18 July 2013

TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUWAFIKIA WANANCHI VIJIJINI


Na Darlin Said
 TAASISI za fedha nchini zimetakiwa kuwa na utaratibu u t a k a o r a h i s i s h a upatikanaji wa huduma zaidi za kifedha kwa wananchi wanaoishi vijijini ili kufikia maendeleo endelevu.
Mwito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF), Dkt. Donatilla Kaino, wakati wa kongamano lililolenga kutoa taarifa juu ya matokeo ya utafiti wa hali halisi ya upatikanaji wa huduma za kifedha katika sekta ya kilimo au AgFiMS Tanzania 2011 Demand Side Technical Report kwa maofisa wa wizara.

Alisema upatikanaji haraka na rahisi wa huduma za fedha kwa wananchi vijijini ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Alifafanua kwamba wakazi vijijini ambao shughuli yao kubwa ni kilimo ndiyo wengi zaidi nchini na hivyo litakuwa ni jambo la busara kama taasisi za kifedha zitafikiria kuimarisha huduma zao katika maeneo hayo ili kufikia maendeleo ya kweli.
Alisema huu ni wakati mwafaka kwa watu kujenga tabia ya kujiwekea akiba kama kweli wanataka maendeleo.
"Kujiwekea akiba ni muhimu kwa mtu binafsi, jamii na taifa zima... tunatakiwa kujenga tabia hii kwa watoto mapema iwezekanavyo," alisema.
Awali akifungua mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Bohela Lunogelo, alisema nafasi ya sekta ya fedha ni muhimu kwa sasa kuliko kipindi chochote katika historia ya Tanzania.
Madhumuni ya ripoti ya AgFiMS Tanzania 2011 ni kusaidia maendeleo ya huduma za fedha kuchochea biashara katika kilimo na kufikisha huduma hizo kwa wakulima.
Kwa mujibu wa wataalamu, maendeleo ya kilimo ni njia bora ya kupunguza umaskini. Asilimia 75 ya watu maskini katika nchi zinazoendelea wanaishi vijijini na asilimia 85 ya watu hao wanategemea kilimo kuendesha maisha yao.

No comments:

Post a Comment