Na Rashid Mkwinda, Mbeya
KIONGOZI wa
dini ya Kiislamu kutoka Msikiti Mtakatifu wa Mecca nchini Saudia, Shekhe Mohamad Al-Hazmi
amevunja ukimya na kueleza kuwa waislamu wanaojiua au kuua nafsi za wengine
kinyume na haki wanafanya dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Shekhe Al-Hazmi ambaye
anafanya ziara katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Arusha na
Kilimanjaro alifafanua kuwa ni haramu kwa waislamu kujitoa mhanga kwa kujiua
kwa madai ya kuipigania dini ya Kiislamu.Akiwa ameambatana katika
ziara hiyo na Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Dhiynureyn Foundation, Shekhe
Said Bin Abri na kutembelea katika msikiti wa Baraa Bin Azb Isanga jijini Mbeya
Shekhe Al- Hazmi alisema hakuna sheria katika uislamu inayoruhusu mtu kujiua.
Akijibu baadhi ya maswali
yaliyoulizwa na waumini wa msikiti huo baada ya swala ya tarawehe ambao
walitaka kujua iwapo baadhi ya watu wenye itikadi ya dini ya Kiislamu huamua
kujiua kwa kujitoa mhanga kwa madai kuwa wanachokifanya ni kuinusuru dini.
Shekhe Al-Hazmi alisema kuwa upo mgongano miongoni
mwa mashekhe wakubwa juu ya suala hilo
na kwamba hata hivyo ni haramu kwa muislamu yoyote kujiua au kuua nafsi
nyingine na kwamba kitendo hicho sio katika maagizo ya dini ya kiislamu.
Alisema kuwa katika zama za Mtume Mussa suala la
kujiua lilikuwa ni sehemu ya kafara ya madhambi lakini katika zama hizi ni
haramu mtu yoyote kujiua na kwamba kwa kufanya hivyo anakuwa amemkosea Mwenyezi
Mungu.
Shekhe Al Hazmi ambaye alikuwa akizungumza kwa
lugha ya kiarabu kupitia mkalimani Shekhe Ibrahimu Bombo aliongeza kuwa yapo
mazingira katika zama hizi ambapo kuna baadhi ya watu wanaamua kujitoa mhanga
na kwamba suala hilo
ni gumu kulielezea kwa kuwa lina hitilafu kwa mashekhe wakubwa wa kiislamu
duniani.
"Mazingira
ya jambo hili ni mazito yanahitaji ufafanuzi wa mashekhe, uislamu umezungukwa
na mambo mengi kwa sasa," alisema Shekhe Al-Hazmi ambaye ni miongoni mwa
maimamu kutoka katika msikiti mtakatifu wa Mecca
nchini Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment