19 July 2013

KAPOMBE HUYOO UHOLANZI


Na Fatuma Rashid

BEKI wa timu ya Simba, Shomari Kapombe anatarajia kuondoka nchini leo jioni kwenda nchini Uholanzi kwa ajili ya kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kapombe alisema anaamini kwa jitihada zake na kumuomba Mungu atafanikiwa kufuzu majaribio hayo.
 Kapombe alisema amejiandaa vya kutosha na anaamini Watanzania wengi wanamuombea na anajua licha ya soka kuwa na changamoto nyingi, hususan kwa soka la kulipwa, lakini anaamini atazishinda.Safari ya mchezaji huyo, imepewa baraka na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Akizungumzia safari ya Kapombe, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema mchezaji huyo amekubaliwa baada ya klabu yake ya Simba kuwasilisha barua rasmi ya kumuombea ruhusa
  "TFF tumempa ruhusa kwani mara baada ya kupata barua kutoka Simba, tuliamua kuwasiliana na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen kwa kuwa mchezaji yupo na timu ya taifa Mwanza ambaye naye alikubaliana na suala hili," alisema.Kutokana na safari hiyo, Kapombe hatakuwepo katika mechi ya marudiano ya kutafuta nafasi ya kucheza Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN), dhidi ya Uganda.Katika mechi ya awali iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stars ilinyukwa bao 1-0 hivyo ili isonge mbele katika michuano hiyo itatakiwa kushinda mabao 2-0 au zaidi.

1 comment:

  1. Kila la heri Kapombe,umeanza vizuri na inshallah Mungu akujalie umalize vizuri ili balozi wetu huko.

    ReplyDelete