12 July 2013

MAN UNITED SHANGWE TUPU THAILAND


BANGKOK, Thailand
KLABU ya Manchester United, juzi asubuhi wametua jijini Bangkok ikiwa ni kituo chao cha kwanza cha ziara yao ya kimataifa wakiwa na kocha David Moyes, ambaye anapata uzoefu wake wa kwanza kwa mashabiki wa klabu hiyo duniani kote.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England, watasafiri zaidi ya maili 20,000 na kutua katika majiji matano ya nchi nne huku wakijiandaa na Ligi Kuu kuwakabili majirani zao Man City na Chelsea ya Jose Mourinho.
Rio Ferdinand, anategemea United wataongeza makali zaidi, kabla ya msimu kuanza kutokana na kutaka kumfurahisha Moyes.
"Ni ukweli kwamba kila mmoja anajaribu kufanya kweli katika ziara hii," Ferdinand alisema katika tovuti ya klabu.
Kwa mujibu wa Daily Mail, Kocha Mkuu Moyes, alipokelewa kwa kishindo na wale waliojitokeza kuipokea United kwenye uwanja wa ndege na kwenye hoteli waliyofikia.
Kazi ya kwanza kwa Moyes, akiwa na Giggs, ambaye amechukua jukumu la kuwa kocha mchezaji msimu huu, ilikuwa kusaini kitabu cha salamu za kheri kwa Mfalme wa Thailand, anayeheshimiwa mno katika nchi hiyo.
Ingawa wachezaji wa United waliruhusiwa kupumzika, mazoezi ya ndani yalipangwa kufanyika baadaye siku hiyo.

No comments:

Post a Comment