19 August 2013

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WANAOTUMIKISHA WATOTO



 Na Elizabeth Joseph, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaojihusisha na biashara haramu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima.Tamko hilo lilitolewa juzi mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi wakati akihutubia katika hafla ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Dkt. Nchimbi alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kutumia mwanya wa maisha ya watoto hao kuwafanyisha biashara ya dawa za kulevya pamoja na ukahaba jambo ambalo ni kuwanyima haki zao watoto na kuwanyanyasa.Aliongeza kwa kuwataka watu hao kuanza kuwatumia watoto, mke, mume ama familia zao katika biashara hizo ili wajue endapo kuna raha ama karaha kwa kufanya vitendo hivyo.
"Wauzaji wa dawa za kulevya na wanaowatumia watoto hawa kuwafanyisha biashara hizo waanze na watoto ama wake zao ili wajue uchungu au kama kuna raha yoyote kwa kuwafanyia hivyo," alisema Dkt. Nchimbi.
Aidha aliwataka viongozi wa siasa nchini hasa wanaoishi mkoani hapa kutothubutu kuleta vurugu za kisiasa zitakazoweza kuvuruga amani ya wananchi pamoja na maisha yao kwa ujumla.
Dkt. Nchimbi pia aliwataka watu wenye uwezo wa mali kutumia mali zao kuwasaidia watoto hao kwakuwa wengine kati yao ndiyo chanzo cha kupatikana kwa watoto hao kwa kutumia pesa zao katika anasa na kuwatelekeza watoto hao.
Kwa upande wake Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Musa Rajabu aliwataka viongozi wa dini nchini kutowadharau watu wasiojiweza pamoja na kuwataka watu ama makampuni yenye mali kuacha tabia ya kukumbatia mali zao wakati kuna jamii inayohitaji kusaidiwa kwa kuwapa chakula, mavazi, elimu na mambo mengine.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya hafla hiyo, Faustine Mwakalinga alisema kuwa waliamua kufanya sherehe hiyo ili kukaa na kufurahi kwa pamoja na watoto hao na kuitaka jamii kuchukua jukumu la kubadili mazingira magumu ya watoto hao na kuyafanya mazuri na yenye hadhi.Jumla ya watoto 420 walishiriki katika hafla hiyo walitoka katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto pia hafla hiyo ilidhaminiwa na makampuni ya simu za mkononi pamoja na Aza

No comments:

Post a Comment