22 July 2013

ISLAMIC BANKING INACHOCHEA MAENDELEO NCHINI - SERIKALI



 Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewatoa hofu Watanzania ikiwataka kutosita kujiunga na kutumia huduma za kifedha zinazofuata kanuni za Kiislamu ikiitaja huduma hiyo kama mkombozi kwa wananchi walio wengi.Akizungumza wakati wa hafla ya futari kwa wateja iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya Salum alisema bidhaa hiyo imeletwa katika muda mwafaka.

"Huduma hii hufuata sheria na kanuni za Kiislamu. Ni huduma inayojali na kufuata maadili na ni furaha kwa Serikali kuona kwamba hatimaye maadili sasa yanaingia hadi kwenye huduma za kifedha."Maadili yakiwa imara katika jamii, tunatarajia pia kupata uchumi imara wenye kukua na viwanda vyenye kuzalisha bidhaa na huduma zenye kukidhi mahitaji ya wote," alisema.
Bi. Saada aliiomba NBC kuendelea kubuni na kuwaletea Watanzania huduma nyingine zenye kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja, wakubwa kwa wadogo, hususan mikopo kupitia huduma ya kibenki ya Kiislamu.Aliitaka pia benki hiyo kutoa elimu kwa Watanzania ili waweze kufahamu kiundani faida ya huduma hiyo ambayo iko wazi kwa yeyote bila kujali itikadi au imani yake ya kidini.
"Ni matumaini yetu kwamba wengi watafaidika kutokana na huduma hii, hasa mtakapoanzisha huduma ya mikopo isiyo na riba kwa mujibu wa kanuni za Kiislamu," alisema.Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bi. Mizinga Melu alimuahidi Naibu Waziri kwamba benki hiyo haitaacha mipango yake ya kuisaidia Serikali kutekeleza kauli mbiu yake ya 'maisha bora kwa kila Mtanzania'. "Tumejizatiti katika hili na kama unavyojua na sisi kauli mbiu yetu ni maisha bora kwa kila mtanzania hivyo tutayatumia matawi yetu yaliyoenea nchi nzima kuwafikia Watanzania kokote waliko na kuwapelekea huduma bora za kifedha ambazo hawajawahi kuzipata wakati wowote," alisema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma ya Kibenki ya Kiislamu, Bw. Yassir Masoud lisema kuwa muda si mrefu NBC itaanzisha huduma za mikopo kupitia bidhaa hiyo, akisisitiza kwamba wanaelewa kuwa watu wengi wanaisubiri kwa hamu kubwa.
Aidha Huduma ya Islamic Banking ya Benki ya NBC ilizinduliwa mwezi Mei mwaka 2010 hapa nchini.

1 comment:

  1. Je huu si udini? Je ifunguliwe Christian Banking? Hii ni nchi isiyo na dini . Raisi Kikwete Unaipeleka wapi Tanzania hii. Ukiwa mwislamu unayeingiza mambo ya Udini. hatupUarabu. Tuko Tanzania hapa au umesahau kama inatakiwa uwe Raisi wa bila dini yeyote? Pia kwenye Vyama. Ulikemea Chadema na mafunzo kwa Vijana wao. Mbona umekaa kimya kwa CCM? jambo jingine Kama Amiri Jeshi, matukio yote ya mauaji hadharani kupitia vyombo vya dola, Umeshindwa kutoa tamko kwa Polisi, JwT, na bomu ambalo jeshi lako la polisi wakisingizia limetupwa kwa makosa. Sasa wewe ni kiongozi wa Amani au vipi? Kama umezidiwa na jeshi au unaliogopa kwa nini usijiuzuru ukaiacha nchi kwa amani. Wapishe wenye moyo wa kuipigania nchi hii na kuleta maendeleo na amani kwa wote. Jeshi unalo na sasa majambazi yanateka mabasi. Lakini upo busy mitaani kwa mambo yasiyo na uzito kila siku. Naona umezidiwa na kazi, basi omba msaada ukapumzike. Taifa linaangamia na huku uko mitaani kukunena yasiyo na msingi. Umetawala mda mrefu, na umefanya mabadiliko mengi na unashindwa kuyamudu.

    ReplyDelete