- MECHI YA NGAO YA JAMII YAINGIZA MILIONI 208/-
Na Amina Athumani
UONGOZI wa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania
Bara Yanga umesema kwa sasa utajipanga upya baada ya mchezo wa juzi dhidi ya
Azam.Mchezo huo wa Ngao ya Jamii ambao ni
kiashiria cha msimu mpya wa ligi 2013-14, ulichezwa jana kwenye uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam,
ambapo Yanga ilifanikiwa kushinda bao 1-0.
Meneja wa timu hiyo Hafidhi Salehe
alisema kwa sasa sio kipindi cha kulegalega kwao kwani wanahitaji kujiandaa vya
kutosha katika dakika hizi za mwisho ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika
ligi hiyo.
Salehe alisema timu hiyo itaendelea na
ratiba yao ya
mazoezi leo katika uwanja wa shule ya Loyola, huku wakihakikisha wanafanya
mazoezi ya hali ya juu ili kuhakikisha wanaingia katika msimu mpya wakiwa fiti
zaidi.
"Ingawa tumeanza vizuri katika
mechi hii ya kukaribisha ligi, lakini tunahitaji mazoezi zaidi kabla ya
kujitupa uwanjani Agosti 24 kuanza ligi na kwa mujibu wa kocha mkuu Ernie
Brants ni lazima timu ipate mazoezi ya ziada ili kuhakikisha tunatetea ubingwa
wetu," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa wachezaji
ambao waliinua katika mchezo huo Kelvin Yondani na Ally Mustapha wanatarajia
kujiunga na timu kuanzia kesho kutokana na hali zao kuendelea vizuri lakini
wachezaji wengine waliosalia wapo fiti.
Wakati huo huo, mechi
hiyo ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza
sh. 208,107,000. Washabiki 26,084 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo
ilimalizika kwa Yanga kuifunga Azam bao 1-0.
Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo
uliokuwa kama ifuatavyo, asilimia 18 ya kodi
ya ongezeko la thamani (VAT) sh. 31,745,135.59, asilimia 10 ya mchango wa
kusaidia jamii sh. 20,810,700, gharama ya tiketi sh. 7,309,866.
Uwanja sh. 22,236,194.76, gharama za mchezo sh.
13,341,716.86, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 5,188,445.44, TFF
sh. 13,341,716.86 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
6,670,858.43. Kila klabu imepata mgawo wa sh. 43,731,183.0
No comments:
Post a Comment