18 July 2013

SITA MBARONI KUINGIA HIFADHI ZA TAIFA


 Na Martha Fataely, Moshi
WATU sita wanashikiliwa na Polisi mkoani Kilimanjaro na Arusha wakiwemo raia wawili wa Kenya kwa tuhuma za kukutwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya mlima Kilimanjaro (KINAPA) bila kuwa na kibali.
Miongoni mwa watu hao sita watuhumiwa wanne walikamatwa jijini Arusha, watatu wakiwa wa familia moja kwa kukutwa na nyara mbalimbali za Serikali na mmoja kwa kukutwa na silaha inayodaiwa kutumika kwenye ujangili.
Akizungumzia tukio la waliokatwa KINAPA, Meneja Uhusiano TANAPA, Pascal Shelutete alisema watu wawili walikamatwa juzi katika njia ya Marangu eneo la Mandara wakizunguka katika eneo la msitu wa hifadhi hiyo.

Aliwataja raia wa Kenya waliokamatwa ni Robert Mwadime Mwakana (30) na Dickson Kawa Mbole (27), wote wakazi wa Taveta nchini Kenya waliodaiwa kutumia njia zisizofahamika kuingia hifadhini humo.
Kwa watuhumiwa wa familia moja, waliokamatwa jijini Arusha na nyara za Serikali, Shelutete aliwataja kuwa ni Charles Mollel, Alex Mollel na Samwel Mollel ambao walikutwa eneo la Kisongo Olasite jijini humo.
Shelutete alisema watuhumiwa hao wa familia moja walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali ambazo ni mifupa mitatu ya twiga yenye uzito wa kilo 10.4 na mfupa mmoja wa tembo wenye uzito wa kilo tano.
Aidha alisema Hifadhi ya Taifa Arusha kwa kushirikiana na Polisi mkoani humo walimkamata mtuhumiwa mwingine mmoja Elias Sifael mkazi wa Leguruki Nkoasenga kwa kukutwa na silaha aina ya shotgun namba C 139415 inayoaminika kutumika kwa ujangili.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema yupo nje ya ofisi na kuwataka waandishi wa habari kusubiri mpaka atakapokuwa ofisini ili kutolea taarifa tukio hilo

No comments:

Post a Comment