24 July 2013

TANROADS MWANZA YAKUSANYA FAINI MILIONI 493.6/-OFISI ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS ) mk o a n i Mwa n z a imekusanya sh.milioni 493.6 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kutokana na kutoza faini magari makubwa ya mizigo na abiria ambayo yalizidisha uzito, anaripoti Wilhelm Mulinda, Mwanza.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Leonard Kadashi, aliliambia gazeti hili jana jijini hapa kwamba, fedha hizo zilikusanywa kwenye mzani wa Usagara Wilayani Misungwi pamoja na Nyanguge Wilayani Magu, kutoka Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu.
Mhandisi huyo alisema kuwa kati ya magari 76,877 yaliyopimwa kwenye mizani hiyo miwili katika kipindi hicho, magari 8,730 yalikutwa yakiwa yamezidisha uzito na hivyo kutozwa faini.
Kutokana na hali hiyo, mhandisi huyo amewataka madereva pamoja na wamiliki wa magari makubwa ya mizigo na abiria kufuata sheria zinazosimamia matumizi ya barabara na kuhakikisha kuwa vyombo vyao havizidishi uzito ili kuzuia barabara zisiharibike mapema.
“Lengo la TANROADS si kutoza watu faini, bali ni kujenga barabara na kuzisimamia na kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa ili barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu,” alisema Mhandisi Kadashi.
Alisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kutunza barabara ili ziweze kudumu kwa muda mrefu bila kuhitaji kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kwa vile serikali inatumia gharama kubwa wakati wa kutengeneza njia hizo.
Pia alisema kuwa wenye magari makubwa ya mizigo kupita kiasi (abnormal) wanatakiwa kuomba vibali TANROADS kabla ya kuanza safari ili kuepuka kutozwa faini ya Dola za Kimarekani 2000.
Aidha, Mhandisi huyo amewaomba wenye magari makubwa ya mizigo na abiria pamoja na wadau wengine wa barabara kutoa taarifa ofisini kwake juu ya vitendo vyovyote vya kuombwa rushwa na wafanyakazi wa TANROADS kwenye mizani ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi yao mara moja.

No comments:

Post a Comment