12 July 2013

JK AKABIDHI NYUMBA WAATHIRIKA WA MAPOROMOKO


 Na Florah Temba, Same
SERIKALI imekabidhi nyumba nane za waathirika wa maporomoko ya ardhi yaliyotokea Novemba 2009 katika Kijiji cha Goha Kata ya Mamba Miamba wilayani Same mkoani Kilimanjaro ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati alipotembelea eneo hilo baada ya kutokea kwa maporomoko.
Katika maporomoko hayo watu 24 walipoteza maisha huku kaya 8 zikikosa mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kuathirika na maporomoko hayo.

Akikabidhi nyumba hizo jana kwa niaba ya Rais Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliutaka uongozi wa wilaya kuhakikisha nyumba hizo zinabaki kuwa mali ya watu hao kama ilivyokusudiwa na Serikali na si vinginevyo.
Gama alitoa agizo kwa uongozi wa wilaya kusimamia nyumba hizo ili wasiwepo watu wa kubadili umiliki wa nyumba za wahanga hao na kwenda kwa umiliki wa watu wengine.
"Ninauagiza uongozi wa wilaya kuhakikisha unasimamia nyumba hizi ili zibaki kuwa mali ya wahanga na wasiwepo watu wa kuja kuwadanganya hawa watoto wadogo na kuwapatia fedha kununua nyumba hizi na kubadili umiliki," alisema Gama.
Gama aliongeza kusema kuwa ni vyema wilaya ikaweka utaratibu wa kuwepo kwa rekodi halali ya umiliki wa nyumba hizo kisheria ikiwa ni pamoja na wahanga hao kuhakikisha wanazitunza na kuzilinda ili ziweze kudumu.
Akitoa taarifa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Joseph Mkude alisema katika utekelezaji wa ujenzi wa nyumba hizo Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kilituma fedha shilingi milioni 162. 3 huku Benki ya NMB ikitoa mchango wa saruji mifuko 100 na mabati 400 vyenye thamani ya shilingi milioni 9.7

No comments:

Post a Comment