18 February 2013
TEF, MCT walaani kududio la Ofisi ya Bunge
Na David John
JUKWAA la Wahariri nchini (TEF), jana limetoa tamko lao
siku chache baada ya Katibu wa Bunge kudai kuwa, ofisi hiyo
inakusudia kuzuia urushwaji wa matangazo ya moka kwa moja
katika vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Kusudio hilo lilitangazwa na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah ambaye alidai kuwa, hali hiyo imelenga kudhibiti
vurugu za wabunge waanaodaiwa kutafuta umaarufu.
Alisema baadhi ya wabunge hawataki kuzifuata kanuni za Bunge hivyo kufanya vurugu na vituko wakijua wanachozungumza kinarushwa moja kwa moja katika televisheni.
Pia Dkt. Kashililah alidai ni kosa kwa wapigapicha kuwapiga picha wabunge wakiwa wamesinzia ndani ya ukumbi wa Bunge hivyo ofisi yake inawasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kupata njia ya kurusha matangazo hayo ambayo yamehaririwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TEF, Bw. Absalom Kibanda, alisema hatua
hivyo inawap shaka na pengine ni ishara ya mwendelezo ya
kinachoonekana kama jitihada mpya za kuuminya uhuru
wa habari nchini.
“Tunashangaa Bunge la Tanzania limejifunza wapi siasa za kufunika mambo yanayowahusu wananchi likijua wanaofuatilia vikao hivyo ndio walipa kodi na wapiga kura wa wabunge ambao uongozi wa Bunge unataka kuwalinda.
“Tangazo hili ni kati ya mambo ya bahati mbaya yanayoikumba
nchi yetu kwa sasa wakati ambao dunia inahimiza uwazi hasa
katika vyombo vya uamuzi,” alisema.
Bw. Kibanda aliongeza kuwa, Tanzania imeto katika mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu hadi 1992, ambao uliifanya Serikali, Bunge na Mahakama kuendeshwa kwa usiri mkubwa.
Alisema mara zote usiri ni chimbuko la matumizi mabaya ya madaraka pia ni kinyume na misingi ya utawala bora hivyo TEF inautaka uongozi wa Bunge kuachana na harakati hizo kwani hazitasaidia kukuza demokrasia, uboreshaji maadili ya Bunge.
“Hatua hiyo itazidisha mashaka ya umma dhidi ya chombo hiki cha uwakilishi kwa wananchi kutaka kufanya kazi zao “gizani”, TEF inaamini kazi ya utangazaji, haipaswi kusimamiwa na uongozi
wa Bunge...wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo ni
dhambi kuweka usiri wa yale yanayozungumzwa,” alisema.
Aliongeza kuwa, jitihada zozote za kuwafungia wabunge ndani na kuhariri kazi wanazofanya na matamko wanayotoa ni ishara ya Bunge kutaka kuficha maovu, udhaifu wa mhimili huo au
mihimili mingine inayowajibishwa na wabunge.
Hatua hiyo itakuwa inawachimbia wabunge kaburi la kisiasa
kwani ndio wanaomulikwa kwa majibu ya maswali ambayo wanayauliza na hatua wanazochukua.
Bw. Kibanda alisema iwapo hali hiyo itatokea, jitihada za uwazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, zitafutika mbele ya jumuiya ya kimataifa.
“TEF tunaamini njia halisi ya kurejesha amani Bungeni ni uongozi wa Bunge kutenda haki kwa wabunge wote maana hata vikao vyao visiporushwa moja kwa moja, vurugu hazitaisha kama wahusika hawataamini kwamba wanatendewa haki,” alisema.
Aliongeza kuwa, Watanzania wamepata fursa ya kuwafahamu wabunge wao baada ya utaratibu wa kurusha matangazo ya moja kwa moja bungeni kuanza miaka ya 2000, hivyo jaribio la kuzuia
matangazo hayo ni kuturejesha enzi za Bunge mazongwe.
Tamko la MCT
Katika hatua nyingine, Baraza la Habari nchini (MCT), limesema kitendo cha Bunge kutaka kusitisha urushwaji matangazo ya moja
kwa moja kwa njia ya televisheni katika vikao vya Bunge ni
ulasimu na kutaka kurudisha nyuma demokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bw. Kajubi Mukanjaga, alisema hatua hiyo ni aibu kwa Taifa na wananchi waliowatuma wabunge wao kwenda kuwasemea kunyimwa haki ya kidemokrasia.
Alisema MCT kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari
nchini, wataendelea kupinga vikali hatua hiyo ambayo kimsingi imelenga kudhoofisha tasnia nzima ya habari.
“Kuhariri habari za wabunge ni kutaka kuendelea kutoa upendeleo ambao wanaoulalamikia wao wenyewe na wananchi wanaofuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni.
“Kitendo hiki hakina tija na hakizingatii taaluma ya uandishi wa habari nchini hivyo hatuwezi kukubali suala hili lipite hivi hivi na kuanzia leo, tunapingfa vikali hatua husika inayotaka kuchukuliwa kama kweli wameazimia kufanya hivyo,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment