24 July 2013

JWTZ WA DARFUR WAZIKWA, ZANZIBAR WAPATA AJALI Mwajuma Juma, Zanzibar na Cresensia Kapinga, Songea
ASKARI saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa katika shambulio la kushtukiza mjini Darfur, nchini Sudan wamezikwa jana katika mikoa mbalimbali walikokuwa wakitoka.
Askari hao walizikwa kwa heshima zote za kijeshi kwenye mazishi yaliyoongozwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimikoa. Visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, aliungana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa vikosi vya ulizi na usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, wafiwa na wananchi katika mazishi hayo
. Askari kutoka Zanzibar waliozikwa ni Shaibu Othman na Mohamed Juma Ally.Dkt. Shein akiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, walishiriki katika dua ya hitma iliyosomwa kwa ajili ya askari hao na kuwasalia katika Msikiti wa Noor Mohammad (S.A.W), Mombasa kwa Mchina, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Wananchi,wafiwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali walihudhuria hitma hiyo. Awali Dk. Shein aliweka saini kwenye vitabu vya maombolezi kwa ajili ya marehemu hao.Baada ya kumaliza dua na swala kwa ajili ya askari hao, Dkt. Shein, aliongozana na viongozi wengine na wananchi kwenda kwenye Makaburi ya Mwanakwerekwe kwa ajili ya mazishi. Katika makaburi ya Mwanakwerekwe mamia ya wananchi walijitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwaaga marehemu hao ambapo wote wamezikwa katika eneo hilo maarufu la Makaruni liliopo Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Makaburi ya askari hao yalichimbwa jirani. Miili ya askari hao ilizikwa kwa taratibu zote za kijeshi na baadaye kufuatiwa taratibu za kidini.
Baada ya mazishi kumalizika zilizomwa salamu za Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete. Katika salama zake Rais Kikwete, alimuomba Mungu aziweke roho za marehemu hao mahali pema peponi.

Rais Kikwete, alisema msiba huo ni wa Taifa zima na si kwa upande wa Tanzania pekee, bali ni Afrika na dunia nzima kwa ujumla.Nao wanafamilia na wazazi wa marehemu hao, walitoa shukrani zao za dhati kwa Serikali zote mbili kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa kuhakikisha marehemu hao wanafika kwenye familia zao na kuzikwa kwa taratibu zote.

Mjini Songea simanzi, vilio na majonzi vilitawala wakati wa mazishi ya askari wa JWTZ, Rodney Ndunguru, wa kikosi cha makomando cha 92 KJ Ngerengere mkoani Morogoro.Mazishi hayo yalihudhuriwa na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Ruvuma wakiwemo askari. Mazishi hayo yalifanyika jana kwenye makaburi ya Mjimwema Manispaa ya Songea.

Katika mazishi hayo yaliyongozwa na Paroko wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea Parokia ya Mjimwema, Padre Noel Duwe. Katika mahubiri yake alitaka Watanzania kutochezea amani na kwamba utulivu walionao Watanzania unahitajika kulindwa kwa namna ya aina yoyote na si vinginevyo.

Padre Due alisema kwa wale wote wanaotaka kuchezea amani na utulivu tulionao wanapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa kuwa Watanzania hawakuzoea vurugu.Kwa upande wake msemaji wa familia ya marehemu, Ndunguru alisema familia imepata pengo kubwa kwa kuondokewa na kijana wao na ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuisaidia.

Alisema kuwa Rodney amefariki akiwa na miaka 28 ambapo kimsingi kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa famila kwani katika uhai wake ilikuwa faraja kwa ndugu.

Wakati huo huo, habari ambazo gazeti hili limepata wakati likienda mtamboni zinaeleza kuwa wanajeshi wa JWTZ waliokuwa wakitoka kwenye mazishi ya wenzao waliouawa mjini Darfur wamepata ajali mjini Zanzibar, eneo la Mwanakwerekwe, umbali wa mita 300 kutoka kwenye makaburi.

No comments:

Post a Comment