26 November 2010

Mawaziri wapya walonga.

*Tibaijuka asema ni kuchapa kazi, vitendo vitaongea zaidi
*Ngeleja: Mgao wa umeme kufikia mwisho, umeme hadi vijijini
*Chami aonya waliochukua viwanda lakini hawaviendelezi
*Maige awatolea macho wasafirishaji wa magogo, wawindaji


Na Tumaini Makene.

SIKU moja baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika nafasi ya uwaziri, baadhi ya mawaziri wameeleza matarajio yao na jinsi walivyojiopanga
kuwahudumia Watanzania.

Takribani mawaziri wote ambao Majira liliwapata jana na kuwa tayari kuzungumza, walionekana kumshukuru Mungu, Rais Kikwete na wapiga kura wao katika majimbo yao ya uchaguzi, wakisema 'utatu' huo ndiyo uliosababisha wao kupata nafasi hizo, huku wote wakiahidi kuwatumikia Watanzania kwa mujibu wa sheria, sera, kanuni na miongozo iliyopo.

Miongoni mwa wateule hao wa rais, Waziri mteule wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Ana Tibaijuka ameweka bayana kuwa, "sasa ni wakati wa kuchapa kazi, vitendo viongee zaidi si maneno."

Prof. Tibaijuka ambaye kwa muda mrefu tangu alipoondoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (CKD) alikuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa katika Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT), alisema kuwa anaamini ameteuliwa katika nafasi hiyo ikiwa ni fursa ya kuwatumikia Watanzania, kwa kutumia ujuzi, uzoefu na uwezo alionao katika sekta hiyo.

Alisema kuwa anashukuru kuwa taifa limekuwa na imani naye alipoamua kurudi nyumbani na kuwania ubunge, hivyo wajibu wake utakuwa ni kulipa imani hiyo kwa kutekeleza kazi zake kuwatumikia Watanzania, kwa namna aliyokuwa akifanya alipokuwa UN-HABITAT.

"Nawashukuru kwa kweli Watanzania kwa imani kubwa ambayo wamekuwa wakiionesha juu yangu, tangu nilipoamua kurudi nyumbani na kuwania ubunge...kwa kweli nimekuwa nikitafakari sana imani hiyo ambayo wamekuwa wakinipatia...nawashukuru kwa kuona kuwa nina mchango ambao naweza kutoa kwa nchi yangu.

"Hivyo sasa kazi sasa iliyo mbele yangu kwa kushirikiana na wenzangu ni kuendeleza masuala ya makazi, kama nilivyokuwa nikifanya Umoja wa Mataifa...sasa ni wakati wa kuchapa kazi kwa kasi kama mwenge (kicheko)...vitendo vinapaswa kufafanua maana ya maneno juu ya nini hasa tunataka kufanya...itakuwa ni vitendo zaidi si maneno,' alisema Prof. Tibaijuka.

Alisema kuwa anatambua changamoto zilizopo katika wizara yake katika kuwahudumia Watanzania, ambapo ni pamoja na masuala ya migogoro ya ardhi, uendelezaji wa makazi hasa mijini ambako sasa idadi kubwa ya watu inahamia na kuishi.

"Tunatambua kazi iliyo mbele yetu ni kubwa... kushughulikia suala la ardhi, maendeleo ya makazi mijini ambako watu wengi sasa wanakimbilia na kuzidi kuongezeka...asilimia kubwa ya watu sasa wanaishi mjini tena katika makazi yasiyopangwa,...eeeh makazi holela...tusipojipanga kuwapokea itakuwa shida, lakini pia wanaishi katika maisha yapi, maisha yao ni bora?

"Hawa ndiyo wanapaswa kuwa soko la watu wa vijijini, lakini pia ili hao watu wazalishe huko vijijini kwa ajili ya wakazi wa mjini, wanahitaji makazi mazuri...kwa kweli hivyo ni vitu vya msingi sana tumepewa kuvifanyia kazi," alisema Prof. Tibaijuka.     

Kwa upande wake waziri mteule wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja alisema kuwa jukumu kubwa lililo mbele yake pamoja na wenzake katika wizara hiyo ni kuhakikisha tatizo la kukatika au mgawo wa umeme linamalizika.

Ingawa alikuwa makini katika kuhakikisha haingii katika utata, pale aliposema 'lakini ni muhimu ikatofautishwa, maana kuna wakati inaweza kutokea kuna matatizo ya mitambo kuharibika hicho ni kitu ambacho kwa kweli kiko nje ya uwezo, maana isije ikatokea hivyo watu wakasema mbona tuliambiwa matatizo la umeme sasa basi.

