05 February 2013

TTCL yateuliwa kusimamia Mkongo wa Taifa


Na Rose Itono

KAMPUNI ya Simu nchini (TCCL), imeteuliwa na Serikali kuwa Meneja wa Mkongo wa Taifa ili kuleta mabadiliko ya kiutendaji
na kiufanisi.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa kampuni hiyo, Dkt. Zaipuna Yonah, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.

Alisema kuteuliwa kwa TTCL katika nafasi hiyo, kutaiwezesha kampuni hiyo kuendeleza Mkongo wa Taifa kwa kutumia vigezo vya utaalamu na miundombinu yao iliyoenea nchi nzima.

“Serikali ina imani kubwa na kampuni yetu ambayo inafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa ili kukidhi matarajio ya Serikali,” alisema na kuongeza kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa mkongo huo, Taifa litapata mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi.

Aliongeza kuwa, mkongo huo una umuhimu mkubwa hata kwa
nchi jirani za Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na Uganda
ambazo zinautegemea ili kuunganishwa na mikongo ya
kimataifa baharini yenye vituo vilivyojengwa Dar es Salaam.

Alisema kampuni za mawasiliano nchini Kenya, pia zimeanza kuunganishwa katika mkongo huo wakati kampuni zilizopo nchini Msumbiji, zinakamilisha taratibu za ujenzi kwenda mpakani ambako mkongo wa Taifa umefika ili ziweze kuunganishwa.

Dkt. Yonah alisema faida za mkongo huo tayari zimeanza kuonekana ambazo ni kuongezeka kwa ubora na kazi ya
matumizi ya mtandao wa intaneti na utoaji huduma za
elimu mtandao kwa baadhi ya taasisi za elimu.

“Kimsingi Serikali imeanza kukidhi matarajio ya Serikali kuziba pengo la matumizi ya Tehama kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hatimaye kukuza uchumi wetu,” alisema.

Alisema changamoto kubwa iliyojitokeza ni usalama wa miundombinu ambayo imepita maeneo mbalimbali ya makazi ya watu, mashambani, misituni, hifadhi za wanyama kama Katavi na maeneo mengine.

Aliwataka wananchi kuitunza rasilimali hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ambapo Serikali imetumia gharama kubwa kuwekeza kwenye mkongo.

No comments:

Post a Comment