05 February 2013

Viongozi, wanachama 21 CHADEMA wahamia NCCR


Na Rashid Mkwinda, Mbeya

VIONGOZI na wanachama 21 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Mbeya, jana walitangaza kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi.


Walisema sababu kubwa iliyowafanya waondoke CHADEMA ni chama hicho kutekeleza matakwa ya viongozi wawili Mwenyekiti Bw. Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa.

Viongozi na wanachama hao walitangaza uamuzi huo katika mkutano wao na waandishi wa habari wakidai kuchoshwa na
tabia ya kufukuzana ndani ya chama bila sababu za msingi.

Walisema CHADEMA hakiwezi kufanya mageuzi ya kweli kutokana na ubadhirifu pamoja na ukiritimba uliopo kwa
viongozi wa Taifa Bw. Mbowe na Dkt. Slaa.

“Tumeondoka kwenye ukiritimba wa kisiasa, wenzetu wamezoea vurugu, kulazimishwa maandamano na kufukuzana katika chama, tumejiweka pembeni na kuja katika mageuzi ya kweli,” alisema
Bw. Moses Mwasubila aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA jijini humo.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Kata ya Isyesye, Bi. Sara Mwasyeba alisema uongozi wa chama hicho unapuuza maoni ya wanachama wa
ngazi ya chini na kufanya walitakalo bila kuwashirikisha.


Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Kata ya Isyesye, Bw. Emanuel Ngogo alisema amekihama chama hicho kwa hiari yake baada ya kuona hakina nia ya dhati ya kuwasaidia Watanzania bali viongozi wachache ndio wanaojinufaisha.

Akizungumzia msimamo wa NCCR-Mageuzi na mikakati yake ya kurejesha heshima na hadhi kwa wananchi, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho na mshauri wa kisiasa Bw. Danda Juju, alisema sera za chama chao zimelenga kuwakwamua Watanzania waondokane na ukiritimba wa kisiasa nchini.

“NCCR-Mageuzi inasimamia kwa dhati rasilimali za Watanzania hasa kwa kuwekeza kwenye kilimo na elimu kwa wanawake, hivi sasa vyama vingi vya siasa vinatekeleza sera hii,” alisema.

Wimbi la waliokuwa viongozi wa CHADEMA kuhamia vyama vingine limekuja siku chache baada ya aliyewahi kuwa Katibu wa chama hicho mkoani humo, Eddo Mwamalala, kutofautiana na viongozi, wanachama na kuhamia NCCR-Mageuzi.

No comments:

Post a Comment