19 July 2013

KODI YA SIMU NI MZIGO KWA WALALAHOINa Alex Marwa
BUNGE ni chombo cha kutunga sheria na pia ni mmoja wa mihimili mitatu inayounda mfumo wa utawala kulingana na mfumo wa mgawanyo wa madaraka. Mihimili mingine ni mahakama na serikali.Katika bunge la bajeti lililopita lilipitisha mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2013/14 limemalizika hivi karibuni mkoani Dodoma na sifa nyingi alipewa Waziri wa Fedha, Dkt.William Mgimwa, kwa dhana ya kwamba bajeti yake imelenga kumkomboa Mtanzania wa kipato cha chini.

Hali kadhalika pongezi nyingi zilitolewa kwa kile kilichodaiwa ya kwamba wizara yake ni sikivu kwa kukubali kusikiliza kilio cha wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kwa kuongeza mgawo wa wizara mbalimbali kama vile maji, kilimo chakula na ushirika, uvuvi, nishati na madini, habari vijana na utamaduni na michezo. Baada ya bajeti kupitishwa kwa kishindo kinachojiri hivi sasa kinashabihiana sana na ile sheria iliyopitishwa ya fao la kujitoa, ilivyoleta suala la sintofahamu na kusababisha bunge hilo hilo ambalo lilipitisha sheria hiyo kupokea hoja binafsi ya Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo na kukubali kusitisha utekelezaji wa sheria hiyo.

Ikumbukwe awali waziri wa fedha alikuwa amekusudia kutoza kodi ya asilimia 14.5 kutoka asilimia 12 ya hapo awali katika huduma zote za mawasiliano ya simu hii ikiwa ni pamoja huduma ya kutuma na kupokea pesa, ujumbe mfupi yaani sms, intaneti, milio ya simu kwa anayepigiwa, sh.1,000 kwa mwezi kwa kila kadi ya simu na tozo la asilimia 0.5 kama gharama ya kuhamisha fedha kutoka benki maarufu kama ‘sim banking’.Baada ya majadiliano marefu na msimamo wa mwenyekiti na kamati yake ya bajeti kupinga tozo hiyo imekuwa na msaada mkubwa sana hususan kwa Watanzania wa kipato cha chini waliopo maeneo ya vijijini ambao wengi wao hawana sifa za kuhudumiwa na benki.
Lakini pia huduma hii imepanua wigo wa huduma za kifedha vijijini na hivyo ongezeko la kodi katika huduma hii zitaongeza gharama na hivyo kuwaumiza zaidi wananchi wa hali ya chini kwa kuwa hawana mbadala wa huduma za kifedha.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha alikubaliana na maoni ya kamati ya bunge ya kutojumuisha kodi hii ya asilimia 14.5 kwenye huduma ya kutuma na kupokea fedha na kupongezwa ya kwamba wizara yake ni sikivu na hatimaye kubakisha tozo la sh. 1,000/- kwa kila kadi ya simu kwa mwezi na hivyo kila Mtanzania anayemiliki simu ya mkononi atalazimika kuilipia sh. 12,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia mwezi Machi, mwaka huu, Tanzania ina watumiaji wa simu za mkononi wapatao zaidi milioni 27 ambapo kwa mujibu wa Jumuiya ya watoa Huduma wa Simu za Mkononi Tanzania (MOAT) takriban watumiaji wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 8 wako vijijini na matumizi yao kwa mwezi ni chini ya sh. 1,000, na hivyo kodi hii itakuwa ni mzigo mkubwa kwao.Kutokana na idadi hii ya wateja zaidi ya milioni 27 wanaomiliki simu za kiganjani, hii ina maana ya kwamba serikali inatarajia kukusanya zaidi ya sh.bilioni 27, kwa mwezi na hatimaye kukusanya zaidi ya sh. bilioni 324 kwa mwaka.Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha mapato yatakayopatikana kwenye kodi hii ya kadi za simu yatatumika kuchangia sekta ya elimu.
Tofauti na nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea, wenye kipato kikubwa ndiyo walipa kodi wakubwa, hali hii ni tofauti na Tanzania ambapo kutokana na kodi hii ya kadi ya simu, tajiri anayetumia muda wa maongezi zaidi ya sh. 500,000 kwa mwezi na mlalahoi anayetumia sh. 1,000 wote watatakiwa kulipa kodi sawa ya kadi zao za simu.

Kimsingi h a k u n a anayepinga serikali kutoza kodi, bali swali la kujiuliza ni je, serikali ilifanya utafiti wowote kabla ya kufikiria kuanzisha kodi hii?Maswali mengine ya kujiuliza ni kwamba walengwa wa kodi hii ambao ni wananchi walishirikishwa kwa kiasi gani katika mchakato mzima wa uanzishwaji wa kodi hii?

Je, ni wananchi wangapi

wanafahamu kuhusu kodi hii?

