22 July 2013

ASHAMBULIWA KWA MAPANGA HADI KUFA Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa Kijiji cha Nyanduturu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Ally Makakatau (46), amefariki baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kukatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Juma Ally alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 19 saa 7:30 usiku baada ya watu wapatao sita kuvamia nyumbani kwa Makakatau na kuvunja mlango wa nyumba aliyokuwemo kisha kumshambulia kwa kutumia mapanga kichwani, mkononi na miguuni.

Ally alisema kuwa watu hao walivamia katika nyumba hiyo na kumtaka marehemu kuwapatia fedha ambazo alikuwa amepata baada ya mauzo ya mafuta aliyokuwa amefanya jioni ya siku hiyo na alipokataa kutoa ndipo waliamua kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili."Watu hao mbali ya kuvunja nyumba ya mfanyabiashara huyo, pia walivunja duka na kuchukua pesa taslimu shilingi m 2,800,000 ambazo zilikuwa ni za mauzo ya mafuta," alisema Ally.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linawasaka watu hao na kuwataka wananchi kuwapatia taarifa zitakazo saidia kuweza kuwapata waliohusika na tukio hilo.Aidha alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Katika tukio lingine, Polisi Mkoa wa Pwani inawashikilia watu 20 raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchi bila kibali.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 7:30 usiku eneo la Mkuranga Mjini Wilaya ya Mkuranga.Kamanda huyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watu hao walikamatwa na askari waliokuwa doria wakiwa wanatembea kwa makundi katika eneo la Mkuranga Mjini.
Alifafanua kuwa watu hao baada ya kuwahoji walibaini kuwa walishushwa kwa gari na kuamua kutembea ili kuweza kuvuka kwenye eneo lililokuwa na kizuizi cha polisi.Aidha, aliwataka wananchi waendelee kutoa taarifa kwa polisi pindi wanapowatilia mashaka wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.

No comments:

Post a Comment