25 July 2013

TUWAENZI MASHUJAA KWA AMANI



JESHI la Ulinzi la Wananchi w a Ta n z a n i a ( JWT Z ) linaadhimisha siku ya mashujaa kila ifikapo Julai 25 ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka mashujaa waliopigana na kushinda vita ya Kagera mwaka 1978/1979.Maadhimisho hayo hufanyika mara moja kwa mwaka na mwaka huu yanafanyika leo katika Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba kwenye makaburi ya mashujaa yaliyopo Kaboya.


Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamhuri ya muungani wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt.Jakaya Kikwete ambapo watakuwepo viongozi waandamizi wa Serikali, vyombo vya Ulinzi na Usalama, vyama vya siasa, taasisi za dini na taasisi mbalimbali za kiraia.

Maombolezo ya uwekaji wa silaha za asili, usomaji dua kutoka kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini.

Wachache wanaowafahamu majina ya mashujaa wetu ambao tunawaheshimu lakini wengi wao hawayafahamu kwa majina ila tunafahamu tu ya kwamba walipigana na kufa, katika jitihada za kutetea uhuru wa nchi yetu.Tunawakumbuka na kuwaheshimu.

Leo tunawakumbuka mashujaa hao kwa fahari. Juhudi zao na vitendo vyao vilivyotutia moyo siku za nyuma na vinatutia moyo mpaka sasa. Ni vizuri Taifa likaendelea kuwaenzi mashujaa hao kwa namna ya kipekee kwani hata kwa kuwatangaza majina yao ili waweze kufahamika kwa si wa kizazi hiki hata cha baadaye.

Hali ya amani na utulivu wa nchi yetu umekuwa si wa kuridhisha hivyo kama mashujaa hao wangeeleza namna ambavyo ilivyokuwa katika mapigano na watu walivyokufa nina imani kuwa ingesaidia kupunguza viashiria vya uchochezi wa vita kwa baadhi ya watu wenye mlengo wa kuwania jambo fulani.

Katika kuhakikisha kuwa mashujaa hao wanakumbukwa, Mkoa wa Kagera umepewa heshima kubwa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kitaifa mwaka 2013 ambayo yanaadhimishwa leo katika Wilaya ya Muleba katika Kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya.

Kanali Mstaafu Fabian Massawe ambaye ni Mkuu wa Mkoa anasema kuwa maadhimisho hayo yataambatana na ziara ya kikazi ya Rais Jakaya Kikwete katika mkoa huo.

Anasema kuwa kamati zilizopewa jukumu la kuandaa maadhimisho ni Kamati ya Mapokezi, Usafiri na Malazi, Kamati ya Ujenzi Uwanja na Mapambo, Kamati ya Chakula na Afya, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Burudani, Habari na Uhamasishaji ambazo zote zimefanikiwa kumaliza kazi zake.

"Maandalizi yote yamekamilika na tumepokea wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa, pia nje ya nchi watakaohudhuria maadhimisho hayo," anasema.

Anasema kuwa ni vizuri wananchi wa mkoa huo wakawa wakarimu kwa wageni wote watakaofika kwa kutekeleza majukumu kama Wanakagera .

Kati ya mambo ambayo wananchi wanatakiwa kuyazingatia ni kila mwananchi kuhakikisha maeneo yake na mazingira yanayomzunguka yanaendelea kuwa katika hali ya usafi kama utamaduni wetu. Pia kumwajibisha mtu yeyote atakayeonekana anachafua mazingira yetu.

Anasema kuwa kila mwananchi anatakiwa kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku yenyewe ya Kumbukumbu ya Mashujaa katika eneo la Kaboya.

"Hatuna budi kuwakumbuka Mashujaa wetu kwa sababu ya historia ya mkoa wetu kushiriki katika vita ya kumwondoa adui aliyekuwa amevamia nchi yetu kupitia ardhi ya mkoa huu mwaka 1978 hadi 1979," anasema kanali Massawe.

Anasema kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anaitunza amani na utulivu kama destuli ya mkoa huo na taifa kwa ujumla ili kuendelea kuwaenzi mashujaa kwa amani na utulivu.

Katika kuhakikisha kuwa sikukuu hiyo inaadhimishwa kwa amani na usalama, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha amani na utulivu vinatawala wakati wote.

"Kwa mwananchi yeyote atakayeona viashiria vya uvunjifu wa amani atoe taarifa mara moja ili taarifa hizo zifanyiwe kazi mara moja,' anasema.

Anasema katika maadhimisho hayo Mkoa wa Kagera umepokea wageni 1,500 wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali pamoja na wageni wengine toka nje ya nchi.

Anasema kuwa Rais Kikwete anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika mkoa huo ambapo anatarajia kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo kama kuweka jiwe la msingi katika ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.

Pia anatarajia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Kagoma- Rusahunga, kuweka jiwe la msingi barabara ya kiwango cha lami Kyaka hadi Bugene,kufungua Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Kanali Massawe anasema kuwa pia rais anatarajia kufungua jengo la kitega uchumi la Chama Kikuu cha Ushirika (KCU Ltd), kuzindua mradi wa maji Muleba, kuzindua kivuko kipya Rusumo (Ngara), kuzindua mradi wa usambazaji umeme vijijini Nyaishozi (Karagwe), kuzindua Wilaya Mpya ya Kyerwa

"Pia rais atazungumza na wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara katika wilaya zetu ndani ya mkoa ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kumsikiliza," anasema.

No comments:

Post a Comment