Mimi nadhani ni vizuri serikali ikajenga utaratibu wa kuwashirikisha wananchi hususan katika maamuzi ambayo yana waathiri moja kwa moja ili kuondoa manung’uniko.

Mpaka sasa hali ya sintofahamu imetanda na cha kushangaza ni kwamba tayari wananchi wanalipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika vocha za muda wa maongezi kwa hiyo kumuongezea mwananchi kodi nyingine ni kutomtendea haki.

Ufafanuzi wa naibu waziri

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha, Bi. Saada Salum alisema wananchi watakuwa wakikatwa kiasi kisichopungua sh.30 kwenye muda wao wa maongezi kwa siku ili mradi ifikie sh. 1,000 kwa mwezi.

Katika kipindi cha mahojiano kuhusu malalamiko yanayotolewa na makampuni ya simu kuwa kodi hii itamuumiza Mtanzania, mtumiaji wa kawaida alisema wizara haiwezi kujua kwa kuwa hii kodi ndiyo kwanza imeanzishwa na wizara haiwezi moja kwa moja kukubaliana na madai yaliyotolewa na makampuni hayo.

Alisema kuwa ikitokea hivyo na wakisikia kauli ya wananchi ni kwa kiasi gani wameathirika, watalazimika kuangalia nini cha kufanya ila kwa sasa hiyo kodi ndiyo imeanzishwa.

“Hatujasikia kauli ya wananchi wenyewe jinsi gani watakuwa wameathirika na hivi sasa ndiyo kwanza kodi hii imeanzishwa” anasema Bi.Saada.

Aliendelea kwa kusisitiza kwamba hivi sasa mapato hayo ni muhimu sana kwa ajili ya kusaidia bajeti ya serikali.

Kuhusu ushirikishwaji wa makampuni ya simu wakati wa mchakato wa kuanzisha kodi hii, naibu waziri alisema kupitishwa kwa kodi kuna michakato mirefu sana ikiwemo makongamano mbalimbali, na uanzishwaji wa kodi hii kwa kiasi fulani ulishirikisha wadau mbalimbali.

“Inaweza kuwa isiwe kampuni ya simu moja kwa moja lakini walishirikisha sekta binafsi na kwa kawaida kuna muundo mbalimbali lakini mchakato huu umewashirikisha pia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na ikumbukwe kulikuwa na mkakati wa ‘big results now’ na hii ilitokana na resource mobilization,” anasema.

An a s ema k uwa wa t u we n g i walishirikishwa na inawezekana kampuni moja haikushiriki lakini nyingine zimeshiriki au mdau mmoja hajashiriki lakini wadau wengine wameshiriki.

Anasema kwa kawaida serikali huwa inapokea sana ushauri kabla ya kuanzisha kodi, kwa hiyo lazima kuna kampuni mojawapo ya simu itakuwa ilishiriki katika mchakato huo.

Bi. Saada anasema kuwa iwapo wizara itapokea malalamiko rasmi ya wananchi kupitia TCRA itayafanyia kazi kuona athari zake ikiwamo kufanya utafiti na kuona ni jinsi gani kodi hii imeleta athari.

“Tunaona malalamiko yamekuwa yakiandikwa sana kwenye magazeti hata kabla ya kodi hii haijaanza iwapo wizara itapokea malalamiko tutayafanyia kazi,” anasema.

Anasema kimsingi MOAT hawajapeleka malalamiko rasmi zaidi ya kutoa matangazo kwenye magazeti na aliwataka wananchi wasitaharuki kwa kuwa kodi hii itakuwa inakatwa kidogo kidogo sana hata haiwezi kuwaathiri kwa siku nzima na huenda ikawa senti 20 au 30 kutegemeana na matumizi ya simu ili mradi kwa siku moja iwe sh. 30.

Alifafanua ya kwamba na kodi hii haipo kwa kadi zote za simu bali zile ambazo zitakuwa zinafanya kazi na wizara inatambua ya kwamba wapo watumiaji wenye simu zaidi ya moja na sio zote ambazo zitakuwa zinafanya kazi.

Anasema kuwa hana uhakika iwapo mtumiaji atakuwa akioneshwa amekatwa kiasi gani na watumiaji ambao hawaweki pesa wanapokea tu simu hawatatozwa kodi hii kwa kuwa makato yatakuwa yakifanyika kupitia muda wa maongezi.

MOAT

Wakati naibu waziri akisema kuwa mchakato wa uanzishaji wa kodi hii uliwahusisha wadau wa makampuni ya simu kwa namna moja au nyingine, taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari na MOAT imezidi kusisitiza ya kwamba haikushirikishwa katika mchakato huo.

Taarifa hiyo inasema kuwa bali walikutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge ili kupata usahihi wa maana ya huduma za mawasiliano ya simu kama ilivyoainishwa katika mswada wa mwaka 2013, ambapo mawasiliano ya simu yalitafsiriwa kuwa ni huduma yoyote inayotolewa na Kampuni ya mawasiliano ya simu kwa kutuma, kupokea mawimbi, maneno, picha, sauti au habari ya aina yoyote kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa picha au mfumo mwingine wowote.

