23 July 2013

WANANCHI WAHOFIA KUMEZWA NA BAHARI



 Na Masanja Mabula, Pemba
WAKAZI wa Shehia ya Msuka katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wameingiwa na hofu juu ya usalama wa nyumba zao baada ya maji ya bahari kuendelea kuvamia nchi kavu kwa kasi siku hadi siku. Wakizungumza jana katika eneo la bandari Msuka walisema kuwa kutokana na hali ya mawimbi ya bahari kuzidi kuitafuna nchi kavu, hivyo wamekuwa na hofu kubwa ya kukosa sehemu ya kuishi kwa siku za baadaye
. Suleiman Assaa Khamisi alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita bahari katika eneo hilo inakisiwa kuwa imechukua eneo lenye urefu wa mita 25 na kusababisha miti mingi ikiwemo minazi kupotea. Aidha, amefahamisha kwamba kutowekwa kwa miti hiyo ambayo kwa sasa imebakia visiki huku baadhi ya mingine ikiwa imetoweka kabisa kwa kung'oka na hivyo kuongeza mmomonyoko ya ardhi katika eneo hilo.
Naye Masahare Nassor Masahare akizungumza na mwandishi wa habari hizi ameitaka Serikali kuangalia uwezekano kuwasaidia katika kutafuta mbinu na njia za kuzuia kazi ya maji ili isiendelee kuyasogelea makazi yao. Alisema kuwa licha ya tatizo hilo kujulikana na baadhi ya viongozi wa Jimbo, lakini bado juhudi za kulitafutia ufumbuzi hazijaonekana.
Ka t i b u wa B a n d a r i y a Msuka Mjawiri Rashid Bakar akizungumzia suala hilo amesema kuwa wamekuwa wakichukua hatua za kupambana na tatizo hilo , lakini juhudi zao zimeshindwa kuleta mafanikio. Alizitaja baadhi ya hatua ambazo uongozi wa bandari umezichukua katika kukabiliana na hali hiyo kuwa ni pamoja na kupanda miti kandokando ya bahari na kuweka viroba vyenye mchanga sungo sungo ili kuzuia hali hiyo. Mjawiri alieleza kwamba, iko haja kwa serikali kuelekeza nguvu zake katika eneo la Bandari ya Msuka kwa kuhakikisha kwamba inajenga ukuta ili kuzuia maji ya bahari yasiendelee kuyavamia makazi ya watu.

No comments:

Post a Comment