24 July 2013

WATOTO WASAJILIWA BURE KUPATIWA VYETI



Na Rashid Mkwinda, Mbeya

ASILIMIA 7.7 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ndiyo waliosajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kati ya asilimia 14 ya watoto wote waliozaliwa, ikiwa ni asilimia 23 tu ya wananchi wote ambao wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa nchini. Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika uzinduzi wa mfumo mpya wa usajili wa vizazi kwa watoto walio chini ya miaka mitano takwimu hizo zimekuwa haziridhishi kwa kutambua umuhimu wa usajili na utunzaji wa kumbukumbu muhimu za vizazi mwaka 2011.

 Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo mpya wa usajili kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri RITA, Vicent Mrisho alisema kudorora kwa mfumo wa usajili kumechangia Serikali kukosa takwimu muhimu kwa mipango ya maendeleo ya Taifa.
Mrisho alisema kuwa, kutokana na kuwepo kwa takwimu zisizoridhisha za kumbukumbu za vizazi mwaka 2011, RITA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilibuni mkakati wa usajili wa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wenye lengo la kuboresha hali ya usajili nchini na kuweka kipaumbele kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano bure.

Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema mfumo mpya wa usajili ni sehemu ya ugatuaji wa madaraka kupeleka huduma katika ngazi ya serikali za mitaa.

Alisema, awali usajili ulikuwa ukifanyika katika ofisi za mkuu wa wilaya hali ambayo ilichangia kujitokeza kwa idadi ndogo na hivyo kuleta changamoto inayohitaji mipango mahsusi na kwamba mkakati huu utatoa suluhisho kwa mpango wa maendeleo ya Taifa.

Uzinduzi huu wa usajili wa vizazi na vifo utafanyika katika mikoa mitano ya Mbeya, Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Geita ambapo kwa Mkoa wa Mbeya kutakuwa na vituo 333 vya usajili katika ngazi ya ofisi za watendaji wa kata na vituo vya afya.

No comments:

Post a Comment