nia yao ya kuwekeza si nzuri, zaidi sana madhumuni yao ni kutaka kuimiliki TTCL yao ambayo ni mali ya Watanzania kwa gharama poa.

Bw. Ndaro alisema Tanzania haipaswi kutegemea makampuni kutoka nje, kwani waliowahi kupewa dhamana ya uendeshaji wa TTCL kama wataalamu hawakuwa na uwezo wa kitaaluma wa kusimamia na kuleta mabadiliko yoyote ya mawasiliano ndani ya kampuni hiyo.

"Kwa muda mrefu serikali yetu ilikuwa inafanya makosa kwa kuruhusu na kuleta kampuni za nje na kuzipa dhamana kubwa ya utawala pasipo kufuatilia utendaji kazi wake," alisema.

Alisema kutokana na serikali kuruhusu uwepo wa makosa hayo, kampuni hizo zilifuja fedha ovyo pasipo kuwekeza kwenye miundombinu ya mwasiliano, bali ni katika kuhakikisha kuwa TTCL inatoweka katika huduma ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa Bw. Ndaro, TTCL inao uwezo wa kujiendesha iwapo itapata sapoti kidogo ya serikali, hivyo aliiomba serikali idhamini mkopo wa sh. bilioni 70 ili kampuni hiyo iweze kujiimarisha katika mtandao wake na kuingia sokoni kibiashara na kuwa ya kisasa.

Bw. Ndaro alisema kuwa wanaamini serikali itakapoimarisha TTCL na kuwa bora katika maeneo ya sauti na data, nchi itakuwa imepiga hatua kubwa mbele katika sekta ya mawasiliano hapa nchini.

"Nchi yetu haipaswi hata kidogo kutegemea kampuni kutoka nje ya nchi, kampuni zilizopo hapa zinajiendesha na muda wowote wanaweza kusitisha huduma zao mara watakapoona hawapati faida waliyoitarajia.

"Mfano kampuni ya (anaitaja) imeuzwa mara kadhaa, tutambue kuwa haya ni makampuni ya kibepari, yapo kibishara tu na si uimarishaji wa huduma hapa nchini," alisema.

Alisema kuwa fedha zinazohitajika ni lazima zipatikane kwa njia yoyote ile, serikali inaweza kuisadia TTCL kupata fedha hizo kwa njia ya mkopo kutoka taasisi za fedha za ndani na nje hususani katika mabenki au kampuni kubwa za vifaa vya mawasialino zilizopo nje ya nchi.

TTCL iliwahi kuletewa mwekezaji mbia, MSI/Detecon, na hadi inamaliza mkataba wake mwaka 2006, kampuni hiyo ilizaa kampuni ya Celtel, huku ikidaiwa kuwa mwekezaji huyo hakumaliza gharama za uwekezaji kadri ya mkataba.

Kampuni ya MSI/Detecon iliyokubaliwa na serikali kuwa mbia wa TTCL tangu kusainiwa kwa mkataba Februari, 21  2001, 'hadi inaondoka mwaka 2007, ililipa dola 60 milioni tu ambazo ni nusu ya gharama.

Kwa mujibu wa mkataba, MSI/Detecon ilikuwa inachukua hisa 35 kwa gharama ya dola 120 milioni (sawa na sh. 150 bilioni), lakini walichuma karibu sh. bilioni 4 kila mwaka tangu 2001 hadi Septemba 2005.

8 comments:

  1. Hivi hata kama twasema huu ni uchumi huria tuliouiga, kwani ni lazima kubinafsisha kila kitu hata njia kuu za mawasiliano?? Hivi tumekosa watanzania wazalendo wakuimarisha na kuendeleza makampuni yetu?? TBC inatarajiwa kubinafsishwa, TTCL nayo, madini ndio hayooo, bandari, Air Tz, reli n.k tutafika mawaziri wetu na Raisi wetu mchakachuaji?? Hamuwaonei huruma watanzania?? Wageni wanachukua vyao tu eeh?? Katiba mbovu ya sasa inasema siasa na uchumi wetu ni wa ujamaa na kujitegemea (Werema uisome ili usikatae mabadiliko yake; stupid!!) Ama hakika mwalimu alisema tutabinafsisha hata magereza!! Tuliahidiwa mvua ya kutengeneza toka Vietnam au tumesahau?? Shame on Tanzanians??!!

