01 February 2013

Sijaridhishwa na taarifa Waziri Pinda kuhusu gesi



Na John Mnyika

SIJARIDHISHA na taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na uamuzi wa Spika Anna Makinda bungeni jana kuhusu mgogoro wa gesi Mtwara, hatua ambazo zinadhihirisha kwamba nchi imefika hali hiyo kutokana na udhaifu wa Serikali na ombwe la kiuongozi na kiusimamizi ikiwemo wa kibunge.


Taarifa aliyoyatoa Waziri Mkuu jana imejibu baadhi tu ya madai ya wananchi, lakini pia imefafanua sehemu ndogo ya masuala ambayo niliyahoji bungeni Julai 27, 2012 lakini Serikali ikakwepa kutoa ufafanuzi.

Taarifa hiyo itawezesha kutuliza mgogoro kwa muda, lakini haijengi msingi wa ufumbuzi endelevu.

Sikubaliani na uamuzi wa Spika wa kubadili uamuzi wake wa awali alioutangaza wa kuunda kamati kufuatia maelezo ya Waziri Mkuu yasiyokuwa na vielelezo vyovyote kwa kuwa kufanya hivyo ni kulinyima bunge fursa ya kuisimamia Serikali ambayo ndio chanzo cha migogoro kuhusu gesi asili.

Spika alipaswa ikiwa amebadili uamuzi wa kuunda kamati ya kwenda Mtwara aunde Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ili ipitie vielelezo kubaini usahihi wa maelezo hayo ya Waziri Mkuu bungeni katika hali ya sasa ambayo nchi ina ombwe la kutokuwa na usimamizi wa kibunge kwenye sekta hizo nyeti kufuatia hatua yake ya kuvunja kamati iliyokuwepo bila kuunda kamati mbadala mpaka sasa.

Ikiwa hana nia ya kuunda kamati ya nishati na madini mpaka mwisho wa mkutano huu wa Bunge, basi anapaswa kurejea barua zangu nilizomwandikia na kutumia madaraka na mamlaka yake kuelekeza kamati nyingine ya Bunge kati ya kamati zilizopo hivi sasa iweze kukutana kwa haraka kuchukua hatua zinazostahili na kuwasilisha taarifa bungeni.

Kwa upande wangu, nafuatilia kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) kupata nakala kamili ya ufafanuzi huo na nitaeleza hatua za ziada ambazo nitazichukua kama mbunge na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.

Kwa ujumla, maelezo hayo hayana tofauti kubwa na yaliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Januari 2013, hivyo sikubaliani na Waziri Mkuu kueleza kuwa suala hilo limekwisha kwa maelezo matupu yasiyokuwa na vielelezo.

Maelezo hayo ya Waziri Mkuu yamedhihirisha kwamba iwapo Wizara ya Nishati na Madini ingetoa majibu bungeni kama nilivyohoji Julai 27, 2012, maandamano na migogoro iliyosababisha vifo na uharibifu wa mali Desemba 2012 na Januari 2013 yasingetokea hivyo ni muhimu waliosababisha hali hiyo wawajibishwe.

Maelezo hayo hayajaeleza hali halisi kuhusu kasoro katika ujenzi wa miundombinu ya gesi katika mradi unaoendelea hivi sasa kuhusu mitambo ya kusafisha gesi Madimba, ujenzi wa bomba kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam na mpango wa uzalishaji wa umeme mkoani Mtwara, na hivyo hatua zisipochukuliwa hivi sasa kurekebisha hali hiyo mgogoro utazimwa kwa muda mfupi lakini utaibuka mgogoro mkubwa zaidi baadaye.

Aidha, Waziri Mkuu hajatoa maelezo kamili kuhusu mipango ya matumizi ya gesi asili katika eneo la viwanda Bagamoyo na pia ujenzi wa Bandari ya Mbegani Bagamoyo, na mahusiano ya mipango hiyo na ile ya Mtwara na Dar es Salaam kuhusu matumizi ya gesi asili na bandari.

Ni muhimu maelezo ya ukweli, uwazi na ukamilifu yakatolewa.
Katika muktadha huo, Bunge kwa niaba ya wananchi linapaswa kutokuridhika tu na maelezo ya Waziri Mkuu kwamba suala hili limemalizika, bali lipewe nafasi ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 wa kuisimamia Serikali.

Spika wa Bunge atumie mamlaka yake kuelekeza Kamati mojawapo ya kudumu ya Bunge kushughulikia suala la gesi asili kama nilivyoomba katika barua zangu kwake za  Oktoba 2012 na Januari 2013 ambazo mpaka sasa hazijapatiwa majibu.

Kamati hiyo ipitie maelezo hayo ya Waziri Mkuu na kuitaka Serikali kuwasilisha vielelezo ikiwemo mikataba ili kurekebisha kasoro zilizopo katika mipango na mfumo wa utekelezaji wa miradi ya utafutaji, uvunaji, usafirishaji, uendelezaji na utumiaji wa gesi asili.

Mwandishi ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)


1 comment:

  1. KWAHIYO ULITAKA TUME IUNDWE ILI UPATE ULAJI JE KAMA USINGECHAGULIWA HIVI UNAJUA HIZO NI KODI ZA WANANCHI UNGETUAMBIA MUNAJITOLEA KAMA ENZI ZA UJAMAA TUNGEKUOMBEA BARAKA ZIWE NAWE

    ReplyDelete