17 July 2013

WAZIRI MAGUFULI AMSHUKIA MKANDARASI BARABARA YA KUSINI


 Na Masau Bwire, Rufiji
WAZIRI wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli, amempa muda wa miezi minne mkandarasi anayejenga barabara ya Ndundu-Somanga yenye urefu wa Kilomita 57 Kampuni ya M. A. Khalaf & Sons ya Kuwait kuwa ifikapo Desemba 30, mwaka huu awe amekamilisha ujenzi vinginevyo afukuzwe.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Dkt. Magufuli, alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara hiyo uliosainiwa Agosti 16, 2008 chini ya Wizara ya Miundombinu kwa wakati huo.
Akizungumza akiwa eneo la mradi, Dkt. Magufuli alikerwa na kampuni hiyo kufanya kazi ndogo kwa muda mrefu kuliko kampuni yoyote duniani.

"Kampuni hii ni ya ajabu kabisa, imevunja rekodi kwa kukaa eneo la kazi kwa muda mrefu kuliko kampuni yoyote duniani, imejenga kilomita 40 kwa miaka mitano kwa wastani wa kilomita 8 kwa mwaka, wangepewa kilomita 150 ambazo kampuni zingine huzikamilisha kwa miaka miwili na nusu ingeijenga kwa zaidi ya miaka 30,"alisema na kuongeza;
"Naagiza ifikapo Desemba 30 mwaka huu, nataka barabara hii iwe imekamilika, nakuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kila baada ya siku tano ufuatilie kinachofanyika, kama hakuna mabadiliko fukuza atafutwe mkandarasi mwingine mwenye uwezo; vinginevyo nitakufukuza wewe, tena, kampuni hii isipewe kazi nyingine yoyote hata kama ni ya kufagia barabara," alisema, Dkt. Magufuli.
Alisema, mradi wote kama ungemalizika kwa wakati, Serikali ingelipa sh. bilioni 58.8 lakini mpaka sasa tayari imemlipa mkandarasi huyo bil. 59 kutokana na ucheleweshaji.
Waziri Magufuli alisema, endapo mvua itanyesha ndani ya kipindi hicho hataki kusikia magari yamekwama kwenye tope.
Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ulitakiwa uwe umekamilike na kukabidhiwa kwa Serikali ndani ya miezi 30 kwa gharama ya sh. bilioni 58.8.
Mkandarasi huyo alishindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ndani ya kipindi cha mkataba (miaka miwili na nusu) ambapo hadi sasa imeshatumia miaka mitano bila kukamilisha kazi hiyo.
Taarifa iliyotolewa kwa Waziri, Dkt. Magufuli na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, ilieleza kwamba, kwa kipindi cha miaka mitano sasa kampuni hiyo imeweza kujenga Kilomita 40 za barabara hiyo huku 17 zikiwa bado.
Mhandisi Mfugale alisema, pamoja na Kampuni hiyo kujenga barabara hiyo kwa viwango na ubora wa hali ya juu, bado imeonekana kutofaa kutokana na ujenzi wake kuwa wa taratibu, tofauti na ilivyotarajiwa, hali ambayo imesababisha manung'uniko kutoka kwa wananchi.
Alibainisha kwamba uwezo wa kifedha wa kampuni hiyo ni mdogo kutokana na kutokuwa na kipato kingine zaidi ya kutegemea fedha za mradi huo tu. Vifaa vya ujenzi vyote ni vya kuazima na uwezo mdogo wa mtambo wa kuzalisha lami ambao huzalisha Km. 1.5 kwa mwezi badala ya Km 6 hadi 8.
Alisema hizo ni miongoni mwa changamoto zinazofanya mradi huo kuchelewa kukamilika.
Mhandisi Mfugale alisema, tayari wameushauri uongozi wa Kampuni hiyo kurekebisha baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wote kukaa eneo la kazi, kutafuta vifaa zaidi vya ujenzi na kubadili mtambo wa kuzalishia lami ili kazi hiyo iliyosalia iweze kukamilika kabla ya mwezi Novemba mwaka huu.
Meneja mradi wa Kampuni hiyo Waleed Mosalam na Mhandisi mshauri, Wondwosel Djan, waliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ndani ya muda waliopewa Dkt. Magufuli

No comments:

Post a Comment