22 July 2013

URA YAIBANIA YANGA, ZATOKA 2-2



Na Hamis Miraji
TIMU ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), jana iliwabana mabingwa wa Tanzania Bara Yanga baada ya kuilazimisha sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.URA ambayo ipo nchini kwa ziara ya kimichezo, juzi iliifunga Simba mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki iliyofanyika katika uwanja huo.
Katika mechi hiyo, Waganda ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 42 lililowekwa kimiani na Lutimba Yoyo, baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga na kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga, Deogritus Munish 'Dida'.Awali ya Yanga ililifikia lango la URA, ambapo kipa wa Watoza ushuru hao wa Uganda alicheza rafu nje ya 18 na mwamuzi kuamuru ipigwe faulo ambayo hata hivyo haikuzaa bao.
Dakika ya 20 Yanga ililiandama lango la wapinzani wao lakini, Didier Kavumbagu akaikosesha timu yake bao.URA nayo ilizinduka dakika ya 27, ambapo nusura ingepata bao la pili baada ya Ngame Emmanuel kuachia kombora ambalo lilidakwa kiustadi na kipa wa Yanga, Dida.
Kipindi cha pili URA iliingia kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la pili lililopachikwa kimiani na Yoyo, baada ya kupiga faulo nje ya 18.Yanga baada ya kufungwa bao hilo ilikuja juu na kupata bao la kwanza dakika ya 58 lililofungwa na Abdallah Mguli, aliyeingia kuchukua nafasi ya Shaban Kondo.Dakika ya 66 Kavumbagu, aliipatia bao la kusawazisha kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa na Juma Abdul.


No comments:

Post a Comment