24 July 2013

SUMAYE AFUNGUKA URAIS 2015



  •  AHOFIA NCHI KUONGOZWA NA WAUZA DAWA ZA KULEVYA
  • ASEMA HAKUNA TAJIRI ANAYETOA FEDHA BILA MASHARTI
Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amewataka Watanzania kutambua kwamba hakuna mtu tajiri anayetoa fedha na mali zake bila masharti; na kuwa iwapo Watanzania watawaweka madarakani viongozi kwa rushwa, wasitegemee Katiba Mpya itajibu matatizo yao ndani ya jamii.


"Tukumbuke kuwa anayekuhonga ili umpigie kura akishaingia madarakani mkataba wake na wewe uliishia pale ulipomuuzia kura yako na yeye kazi atakayofanya akipata hiyo ofisi au madaraka ni kusaka rushwa na kufisadi mali za umma ili arudishe fedha zake alizotumia kukununua wewe na wenzako," alisema Sumaye.

Sumaye alitoa kauli hiyo mjini Morogoro jana wakati akifungua maadhimisho ya 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).

Alisisitiza kuwa; "Kama huamini wewe nenda ukamwombe fedha iwapo hana kura anayokuomba halafu usikie jibu atakalokupa."Alisisitiza kuwa kiongozi wa aina hiyo ataongeza nyingine (fedha) nyingi zaidi za kukununua tena safari ijayo. "Mtu wa aina hiyo kipaumbele chake si jamii na umma, bali ubinafsi wake na wale marafiki zake waliomfadhili wakampa zile fedha,"alisema Sumaye.

Sumaye alisema hata katiba iwe nzuri namna gani na ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo, kama tutaweka viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo katiba wala haitasaidia.Kiongozi huyo mstaafu alisema ni lazima katiba nzuri mpya iambatane na serikali safi yenye kusimamia masilahi ya umma.

"Huwezi kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata rais kwa rushwa ya kuwanunua wapigakura halafu utegemee katiba mpya itajibu matatizo ya jamii," alisisitiza Sumaye.Alisema yeye ukimuuliza kuhusu katiba tuliyonayo sasa atasema ni ni nzuri tu na tungeweza kufanya marekebisho katika maeneo machache kama pana haja ya kufanya hivyo.

"Tatizo letu liko katika kutekeleza na kusimamia sheria zetu tulizozitunga kutokana na maelekezo ya jumla ya katiba yetu. Baada ya katiba Bunge hutunga sheria mbali mbali kukidhi matakwa fulani fulani katika jamii," alisema na kuongeza;

"Kwa hiyo pamoja na kutengeneza katiba mpya, jambo muhimu sana ni kuwa na serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria zetu ili kulinda yale yaliyoelekezwa katika katiba."

Alisema kuwa katiba itatamka haki ya mtu kuwa na mali na itatamka wajibu wa serikali kulinda mali ya mtu. Alisema katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo mwizi.

Alisema kuwa ili vyote hivyo viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni serikali.Alisema kama serikali haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu, tutaishia kulalamika tu maonevu na maumivu yataendelea kuumiza jamii.
Alisema Katiba Mpya bila kuwa na watu madhubuti, watu waadilifu, wanaochukia rushwa na ufisadi kwa dhati kuongoza nchi yetu haitakuwa na msaada wowote katika kuboresha maisha ya Watanzania."Nataka nieleweke vizuri kuwa mimi sizungumzii serikali yangu iliyoko madarakani, bali nazungumzia Katiba Mpya na serikali itakayozaliwa baada ya hapo, alisema Sumaye na kuongeza;
"Nazungumzia uchaguzi ulioko mbele yetu mwakani na mwaka 2015, simzunguzii mtu yeyote bali naizungumzia tabia mbaya. Najua hata hapa wapo watu wametumwa nendeni mkamsikilize huyo Sumaye leo (jana) atasema nini.Hakuna haja ya kutafiti nitakachosema maana kinaeleweka. Nimesema mimi sitanyamaza kupambana na rushwa na ufisadi na maovu mengine hata siku moja. Wala sitaacha kukemea tabia hizi mbaya zinazoangamiza jamii yetu na taifa letu."

Sumaye alisisitiza; "Kama wewe ni mhusika una tabia zinazofanana na hizo dawa ni kuziacha au uvumilie tu haya maneno yaendelee kukuchoma moyoni."Aliwataka Watanzania wote kupitia wakati huu wa kutengeneza Katiba Mpya waanze kutengeneza v i c hwa n i mwa o s e r i k a l i itakayosimamia utekelezaji wa katiba hiyo kwa masilahi ya umma, yenye uwezo na yenye uadilifu usiotiliwa shaka.

Alisema, kazi ya kukemea uovu na hasa uovu wa rushwa za uchaguzi lazima ifanywe na kila Mtanzania mwadilifu ili waovu hao wasipate uongozi wa kununua maana wataifanya kazi ya kutunga Katiba Mpya ambayo ni kazi ya gharama kubwa iwe imepotea bure.

Dawa za kulevya

Akizungumzia dawa za kulevya, Sumaye alisema tatizo hilo kwa sasa ni kubwa ndani na nje ya nchi na vijana wengi wameathirika.Alisema biashara hiyo ni haramu inayohusisha fedha nyingi na mitandao mipana. Alibainisha kwamba katika baadhi ya nchi duniani, biashara hiyo hukithiri mpaka wahusika huweza kujenga majeshi ya kupambana na majeshi ya serikali ana kwa ana.

"Nchini mwetu hatujafikia hatua hiyo, lakini ikiachiwa ikaendelea yaweza kufika huko. Biashara hii huharibu sana vijana wetu na kugeuka zezeta au wakawa wahalifu wa kutisha," alisema Sumaye na kuongeza; "Kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayosaka ni urais, tumeshajiuliza hizo fedha nyingi hivyo anapata wapi?

Kama anajihusisha na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu watapona? Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea mwaka kesho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu

3 comments:

  1. hahahahaaaaaa..... huyoSumaye hana jipya, kwanza yeye alitakiwa kushtakiwa kwani yupo kati ya walomaliza kuuza hii nchi kwa mikataba mibovu ya madini ambayo mpaka hivi sasa linaligharimu taifa hili changa. "Nyani haoni kundule"

    Sumaye katoi boriti jichoni mwako kwanza , ndo uje uwatolee watz

    ReplyDelete
  2. aloyasema Sumaye yanamantiki kwa mwenye akili timamu. Maneno yake 'hatusemi yeye binafsi' yana mantiki. Na watu hawa wanaweza kupata urahisi sana wa kuangamiza taifa kupitia mgombea binafsi. Bado tunahitaji mtu mwenye udhamini wa chama ili angalau kuwe na baraka za watu wengi kwake yeye kuwania nafasi fulani. Ukiacha wazi ndiyo wwezi, wauza dawa za kulevya, wahujumu uchumu watapenya na kuliangamiza taifa. Mungu ibariki Tnazania na Watanzania!!!! Msese

    ReplyDelete
  3. Sumaye amesema jambo la Muhimu tna sana <NImependezwa na maon yake sasa kazi kwa watanzania kutafakari kuhusu nani anayeweza kutuongoza (kuwa raisi )2015
    Tena kwakuongezea inabidi watanzania wote tuache itikadi za uvyama tuchague Mtu atakayeongoza Taifa letu <TAIFA lililo na matatizo lukuki
    MWISHO watanzania napenda kuwaasa Tuchague kiongozi bora na si bora kiongoz

    ReplyDelete