19 July 2013

HUJUMA ZAENDELEA KUIANDAMA TANESCO


Na Florah Temba, Hai

SHIRIKA la umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika kipindi cha Januari hadi Julai 17 mwaka huu,kutokana na wizi wa nyaya za umeme zenye urefu wa mita zaidi ya 5,000.
Hayo yalibainishwa jana wilayani Hai na Ofisa Usalama wa TanescoMkoa wa Kilimanjaro, Edwin Isaac wakati wa kutolewa kwa taarifa ya wizi wa nyaya za umeme zenye urefu wa mita 1,000 katika Kata ya Kia, Wilaya ya Hai mkoani humo tukio ambalo limetokea usiku wa kuamkia Julai 17 mwaka huu.

Isaac alisema katika kipindi hicho cha Januari hadi Julai mwaka huu kumekuwepo na matukio zaidi ya 10 ya wizi wa nyaya za umeme katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, na kwamba matukio hayo hutokea nyakati za usiku na kulisababishia shirika hilo kupata hasara kubwa."Hujuma hizi za wizi wa nyaya za umeme zimekuwa zikisababisha hasara kubwa na madhara makubwa kwa wananchi, kwani zinapoibiwa nyaya kama hizi watu wanaohudumiwa na shirika hili katika laini iliyoibiwa hukosa umeme kwa muda na kulilaumu shirika huku tatizo likiwa ni watu wachache wasio na huruma," alisema Isaac.
  Kutokana na hali hiyo, Isaac aliiomba Serikali kufuatilia kwa karibu matukio hayo ili kubaini liliko soko la nyaya za umeme na mtandao unaohusika na vitendo hivyo hatua ambayo itasaidia kupunguza matukio hayo ya wizi na kuokoa fedha ambazo hupotea kwa kurudisha nyaya mpya za umeme mara baada ya kutokea kwa wizi.
Alisema kuna haja pia ya Serikali kutazama upya sheria inayotumika kwa sasa kuwabana watu wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ikiwemo wizi wa nyaya za umeme na kuhakikisha zinawekwa adhabu kali kwa wale watakaobainika, ili kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa likisababisha hasara kubwa kwa shirika hilo."Tunaiomba Serikali iongeze ma k a l i kwe n y e s h e r i a n a kuhakikisha inatoa adhabu kali kwa wale watakaobainika kuiba nyaya za umeme, lakini pia tunaomba kesi za aina hii zisichukue muda mrefu mahakamani, zisikilizwe kwa haraka na adhabu zitolewe ili kuwa fundisho kwa watu wengine ambao wanajihusisha na vitendo hivi," alisema.

Aliongeza kuwa kuna haja pia ya Serikali kufuatilia biashara ya vyuma chakavu na kuchunguza vyuma ambavyo vimekuwa vikipelekwa katika biashara hizo, ili kubaini miundombinu ya umeme ambayo imekuwa ikiibwa na kuuzwa kama vyuma chakavu.Akitoa taarifa za tukio la wizi wa nyaya za umeme lililotokea Julai 17 mwaka huu Meneja wa TanescoWilaya ya Hai, James Chinula alisema nyaya zenye urefu wa zaidi ya mita 1,000 zilizoibiwa zinathamani ya zaidi ya shilingi milioni 40.

Alisema tukio hilo ambalo lilitokea Julai 17, saa saba za usiku katika laini inayoanzia Kiungi hadi Mererani Kata ya Kia Wilaya ya Hai lilisababisha baadhi ya maeneo ikiwemo Mererani kukosa huduma ya umeme.Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga alisema wizi wa miundombinu ya umeme katika wilaya hiyo umeendelea kushika kasi, hali ambayo imekuwa ikilisababishia taifa kupata hasara kubwa.

Kutokana na hali hiyo mkuu huyo alisema kwa sasa wanampango wa kuwashirikisha wananchi katika kudhibiti tatizo hilo, ambalo limeonekana kuendelea kukithiri katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Aidha mkuu huyo aliwataka pia wananchi wilayani humo kutoa ushirikiano kwa Tanesco na kuhakikisha wanawafichua wahusika wote wa wizi wa miundombinu ya umeme ikiwemo nyaya, ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria na kukomesha tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment