23 July 2013

WIZI MTANDAONI WATIKISA BENKI



Revina John na Jazila Mrutu.

UTAFITI umegundua kuwa benki za kibiashara na taasisi binafsi katika nchi za Afrika Mashariki huwa zinapoteza zaidi ya sh. bilioni 80 kwa mwaka kutokana na wizi wa mitandaoni.Afrika Mashariki kwa sasa inaundwa na nchi tano ambazo ni Tanzania, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Rais wa Taasisi huru ya kimataifa isiyokuwa ya Kiserikali inayohusika na Kusimamia na Kutoa Mafunzo na Maarifa ya Mifumo ya Mitandao hapa nchini (ISACA), Boniface Kanemba wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Kanemba alisema kuwa, wizi wa mitandao umekuwa ukifanyika sana katika benki na taasisi mbalimbali zisizokuwa za kiserikali ambapo kiasi hicho cha fedha huwa zinaibwa kila mwaka."Pia matumizi ya huduma za kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu za mikononi yameongezeka kwa kasi, hivyo kuongeza matukio ya wizi yanayohusiana na miamala yake," alisema Rais huyo.

Aliongeza kuwa, mbali na wizi wa fedha kampuni binafsi zikiwemo taasisi za kiserikali zinapoteza taarifa nyingi zikiwemo zile binafsi na nyaraka muhimu za matumizi ya ofisi bila kujua."Kutokana na wizi wa mitandao wa muda, taasisi yetu imeandaa semina ambayo itahusisha nchi tano za Afrika Mashariki, kampuni kutoka nchi za Ulaya, Amerika na Afrika Kusini,ikiwa na lengo la kuelimisha juu ya matumizi ya kompyuta na mitandao yake katika nyanja zote," alisema.

Alisema kuwa, semina hiyo itachukua siku tatu kuanzia Julai 28-30 mwaka huu mkoani Morogoro ambapo itafunguliwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

No comments:

Post a Comment