"Lakini kwa kweli nia yetu ni kuhakikisha kuwa matatizo ya umeme yanapungua kabisa kama si kumalizika, tuna miradi mingi sana ambayo nikikutajia yote utaandika makala...ipo ile inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ipo inayosimamiwa na MCC (Millenium Challenge Corporation) na ile ya Benki ya Afrika ADB.

"Miradi ya REA ambayo iko katika mikoa takribani 16 inahusisha jumla ya bilioni 103, ile ya MCC ni dola za Marekani milioni 206, mikoa ya Mwanza, Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa, Tanga, Kigoma upande wa Mto Malagarasi...ADB wenyewe wako Mwanza, Shinyanga, Bukombe, Arusha na Dar es Salaam," alisema Bw. Ngeleja.

Aliongeza kuwa jukumu lingine litakuwa ni kuhakikisha kuwa sheria na sera mpya ya madini inafanya kazi kwa ajili ya maslahi ya Watanzania, akisema kuwa hizo ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wadogo. Pia kuhakikisha kuwa manunuzi yote yanayofanywa na makampuni ya uchimbaji madini yanafanyika ndani ya nchi.

Dkt. Cyril Chami ambaye ni Waziri mteule wa Viwanda, Biashara na Masoko alisema kuwa wizara yake itakuwa na changamoto ya kuhakikisha inatimiza matarajio ya Watanzania katika sekta hiyo ambayo yameoneshwa katika hotuba ya Rais Kikwete wakati akizindua bunge la 10 hivi karibuni.

"Napenda sana kuwashukuru watu wangu wa Moshi Vijijini walioamua kwanza kuniamini hata rais naye akaniamini kushika nafasi hii...Unajua katika wizara hii kuna changamoto kubwa katika sekta zake tatu za viwanda, biashara na masoko...kila sekta inayo majukumu yake tofauti.

"Kama ulivyosikia katika hotuba ya mheshimiwa rais wakati wa kufungua bunge, alisema kuwa tuna matumaini katika eneo la wizara hii, kazi yangu ya kwanza ni kuhakikisha kuwa kwa kushirikina na wenzangu pale kasi iliyokuwepo inaendelezwa au kuongezwa...unajua unaposikia kuwa Tanzania tumefikia hatua ya kuuza bidhaa nyingi Kenya kuliko wao walivyouza kwetu si kitu kidogo.

"Tunatakiwa kufikia mwafaka na wale waliochukua viwanda ambavyo sasa havifanyi kazi, ama tuvichukue tuwapatie watu wengine au tuviache hivyo hivyo au tuwaachie vifanye kazi nyingine lakini katika makubaliano maalumu...tuna jukumu la kuwahimiza Watanzania kuanzisha viwanda vipya, kwani gharama ya kuendeleza kuwekeza katika viwanda vya tangu enzi za Mwalimu Nyerere inaweza kuwa sawa na kuanzisha vipya.

Kwa upande wake waziri mteule wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige alisema kuwa amejiandaa kutekeleza na kusimamia majukumu yake kwa mjibu wa sheria na kanuni zilizopo bila ya kubabaika, huku akitambua kuwa wizara anayoiongoza ni nyeti na moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa nchi.

"Sina mengi ya kusema kwa kweli, unajua mimi pale ni mzoefu, kwa hiyo sitakuwa na muda wa kusema labda bado najifunza hapana, ni jukumu la kuwaweka pamoja wadau wote wa shughuli za utalii ili wajue kuwa tutafanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo...unajua wizara ile ni muhimu sana katika mapato ya serikali.

"Naongoza wizara ambayo najua kabisa kuwa itasaidia kupatikana kwa mapato ambayo yatasaidia serikali kutekeleza ahadi tulizoahidi katika uchaguzi, suala la kuongeza watalii maana yake unaongeza pato la kigeni... natambua changamoto zilizopo za ongezeko la watu na shughuli zao ambazo zimetishia hata maeneo ya hifadhi.

"Kuna masuala ya illegal natural resources utilization (matumizi ya maliasili isivyo halali), kuna masuala ya maadili ya watumishi wetu...ndiyo matatizo katika vitalu na uwindaji haramu na ukataji na usafirishaji wa magogo yote yamo katika mkumbo huo tu wa uzembe na kushindwa kusimamia sheria na kanuni, mimi sioni katika kusimamia hapo kwa uwazi kabisa, straight foward kuzuia hali hiyo," alisema.

11 comments:

  1. Ngereja acha hizo porojo zako...Mimi najua itakuwa kama juzi tu.Maneno mengi kazi hakuna..Unaongelea umeme wakati mgao ndo uko tayari..Kwanza ungetatua la mgao wa umeme ndo uweze kutuambia hayo maneno yako...

    IFAKARA MAN...