    ReplyDelete
  2. Mkwere anachukua chake mapema. Nasubiri hizo ahadi zake kibao. Hata pesa hana anatembeza bakuri tu nje ya nchi hata wao watasema basi. Kama tungekuwa na akili tungeiga Rwanda. Sisi ni kununua mashangingi basi. Hakuna baraza la mawaziri kila mtu anasema lake. Vizee vilivyochoka toka DSM na yule shetani Shekhe yahya marehemu ndo wasemaji wa kuu wa ikulu. Tatizo hatuna rais. Muda mwingi anafikiria afya yake na namna ya kuongeza wake.

    ReplyDelete
  3. Serikali ya Kikwete sijui wanamawazo gani; hivi nyara muhimu za serikali zitakuwa zinapitishwa katika mtandao wa watu binafsi? huu ndio mwanzo wa uchakachuaji na kutokuwa naserikali makini? sitaki sema zaidi ila Tanzania tujihurumie kwani mambo si mambo...! Siku za karibuni katika ufahamu wangu niomeshuhudia kiwanda pekee cha matairi TZ kinafungwa? Mungu uturehemu

    ReplyDelete
  4. Sio lazima wanunue tulizozijenga tayari. Kama kweli wana nia ya KUWEKEZA waombe kujenga njia mpya ya mawasiliano sio kununua iliyopo. Hizo biashara za KIHUNI. Serikali jionyesheni kuwa nanyi pia mnaweza kusimamia. Kama tuna weza kuwa na fedha za kuilipa DOWANS billion miamoja tutashindwaje kuwasaidia TTCL shilingi billion 70? Kikwete, Pinda, Werema na Sipika Makinda AMKENI sasa. Wananchi tumechoka sana kusikiliza ufinyu wa mawazo yenu. tuliwachagua tuliwaamini kuwa mtasimamia miradi kama kunashida ajirini wataalamu toka huko nje.

    ReplyDelete
  5. Huu ni wendawazimu.
    Lazima kuna mtu anafaidika na madili haya.
    Ilikuja Celtel, ikaneemeka na miundo mbinu ya TTCL. Tukasikia wamenunua management toka Canada, watu wakala ikatoka. leo tena Wavietnam au airtel iliyotokana na CELTEL iliyotokana na TTCL?

    Hii yote ni siasa kuingilia biashara. Tangu lini director wa kampuni anateuliwa na rais?

    ReplyDelete
  6. Mimi nina hakika, huyu anayetukana Rais, na wakwere wote ni huyu huyu mwandishi wa majira. Majira gazeti nilipendalo linashuka hadhi. Afukuzwe kazi mwandishi haraka. Asijifanye yeye ni anonymous.

    ReplyDelete
  7. Kidogo wakati mwingine serikali iwe na busara kwenye ufanyaji wa maamuzi,nyinyi mliokuwa humo serikalini tumewaweka kama wasimamizi wetu na waangalizi wa mali zetu,msiwe kila mkikaa huko kwenye maofisi yenu mkinywa kahawa za bure na kujifanyia maamuzi ambayo hata hayaeleweki.Hizo ni mali zetu,msije mkaifanya kampuni ya simu ikawa kama Tanesco(Tafadhalini).

    Hilo ni shirika muhimu sana katika kulipatia taifa kipato chake.Bandari mlishagawa,Tanesco nayo haijielewi,na simu nao ndiyo haooo....

    Mimi nafikiri bora tubinafsishe barabara zetu kwa hao wawekezaji na watu wazitumie kwa kulipia kwani haya yatakuwa ni maendeleo makubwa(mtazamo wangu)Barabara hata kwenye nchi zilizo endelea mfumo huo pia upo.

    Oneni huruma wakuu wetu,tuwe na imani na vyetu si vyenu bali vyetu sote.

    ReplyDelete
  8. tunalalamika nini jamani??TTCL imekukuwepo miaka kibao ikitokana na posta na simu.ilikuwa ikiongozwa na watanzania hao hao.walichofanya ni kuiba tu.leo wamekuwa na uchungu na nchi?umetoka wapi.kwani wameua RTC,TRC na makampuni kibao yaliyoanzishwa enzi za ujamaa wa mwalimu

    ReplyDelete