Na Reuben Kagaruki
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia,Prof. Patrick Makungu, amesema mpango wa utekelezaji,
uanzishaji wa Anwani za Makazi na Misimbo (alama) ya posta itasaidia
kurahisisha mawasiliano na kuchochea maendeleo nchini.
Profesa Makungu
alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam mara baada ya kufungua semina ya siku moja ya wakurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu wa wizara hiyo katika kuwajengea uelewa pamoja na kuhamasisha
matumizi ya anwani za makazi na misimbo ya posta.
Alisema hatua
hiyo ni muhimu katika ulimwengu wa sasa katika kurahisisha mawasiliano na
maendeleo.
Alibainisha
kuwa jiji la Dar es Salaam ni muhimu zaidi kwa sababu huchangia asilimia 70 ya
mapato yatokanayo na kodi.
Alisema awamu
ya kwanza ya mpango huo kwa jiji la Dar es Salaam ilizinduliwa rasmi na
Septemba 14, 2012 na Rais Jakaya Kikwete ambapo utekelezaji wake unahusisha
serikali, taasisi za serikali, taasisi zisizo za kiserikali na sekta binafsi.
Profesa Makungu
alisema, Mkoa wa Dar es Salaam umeanza kutekeleza mpango huu ambapo tayari
baadhi ya wizara na taasisi zimeanza kutumia misimbo hiyo ya posta na wananchi
wahamasike kuupokea.
Alisema, kamati
tendaji kwa kushirikiana na wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia na
mamlaka ya mawasiliano Tanzania, Shirika la Posta, Manispaa zote za Mkoa wa Dar
es Salaam na wadau mbalimbali wameandaa mipango ya utekelezaji katika jiji
zima.
Naye Mkurugenzi
wa Masuala ya Posta, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Rehema Makubwi, alisema
programu hiyo itasaidia huduma za posta kuimarika.
"Pia
inasaidia katika kutambua wananchi walipo; na wakati wa dharura ya majanga kama
magonjwa na moto kupata huduma kwa urahisi na huu ndiyo mfumo nzuri zaidi
katika kukabili masuala haya.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Uchukuzi, Issa Nchasi,
alisema mpango huo katika wizara yake umefika wakati mwafaka.
"Hii itaongeza ufanisi katika Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari na Maziwa (TPA), mizigo au bidhaa kumfikia mmiliki moja
kwa moja bila ya kubahatisha alipo kutokana na kuwepo kwa anwani za
uhakika,"alisema.
No comments:
Post a Comment