22 July 2013

WANANCHI WALALAMIKIA KAMATI ZA MAJI Na Said Hauni, Lindi
WANANCHI wa Kijiji cha Milola Mashariki Wilaya ya Lindi wameilalamikia kamati mbili zilizopewa kazi ya kukusanya maduhuli yatokanayo na michango na mauzo ya maji katika kipindi cha miaka miwili sasa.Madai hayo yametolewa jana na wananchi hao, walipokuwa wakiwasilisha kero zao mbalimbali zinazowakabili kwa Mkuu wa Mkoa huo, Ludovick Mwananzila, katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya mahakama ya mwanzo.

Wananchi hao wamelazimika kutoa kilio hicho kutokana na kuwepo kwa madai kwamba wakazi hao hawataki kushiriki kazi za kujiletea maendeleo yakiwemo kuchimba mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba ya maji kutoka kijiji cha Namtanga hadi kijijini hapo.Inaelezwa kwamba serikali kupitia wizara ya maji imetoa jumla ya sh. milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa mabomba 600 ya maji na kuwasilishwa kwenye kata tayari kwa ajili ya kuyalaza kutoka chanzo cha maji kilichopo Kijiji cha Namtanga hadi Milola.
Akiwasilisha kilio chao kwa niaba ya wakazi wenzake,Ibrahimu Said Malango,alisema wananchi wa kijiji hicho, wanalazimika kususia kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao kutokana na viongozi wao zikiwemo na kamati mbili zilizopewa kazi ya kukusanya maduhuli wa ushuru wa maji kutia ndani michango wanayotoa.Malango alidai kwamba kamati ya kwanza imetia ndani jumla ya sh. milioni 15 na iliyofuata inadaiwa pia kutafuna kiasi cha sh milioni 16. 8 na kufanya jumla ya maduhuli yaliyotafunwa kufikia sh. milioni 31.8.
"Katika suala la kuchangia maendeleo sisi wana Milola tupo mstari wa mbele,tatizo tunakatishwa tamaa na baadhi ya viongozi wetu..sikufahamu kama ziara yako hii utagusia suala la maji ningechukuwa risiti zangu uzione," alisema Malango huku akipigiwa makofi na wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.Malango alisema wananchi walikaa kikao kupitia taarifa ya mapato na kubaini fedha zilizokusanywa zimetiwatumiwa na watu aliowaita kuwa ni wajanja wachache huku hakuna hata senti moja iliyotumika kwa kazi yeyote iliyohusu kusukuma maendeleo ya kata yao.
Alisema mwezi Juni mwaka huu,kamati nyingine iliyoundwa imefanya tathmini na kupata thamani ya fedha zilizokusanywa na kamati ya pili na kubaini sh. 16,800,000 zilizokusanywa zimetafunwa na kamati hiyo yenye wajumbe wanane.
Malango alisema wingi wa mapato yanayopatikana ndani ya kata yao,yangetosha kubadilisha sura ya kata yao,ikiwemo hata ununuzi wa mabasi au matrekta ambayo yangewasaidia kwa kazi ya kusafirisha abiria na kilimo.
Wananchi hao wamesema kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wao,ikiwemo kamati za maji, zilizochaguliwa vipindi vilivyopita kutokuwa waaminifu kunawafanya wananchi wakatishwe tamaa ya kushiriki kazi za kujiletea maendeleo yao.Baada ya kilio hicho, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila amewataka viongozi wa serikali wa kijiji hicho, kuhakikisha wanatumia Sheria na kanuni zilizowekwa za kuwapatia wananchi taarifa za mapato na matumizi yanayoingia ndani ya kijiji chao ili kuondoa malalamiko kwa jamii.
"Ebu mwenyekiti wa Serikali ya kijiji kaa na watendaji wako na mtoe taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji chenu, ili kuondoa malalamiko......, hapa leo wanasema milioni 15 za maji zimetafunwa kumbe inaweza kuwa ni milioni tano tu sasa ni bora mkaeleza ukweli," alisema Mwananzila.Pia mkuu huyo wa mkoa amuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Grace Mbaruku, kuunda tume itakayofuatilia madai ya wananchi hao ili kubaini ukweli wa madai hayo na pale itakapobainika kuwa yana ukweli achukue hatua kwa wahusika.

No comments:

Post a Comment