19 July 2013

MABOMBA YA GESI YAWASILI MTWARANa Cornary Anthony, Mtwara
SHEHENA ya kwanza ya mabomba ya ujenzi wa bomba la gesi imewasili mkoani Mtwara na kupokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika hali ya amani na utulivu mkubwa.
Shehena hiyo ya kwanza ya mabomba hayo iliyowasili mkoani hapa jana ina uwezo wa kujenga bomba la umbali wa kilomita 50. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Pinda aliwahakikishia wana- Mtwara kwamba mchakato mzima wa kuchakata gesi utafanyika Mtwara na Songosongo, wilayani Kilwa. Alisema mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi utajengwa na kampuni ya CETDC ya nchini China na kwamba Serikali itatoa zaidi ya dola bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mtambo huo.
Alitoa mwito kwa wananchi wa Mtwara kuwa walinzi wa bomba hilo katika maeneo yao litakakopita kwa kuiga mfano wa wenzao wanaoishi maeneo inakopita Reli ya Kati. Waziri Pinda alisema fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kiasi cha dola bilioni moja zimekopwa kutoka Benki ya Exim ya China kwa mkopo wa masharti nafuu ambapo zitarejeshwa Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili. "Kwa hiyo mradi huu ni wa Watanzania na sio wa China kama wengine wanavyodhani," alisema. Aliwataka wananchi wa Mtwara kuwa na imani na Serikali kwani kila kitu kitafanyika kwa uwazi.
Waziri Pinda alisema vijiji ambapo bomba hilo litapita watanufaika na umeme. Mbali na kunufaika na umeme, Pinda alisema wananchi wa Mtwara kupitia mradi huo watanufaika na huduma za maji salama, elimu na afya. Mbali na hiyo alisema mapato ya halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara yataongezeka. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Marco Mwanga, aliwataka viongozi wa Mtwara na Lindi kurudi kwa wananchi kuwapa elimu ya kutosha kuhusiana na mradi huo bila usiri.Alisisitiza kuwa ujenzi wa mradi huo hautakuwa na faida iwapo utatumika ubabe.

No comments:

Post a Comment