05 February 2013

Wajasiliamali wanawake TWCC watakiwa kukuza masoko


Na David John

MKURUGENZI wa Wizara ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kagyabukama Kiliba amewataka wajasiliamalli wanawake kutumia fursa zilizopo katika jumuiya hiyo ili kuweza kukuza masoko ya biashara zao.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika hafla ya kufunga mafunzo ya semina ya ujasiliamali kwa kikundi cha wanawake wajasiliamali wanachama wa chemba ya wanawake wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambao wapo chini ya usimamizi wa Taasisi ya trade Mark Afrika mashariki.

Kiliba alisema kuna haja kubwa ya wanawake nchini kujenga timu ya pamoja katika kufanya biashara zao ili kufaidika na soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa pamoja kuitumia vizuri ofisi ya jumuiya hiyo hapa nchini.

"Napenda kusisitiza kuwa kuna umuhimu wa kufanya biashara kwa umoja hivyo na wasihi wanawake zaidi kujiunga katika vikundi kama hivi ili kuweza kuwa na sauti moja  ambayo itawafanya kukabiliana na changamoto zilizopo huko mipakani,"alisema.

Alisema bila kuwa na sauti moja ya Serikali ama Jumuiya Afrika Mashariki haitaweza kujua matatizo yanayowakuta wafanyabiashara hasa wajasiliamali wanawake hivyo wakiwa pamoja wataweza kutatua kwa urahisi matatizo watakayokabiliana nayo  katika biashara zao kuliko kila mmoja kufanya kazi peke yake.

"Natumaini kuwa mafunzo haya yamewapa ujasiliamali mkubwa na uthubutu wa kusema na mimi nitaaza na ni vizuri mkakumbuka kuwa hatua mia lazima ziaze na hatua ya kwanza nyie mnaopambana hiyo ndiyo mifano hai ya kueleza na kuwabadilisha kuwafunza, wafanyabiashara wanaochupukia na wenye uoga wa kuthubutu kwenda nje ya Tanzania kufanya biashara, "alisema.

Alisema Ofisi ya Wizara ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika mashariki ipo wazi kwa ajili kusikiliza matatizo ama changamoto ambazo zinazojitokeza katika shughuli zao hasa kwa upande wa mipakani.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TWCC, Fatuma Riyami alisema mafunzo yalilenga namna ya kuuza bidhaa zao katika soko la Afrika Mashariki,lakini pia kujua sheria za jumuiya ya soko hilo ili kuweza kukabiliana na changamoto za mipakani.

Alisema wakati mwingine wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kutojua sheria za mipakani hivyo kupitia mafunzo hayo wameweza kufundishwa namna ya kuweza kukabiliana na changamoto hizo pindi wanapokwenda kufanya biashara hizo.

"Kuna wanawake ambao waliaza mapema kuingia katika soko lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto na hasa za kutojua sheria za jumuiya hivyo naamini hawa walioshiriki mafunzo haya watakuwa wamejua namna yakukabiliana nazo, "alisema.

No comments:

Post a Comment