22 July 2013

CRDB KUTHAMINI IMANI ZA WATEJA Na Allan Ntana, Tabora
UONGOZI wa Benki ya CRDB tawi la Tabora umesema utaendelea kuheshimu na kuthamini misingi ya maadili na imani za wateja wake kwa kuunga mkono utekelezaji wake. Meneja wa tawi la CRDB Tabora, Sdney Bakari alisema hayo kwenye taarifa yake aliyoisoma kwenye hafla ya futari ilifanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma,(TPSC) tawi la Tabora.

Bakari alisema hafla hiyo ya futari ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa waumini wa dini zote ni miongoni mwa ushiriki wa Benki ya CRDB kwani benki hiyo imeshafanya shughuli nyingi za kijamii kwa kushirikisha taasisi kadhaa. Aidha, meneja huyo alisema CRDB imeshafanya shughuli hizo ikiwa ni pamoja na misaada ya vifaa na vyakula kwa taasisi zinazosaidia makundi ya watu wenye uhitaji.
"Makundi ambayo hadi sasa CRDB imekuwa ikitoa misaada na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali ni yatima,wagonjwa,waliokumbwa na majanga na walemavu," alisema Bakar. Alisema benki hutenga kiasi kidogo cha faida yake kusaidia jamii na hii imekuwa ni moja ya sera za benki kila mwaka kwani wanathamini mafanikio yao yanayotokana na wateja wake na jamii inayowazunguka.
Akizungumzia baadhi ya huduma zake kwa wateja wake alisema, wameamua kusogeza huduma ijulikanayo kama 'Fahari Huduma' ambayo ni huduma inayomwezesha mteja wa CRDB kupata huduma za benki kama kujua salio, kuweka na kutoa fedha, kupokea fedha, kutuma fedha na huduma za ufunguaji akaunti kupitia mawakala maalumu. Bakar alisema zaidi ya hapo hadi sasa CRDB imeendelea kutanua wigo ili kusogeza huduma kwa wateja wake ambapo hadi sasa wanatarajia kufungua matawi wilaya za Sikonge na Urambo huku kukiwa na tawi jipya lililoanzishwa hivi karibu mkoani hapa.
Katika hafla hiyo meneja huyo alisema kuwa wanatarajia kuchangia kiasi cha sh milioni 2 kuchangia shughuli za Baraza Kuu la Idd linalotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Tabora. Naye Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Shaban Salum katika salamu zake aliipongeza Benki ya CRDB kwa hatua hiyo muhimu ya kuungwa mkono najamii nzima.
Shekhe Salum alisema sehemu ya hiyo ya hafla ya futari iwe ni sehemu ya kumtaka Mwenyezi Mungu msamaha ili tupate malipo, heri nyingi na Baraka. Alisema mwenyezi Mungu alituletea mwezi bora na tuwe waungwana naye atusamehe zambi zetu.

No comments:

Post a Comment