Na Hamisi
Nasiri, Masasi
HOSPITALI ya Mji wa Masasi mkoani
Mtwara, Mkomaindo imepokea madaktari bingwa kutoka Shirika la Kimataifa la
AMREF kwa ushirikiano na Serikali kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma ya
matibabu kwa magonjwa sugu ya akina mama bure kwa kipindi cha siku nne.Akizungumza na Majira jana ofisini
kwake kuhusu ujio wa madaktari hao Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt.
George Kumwembe alisema kuwa madaktari hao bingwa kutoka Shirika la AMREF kwa
kushirikiana na Serikali tayari wameshawasili katika hospitali hiyo kwa lengo
la kusaidia kutoa huduma ya matibabu bure kwa magonjwa sugu ya akina mama hasa
yanayohusiana na matatizo ya mfumo wa uzazi.
Alisema kuwa akina mama wengi siku hizi
wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo ya mfumo wa uzazi na kuwafanya wahangaike
katika hospitali za rufaa pamoja na waganga wa kienyeji kwa gharama kubwa
kutafuta matibabu ya magonjwa hayo hivyo uwepo wa madaktari hao kwa siku hizo
nne kutawasaidia kupata huduma stahili na kuweza kupata ufumbuzi wa matatizo
yao mbalimbali yanayowasumbua na kusababisha baadhi yao kushindwa kuzaa kabisa.
Dkt.Kumwembe alisema kuwa kuwepo kwa
madaktari hao sambamba na utoaji wa huduma hiyo kutawapunguzia gharama akina
mama wengi wilayani humo ya kwenda katika hospitali za rufaa ambapo huko
magonjwa ya aina hiyo gharama zake zinakuwa kubwa hivyo akina mama wajitokeze
kwa wingi ili kupata huduma hiyo ambayo inatolewa bure na madaktari hao.
Alisema kuwa baadhi ya magonjwa ambayo
akina mama yamekuwa yakiwasumbua mara kwa mara ni pamoja na uvimbe ndani ya
tumbo la uzazi na kuzipa njia ya uzazi ambapo alidai kuwa moja ya tatizo
linalochangia kuwepo kwa magonjwa hayo yanayohusiana na matatizo ya mfumo wa
uzazi ni pamoja na magonjwa ya kujamiiana.
"Magonjwa haya mara nyingi
yanasababishwa na magonjwa ya kujamiiana hivyo mimi natoa wito kwa akina mama
kuitumia fursa hii kuja hapa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu kwa hawa
madaktari badala ya wao kuendelea kukimbilia kwa waganga wa kienyeji na kwamba
mara wanapokumbwa na matatizo kama haya ni bora kupata vipimo vya kitaalamu
kwanza na si kutafuta mitashamba,îalisema Dkt. Kumwembe.
Kwa upande wao baadhi ya akina mama ambao
walifika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuonana na madaktari hao walielezea
juu ya furaha na waliupongeza mpango huo na kusema kuwa ujio wa madaktari hao
wilayani humo kutawasaidia kufahamu matatizo yao iwapo watafanikiwa kuonana na
madaktari hao na kwamba wameiomba serikali kuwa mpango huo uwe wa mara kwa mara
na kulaumu kwamba siku nne zilizowekwa za utoaji huduma hiyo ni chache
No comments:
Post a Comment