12 July 2013

SERIKALI YALAUMIWA


 Na Rehema Mohamed
WADAU wa elimu nchini, wamesikitishwa na kitendo cha kushindwa kujazwa kwa nafasi 10,074 za kidato cha tano kutokana na kufeli mtihani kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne 2012 na kuitaka Serikali itekeleza kwa vitendo ushauri ambao wameutoa ili kuinua kiwango cha elimu nchini.
Ushauri huo ulitolewa Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti na wadau hao akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizaberth Missokia, ambaye alisema Serikali inapaswa kuwa na mfumo mzuri wa kuandaa walimu wenye sifa badala ya kupeleka vyuoni wale waliofeli.

"Mazingira ya shule yanapaswa kuwa ya kuridhisha, vifaa viwepo ili msingi wa kufundisha uwe imara, wanafunzi wasibebeshwe masomo mengi ambayo hayana faida," alisema Bi. Missokia.
Al i s ema u p o umu h imu wa walimu kupatiwa mafunzo wakiwa kazini na mitaala inapobadilishwa, washirikishwe na kupewa mafunzo ambapo ruzuku iliyotengwa ili kupelekwa shuleni, iwafikie wahusika kwa wakati ili kuwawezesha walimu wanunue vitendea kazi.
"Madai ya walimu yapatiwe ufumbuzi kwani wasipokuwa na kipato cha kutosha ni vigumu kuwa na ari ya kufanya kazi na wale wanaofanyakazi katika mazingira magumu wapewe motisha ili waweze kujituma zaidi," alisema.
Aliwataka Watanzania wasimame imara kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora ambayo ni haki yao kikatiba ambapo mwanafunzi anapokosa msingi mzuri kuanzia ngazi ya chini ni athari kwake hasa anapofika Chuo Kikuu.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Alphonce Kyessi, alipoulizwa uzoefu aliopata kwa wanafunzi wa sasa ukilinganisha na kipindi cha nyuma, alisema vijana wengi vyuoni hawataki kwenda maktaba kujisomea wanafunzi wengi hawasomi kabisa tofauti na zamani, ukishafundisha baadhi yao hawaendi maktaba kusoma na wengine usipokuwa makini hata notisi hawachukui kabisa," alisema.
Alisema idadi ya wanafunzi mashuleni ni kubwa ukilinganisha na nyenzo zilizopo tofauti na zamani ambapo mfumo wa elimu ulikuwa sio mbaya bali nyenzo ndiyo hazipo kabisa.
Naye Profesa Ngemba Maruku kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema kuwa viwango vya elimu vimepungua kwa sababu walimu wamekosa mori wa kufundisha na baadhi yao hawasomi kwa nia ya kujifunza bali wanataka kumaliza masomo.
Aliitaka Serikali ikubali kutumia fedha za kutosha kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuleta mabadiliko kwa kuajiri walimu, kuboresha mazingira ya kazi na ufundishaji. 

No comments:

Post a Comment