MOAT inaeleza kuwa inatambua jitihada za serikali katika kukusanya kodi kwa ajili ya mipango ya maendeleo kwa wananchi, hata hivyo imebainisha kuwa kuanzishwa kwa kodi hii kunakinzana na juhudi za kuwapunguzia mzigo wa kodi wananchi wenye kipato cha chini.

Jumuiya hiyo inasema kuwa ukuaji wa mawasiliano ya simu katika muongo ujao utatoka maeneo ya vijijini hivyo uanzishwaji wa kodi hii ya sh.1,000 kwa kila mtumiaji wa simu kila mwezi utazuia juhudi zaidi za ukuaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini kwa sababu watu wengi ambao ni wenye kipato cha chini hawataweza kumudu huduma ya mawasiliano.

Maoni ya wananchi

Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, Bw.Yohana Noah anasema anasikia tu iliongelewa bungeni kuwa wananchi wanapaswa kulipia kadi za simu sh. 1,000 na hafahamu nini kinachoendelea ila anaamini serikali haijatenda haki kwa kuwa maisha ni magumu,.

“Tunalipa ankara za umeme, maji na ving’amuzi na hivi sasa hata kumiliki simu ya kiganjani imekuwa anasa, hii inashangaza sana,” alisisitiza.

Anasema kuwa kuna vyanzo vingi vya mapato ila anashangaa ni kwa nini watu wenye kipato cha chini wanakandamizwa.

Naye mkazi mmoja wa Gongolamboto Mzambarauni aliyejitambulisha kwa jina Amina Said anasema hana taarifa na kodi hiyo na hajui chochote kuhusiana na hilo, ila baada ya kufafanuliwa kuwa kuna kodi ya sh. 1,000 kwa mwezi alisema, kodi inapaswa kuwepo kwa watu wanaofanyia biashara simu zao na sio hata kwa wale ambao hawana biashara yoyote na simu zao zaidi ya mawasiliano tu.

“Kodi hii ni aina nyingine ya ufisadi na inaonesha ni jinsi gani viongozi wetu hawana huruma kwa wananchi, hata kama wameamua kuweka kodi hii mbona hakuna uwazi ni jinsi gani itakuwa inakusanywa?” Anasema Bw. Sebastian Sungi wa Gongolamboto.

Anasema nchi ina vyanzo vingi vya mapato na hakukuwa na sababu ya kuanzisha kodi hii.

CCM

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye anasema kuwa CCM inapinga tozo hii kwa kuwa ni mzigo kwa wananchi na haikuzingatia tofauti ya vipato vya wananchi ambao wengi wao matumizi yao ni ya kiwango cha chini.

“Kama chama tawala hatuwezi kukaa kimya kwenye jambo ambalo tunaliona linawabebesha mzigo wananchi na huenda likarudisha nyuma maendeleo yao na Taifa, hivyo kuchelewesha jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla,” anasema Bw. Nape katika taarifa yake.

Anasema kuwa cha kushangaza ni kwamba serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na wabunge wengi ambao siku zote tumekuwa tukishuhudia bungeni kura zikipigwa wao huongoza kwa kusema ‘ndiyooooo...’ ni wa CCM, na kodi hii ilipata baraka za baraza la mawaziri ambalo ni la serikali ya CCM.

Hivyo kauli hii ya Nape imechelewa sana.

Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba akizungumza na gazeti hili hivi karibuni alisema kuwa suala hili linapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa ni nyeti na linagusa wananchi.

Anasema kuwa anakubali kwa dhati tozo hii itazamwe upya ili kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha na kumtaka Mbunge wa jimbo la Ubungo,John Mnyika kuacha kulifanya suala hili ni la kisiasa.

Hata hivyo inaonesha kuwa kauli hii ina mkanganyiko mkubwa kwa kuwa kwa mujibu wa maelezo ya Naibu Waziri wa Fedha, Bi. Salum, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilishirikishwa katika mchakato mzima wa kuipitisha kodi hii na hivyo inashangaza pale naibu waziri ambaye alishiriki kubariki kodi hii, kugeuka na kusema kodi hii ni mzigo kwa wananchi.

Kimsingi wananchi wanaeleza kuwa serikali ilikurupuka katika hili na yeye kama ambavyo ilikurupuka kwenye sheria ya fao la kujitoa, hivyo hivyo ni vizuri kutafutia ufumbuzi suala hili badala ya kulikwepa na kuwepo kwa lawama na manung’uniko yaliyotokana na tozo hii.

Imefika wakati kwa serikali kujenga utamaduni wa kufanya tafiti kwanza kabla ya kuanzisha tozo mbalimbali na sio kus

No comments:

Post a Comment