    ReplyDelete
  2. Nawapongeza sana Waheshimiwa wateule. Ni kweli tunahitaji vitendo kuliko maneno na kazi ionekane. Nawatakia kazi njema kwa hayo mliyotuahidi ili msiwaangushe wapiga kura wenu na Rais wetu kwa jinsi alivyowaamini na kuamua kuwateua.

    Ushauri wangu ni mumtangulize Mungu kwa kila jambo nae atawasaidia na Mungu awe mstari wa mbele sio maslahi ya kitu kingine maana mkumbuke kesho mtaenda kuapishwa na Mungu atakuwa shahidi. Msije mkapata laana kwa kuapa uongo na kuahidi uongo mbele ya Mungu na wananchi. Mungu halali wala hadanganywi.

    ReplyDelete
  3. Ngeleja, huu mgao unaoendelea nchi nzima sasa hivi bila taarifa raisi ya TANESCO maana yake ni nii? Anza na hilo kwanza.

    ReplyDelete
  4. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 26, 2010 at 12:56 PM

    Wakifanya walichoahidi,Tanzania itaendelea kuliko Afrika Kusini.Wasipofanya,tutawasms 2015.Moja lazima litokee.Subira yavutwa na heri!

    ReplyDelete
  5. Tuone Matendo sio majigambo. hali ya wananchi ni hoi. bei za bidhaa na gharama za maisha kwa jumla ziko juu. shilingi imeporomoka ukilinganishwa na dola ya marekani

    ReplyDelete
  6. Wanaongea leo, kesho walishasahau walichoongea, hapa tusubiri migogoro tu sio mbali kama kawaida yao kugombana na wananchi bado wanasherekea vyeo hawajaingia ofisini, yetu macho.

    ReplyDelete
  7. fyongo tupu ngeleja,mahanga,mkuchika,sophia simba na hawa ghasia vichwa maji tupu

    ReplyDelete
  8. BWANA MAIGE NI BORA USISEME KITU MUD HUU KWANI WIZARA ULIYOPO SIDHANI KAMA UTAIWEZA KWA VILE, NI WIZARA YA DOLLA, WAFANYABIASHARA WENGI WA IDARA HIYO NI WATU WANOMILKI MADOLLA MENGI NA WANAPENDA KUHONGA MAWAZIRI, HIVYO KELELE ZAKO HIZI ZA MWANZO ZITAZIDISHA UKUBWA HONGO UTAKAYOPEWA, WEWE SUBIRI UTAONA MAWAKALA WA MAKAMPUNI HAYO WATAKULETEA BAHASHA BAHASHA NA HATUTAKUSIKIA TENA NA TAMBO ZAKO.KWELI WEWE UNAWEZA KUZUA UHALIFU WA VITALU, UWINDAJI HARAMU WA WATU KUTOKA MATAIFA YA KIGENI WANAUA WANYAMA BILA HATA VIBALI,

    ReplyDelete
  9. Kindly note that becoming a leader can not be one man show, they all need our maximum support. since we see what is happening in the field and we have to report and they have to act promptly.
    wakikubali hilo then we will have very effective team, otherwise mhhhhhhhhhhhh.

    lakini najua hiyo team ni ngumu vilevile maana acess na hawa jamaa... waweza kufight 5yrs na usiwaone

    ReplyDelete
  10. POROJO TU NI HAOHAO TU, HAMNA LOLOTE.

    ReplyDelete
  11. Watanzania bado vichwa maji, tunaahidiwa asali halafu mwishowe unapewa nta na kuambiwa asali mlishapewa si unaona nta hii!!! Tatizo sio watu ila mfumo mzima wa serikali. Hakuna mwongozo wa majukumu ya wafanyakazi wa serikali. Hamisi anatakiwa ajue nini wajibu wake kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni. Rehema anatakiwa ajue wajibu wake jumatatu hadi ijumaa. Halafu mkurugenzi anatakiwa ahakikishe wafanyakazi wake wanatimiza hayo la sivyo wanawajibishwa. Waziri anatakiwa akague ripoti ya wakurugenzi kila wiki na ajue nini wanafanye wiki ijayo. Hata ukiwa na magufuli mia mbili kama wafanyakazi hawana majukumu ya msingi na elimu kazi, uwepo wao ni bure. Nchi zilizoendelea hakuna bosi wala tarishii. wote wana majukumu na wana kuwepo kazini muda sawa na likizo ni sawa. Ofisa uajiri hana huruma na bosi akichelewa mara tatu mfululizo. tukifikia hapo tutaendelea, la sivyo vigogo wataendelea kuishi kama peponi na mkulima ataendelea kulala kwenye tembe huku akitibiwa na asprini feki zilizo expire muda wake.

    ReplyDelete