MAMLAKA ya chakula na Dawa (TFDA)
imeteketeza tani 6.143 za bidhaa mbalimbali ikiwemo chakula, dawa za binadamu,
mifugo pamoja na vipodozi katika kipindi cha mwaka 2012/13.Hayo
yalibainishwa hivi karibuni mkoani hapa na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Chakula
na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati, Florent Kyombo wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari na kuongeza kuwa bidhaa hizo zilikuwa na thamani ya zaidi
ya sh.milioni 92.
Kyombo alisema
kuwa bidhaa hizo ziliteketezwa katika Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na
Kigoma ambapo katika zoezi hilo jumla ya vibali mia tatu kumi na tisa vya
kuteketeza bidhaa vilitolewa kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 ambayo ni sawa na
asilimia 638 ya lengo la kuteketeza shehena 50 kwa mwaka wa fedha uliopita.Aidha Kyombo aliwataka wananchi kuwa na
uelewa wa kusoma tarehe za mwisho wa matumizi ya bidhaa mbalimbali wanazonunua
madukani ili kujua muda wake wa matumizi kama umemalizika.
Pia aliwataka wananchi kutoa
ushirikiano kwa kutoa taarifa TFDA iwapo watagundua kuwa kuna maduka yanauza
bidhaa ambazo ni feki ama zimemalizika muda wake ili hatua stahiki zichukuliwe.Hata
hivyo alitoa wito kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanafuata Sheria
za TFDA ikiwa ni pamoja na kulipia majengo yao kwa wakati na kuwa na vibali vya
kuendeshea biashara zao ili kuepuka usumbufu
.
No comments:
Post a Comment