19 August 2013

WAVAMIZI MISITU WAPEWA WIKI MOJA KUONDOKA



Na Steven Augustino, Tunduru
MKUU wa Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ametoa wiki moja kwa wakulima na wafugaji wa jamii ya Kisukuma kuondoka katika eneo la hifadhi ya msitu wa Shamba la bibi vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao
.Nalicho alitoa agizo hilo baada ya Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kufanya ziara ya kushtukiza katika msitu huo na kujionea hali halisi ya uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu iliyopo katika hifadhi hiyo inayounganisha Vijiji vya Nangunguru, Majala na Mkalekawana katika Tarafa ya Nampungu Kata ya Nandenbo wilayani humo.
"Natoa siku saba kwa watu wote waliovamia msitu huu wa hifadhi waondoke, haiwezekani watu waendelee kuishi wanavyopenda na kuharibu mazingira katika vyanzo vya maji na hifadhi ya misitu kana kwamba Serikali haipo," alisema
Alisema katika kutekeleza agizo hilo kwa watakao kaidi amri hiyo ofisi yake itatumia sheria Namba 24 kifungu cha 16 kinachompa mamlaka ya kuharibu makazi au mali baada ya mhusika kukataa kutekeleza amri halali ya iliyotolewa na mamlaka husika.
Pamoja na kutolewa kwa amri hiyo dhidi ya wakulima na wafugaji hao DC, pia aliwataka watendaji kata na vijiji kwa kushirikiana na maofisa Tarafa wilayani humo kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwaelekeza wafugaji
kufuata taratibu za kuonana na viongozi wa vijiji husika, kufanya mikutano inayo wahusisha wananchi katika maamuzi ya kuwapokea wafugaji hao ili kuyaondoa maeneo yao katika migogoro ya aina hiyo.
"Kwavile mifugo ni muhimu kwetu na endapo itatumika vizuri na kwa kuzingatia kanuni, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Serikali, italeta manufaa kwa
Wananchi wetu," alisema Nalicho na kuongeza kuwa mtindo wa kuishi kwa uhasama kati ya wafugaji na wakulima hauwezi kuwa na tija.
Awali akizungumza katika ziara hiyo Ofisa misitu wa Wilaya ya Tunduru, Rashid Mtotela alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wakulima na wafugaji hao waliuvamia msitu huo mwaka 2006 /2007 na kuendelea kujiimarisha kila mwaka baada ya kubaini kutokuwepo kwa vikwazo vyovyote kutoka serikalini.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nangunguru, Said Rashid Mkwekwele, Mtendaji wa Kijiji hicho, Zainabu Twaha na Ofisa Tarafa wa Nampungu, Joshua John waliwalaumu baadhi ya wakuu wa Idara katika halmashauri ya wilaya hiyo kuwa umekuwa na kigugumizi katika ufuatiliaji na uchukuaji wa maamuzi juu ya migogoro hiyo

No comments:

Post a Comment