12 July 2013

TBS YAFUNGA KIWANDA CHA MKATE


 Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango nchini (TBS) limefunga kiwanda cha kutengeneza mikate cha Yami Yami Garden Restaurant kilichopo Posta Jijini Dar es Salaam kutokana na kutengeneza mikate bila kuwa na leseni ya viwango vya ubora wa shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya maofisa wa shirika hilo kufunga kiwanda hicho, Mwanasheria Mwandamizi wa TBS, Baptister Bitaho, alisema pamoja na uongozi wa kiwanda hicho kujitetea kwamba wanaendelea na utaratibu wa kupata cheti cha ubora cha TBS, wameamua kufunga kiwanda hicho.

"Uongozi wa kiwanda unajitetea kwamba wanaendelea na utaratibu wa kupata cheti cha ubora, pamoja na utetezi huo, TBS imesitisha uzalishaji hadi pale watakapopata cheti hicho kutoka kwetu," alisema.
Bitaho, aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kusitisha uzalishaji huku wakiwa wanaendelea na utaratibu wa kupata kibari.
Naye, Mkaguzi Lazaro Msasalaga, alisema kuwa shirika hilo limeamua kufanya hivyo kutokana na mzalishaji huyo kukaidi amri ya shirika ya kumtaka afanye utaratibu wa kupata cheti cha ubora.
Alisema zoezi la kufungia viwanda lilianza mkoani Tanga na sasa limehamia mkoani Dar es Salaam ambapo wanafanya ukaguzi kwenye viwanda vya mikate.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwataka wazalishaji wa bidhaa kuthibitisha ubora kabla ya bidhaa haijauzwa sokoni.
"Leo tumeamua kufanya operesheni hii kuangalia kama mikate inayotengenezwa ina viwango vya lazima na kama haikidhi hatua inayofuata ni ya kufunga uzalishaji," alisema.
Alisema kuwa kuna viwanda 15 tu vya kutengeneza mikate nchi nzima ambavyo vimesajiliwa na kutokana na hali hiyo ndio maana wameamua kufanya zoezi hilo.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano, Fatma Omari, alisema kuwa hawakuwa na taarifa lakini wanaendelea na utaratibu ili waweze kufuatilia leseni ya ubora.
"Ni ghafla sana TBS kufunga uzalishaji wa mikate, lakini tunafanya utaratibu kupata leseni," alisema.

No comments:

Post a Comment